
| Baadhi
ya waumini wa dini ya Kiislamu madhehebu ya Answar Sunna wakiungana na
waislamu wengine duniani katika ibada ya swala ya Idd katika Viwanja vya
Kiwanja Ng oma Jijini Mbeya leo asubuhi |



WAUMINI wa dini kiislamu madhehebu
ya Answar Sunna mkoani Mbeya wameswali swala ya Idd leo katika Viwanja vya
Kiwanja Ngoma na kuwataka Mashekhe kutotumia lugha za
uchochezi zinazojenga chuki baina ya Waislamu.
Akizungumza na umati wa waislamu
waliojumuika katika ibada hiyo ya kukamilisha kwa mfungo wa mtukufu wa
Ramadhani, imamu aliyeswalisha swala hiyo Shekhe Ibrahimu Bombo
alisema kuwa baadhi ya Mashekhe wakubwa wamekuwa wakitumia vyombo vya
habari kujenga chuki kwa waislamu.
Alisema, swala la ibada ni wajibu
kwa waislamu wote na kwamba yapo mambo ambayo waislamu wanatofautiana
katika kufanya ibada maalumu ambayo hutokana na uelewa na kwamba jambo
hilo halipaswi kuleta mgongano baina ya waislamu.
‘’Wapo mashekhe wa
taasisi fulani hujitokeza katika vyombo vya habari na kuleta kejeli dhidi
ya wengine kuhusu uelewa wa mambo, hakuna mamlaka iliyo juu ya sheria
inayopaswa kuwakejeli ama kuwatukana wengine, jambo hili lisipoangaliwa
linaweza kuleta chuki,’’alisema Shekhe Bombo.
Alisema uislamu unajengwa kwa
umoja na mshikamano na kama yapo mambo ambayo waislamu wanapishana yanapaswa kujadiliwa
kulingana na mafundisho ya dini hiyo badala ya kundi la watu fulani kujiona ni
bora zaidi ya kundi jingine.
‘’Sisi sote tunafuata mafundisho ya
Kitabu cha Koran na Hadithi za Mtume Muhammad (SAW) anayefuata mafundisho
haya kwa dhati hawezi kukurupuka na kukejeli wengine,’’alisisitiza
na kuongeza.
‘’Wanaohoji kwa nini tunaswali leo,
tunasema kuwa sisi tunaswali mwezi wa Kimataifa ambao dunia nzima
wanaswali,wale watakaoswali kesho hakuna anayewazuia na wala ninyi
msiwakejeli ambao leo bado wamefunga na wao hawapaswi kuwakejeli ninyi ambao
leo mnakula mchana,’’alisema.
Kwa upande wake Shekhe Rajab Nzunda
alisema kuwa Waislamu wanapaswa kufuata na kuendeleza mafundisho ya mwezi
mtukufu wa Ramadhani ambapo wengi waliamua kuacha maasi na kujikita katika
ibada.
‘’Mwezi wa Ramadhani umetufundisha,
uchamungu, hatupaswi kurejea tena katika maovu ambayo yalitakaswa na Mwezi
huu,tusirejee tena kufanya madhambi, tuendeleze ibada na uchamungu tuliodumu
nao kwa mwezi mzima,’’alisema Shekhe Nzunda.(STORI NA PICHA NA mkwinda blog)

0 comments:
Post a Comment