Wanajeshi wa Brigedi Maalum wakiwa katika mazoezi
makali yaliyofanyika hivi
karibuni huko Goma Mashariki ya Demokrasia ya Kongo.
Na Mwandishi Maalum.
MISEHENI ya Kutuliza Amani katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ( MONUSCO) imetangaza kwamba kwa mara ya kwanza itaanza
kuitumia Brigedi Maalum (Force Intervention Brigade) katika kudhibiti eneo
maalum la usalama (security zone) kuzunguka mji wa Goma ulioko Mash
ariki ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na imewapa saa 48 waasi kusalimisha silaha
zao.
Taarifa iliyotolewa na MONUSCO na kusambazwa na
Idara ya Mawasiliano ya Umoja wa Mataifa jana jumanne, inaeleza kwamba watu
binafsi katika eneo la Kivu ya Magharibi ambalo linajumisha Goma na Sake na
ambao hawahusiki na vyombo vya usalama watapewa saa 48 kuanzia saa kumi jana
kwa saa za Goma (Jumanne ) kuzisalimisha silaha zao katika Misheni hiyo na
kujiunga na mchakato wa DDR/RR unaoratibu upokonyaji, usambaratishaji,
urejeshwaji makwao, kuwaunganisha na jamii na kuwapatia makazi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo zaidi ya wananchi
milioni moja wanaishi katika eneo dogo la Goma na Sake na kando kando ya
barabara ambayo inawaunganisha na kambi ya wakimbizi ya Mugungu ambayo ni
makazi ya muda ya watu karibu 70, 000 ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na
mapigano.
Kwa mujibu wa MONUSCO, tangu kati kati ya mwezi Mei
eneo hilo limeshuhudia mapigano ya mara kwa mara kutoka kwa kundi la M23 dhidi
ya majeshi ya Serikali ya FARDC ikiwa ni jaribio la wazi la kutaka kusonga
mbele kuelekea Goma na Sake.
“ Katika mashambulizi hayo, likiwamo la hivi
karibuni la Julai 14, M23 walitumia kiholela silaha zao za moto zikiwamo silaha
nzito ambazo zimesababisha wananchi kujeruhiwa” .
Taarifa hiyo imeongeza kwamba kundi hilo la M23
katika mashambulizi hayo limelenga pia Vituo vya Umoja wa Mataifa.
Aidha taarifa hiyo inabainisha kwamba eneo hilo
maalum la usalama ( security zone) litasaidia kudhibiti tishio la moja kwa moja
mbali na eneo la nje ya Goma na pengine eneo hilo linaweza kupanuliwa na
kurudiwa sehemu nyingine kutakako hitajika.
Tamko hilo la kutoa saa 48 kwa waasi kusalimisha
silaha zao linafuatia kuwasili katika eneo la Goma kwa Kamanda Mkuu wa MONUSCO,
Luteni Jenerali Carlos Alberto dos Santos Cruz, ambaye alitangaza kwamba
Misheni ya MONUSCO itaunga mkono jeshi la Serikali ( FARDC) katika kuanzisha
eneo la usalama kuzunguma eneo la Goma na vitongoji vyake.
Taarifa hiyo inamkariri Kamanda Mkuu wa MONUSCO
akiyapongeza majeshi ya serikali kwa kazi nzuri iliyofanya wiki iliyopita ya
kuwadhibiti M23. Ingawa anasema eneo la Goma na Sake bado limo katika mazingira
magumu sana na kwamba ni wajibu wa wahusika wote kuhakikisha wahalifu wote
hawaendelei kuhatarisha raia wa eneo hilo.
Kwa mwaka uliopitia , kundi la M23 pamoja na makundi
mengine yenye silaha yamekuwa yakipambana mara kwa mara na majeshi ya serikali
katika Mashariki ya Kongo, huku makundi hayo yenye silaha mwezi Novemba mwaka
jana yakiikalia Goma kwa muda.
Aidha mapingano ya hivi karibuni ambayo safari hii
yalihusisha pia kundi jingine la wanagambo wenye silaha lenye asili yake nchini
Uganda, yamesababisha zaidi ya wananchi 100,000 kuyakimbia makazi yao na hivyo
kuongeza mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo linalohusisha watu wengine 2.6
milioni ambao wameyakimbia makazi yao huku wengine 6.4 milioni wakihitaji
chakula na huduma za dharura.
Wakati huo huo, Kaimu Mkuu wa MONUSCO Bw. Moustapha
Soumare katika taarifa yake ametoa wito kwa pande zote kutafuta suluhu ya
kisiasa kwa matatizo ya DRC kupitia Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa
kuhusu amani, usalama na ushirikiano wa maendeleo katika DRC na eneo la Maziwa
Makuu uliopitisha mwezi wa Februari na viongozi 11 wa Afrika na Taasisi nne za
Kikanda na Kimataifa.
Aidha akasema katika kipindi hiki ambacho suluhu la
kisiasa linatafutwa MONUSCO itatumia nguvu iliyonayo kuwalinda wananchi dhidi
ya hatari zitokanazo na makundi ya waasi.

0 comments:
Post a Comment