MIHADHARA ya
dini iliyokuwa imepigwa marufuku na Serikali imeruhusiwa kuendelea kwa
masharti ya kutojihusisha na mahubiri yanayolenga kupandikiza chuki
miongoni mwa Wakristo na Waislamu.
Serikali pia imewataka viongozi wote
wa dini kuwakataa na kuwapiga marufuku watu wanaojiingiza katika nyumba
za ibada huku wakiwa na malengo ya siasa.
Akizungumza katika kongamano la Umoja wa Wahadhiri wa dini za
Kikristo na Kiislamu Dar es Salaam juzi, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo
wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja alisema Serikali haiwezi kuingilia
shughuli za dini kama zinaendeshwa kwa ustaarabu bila kuvunja sheria.
Chagonja ambaye alimwakilisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk.
Emanuel Nchimbi alisema Serikali haijawahi kupiga marufuku mihadhara
yoyote inayoendeshwa bila kusababisha vitendo vya chuki na uhasama kwa
Watanzania.
Kuruhusiwa kwa mihadhara hiyo kumekuja ikiwa imepita zaidi ya miezi
minane tangu Serikali ilipopiga marufuku mihadhara hiyo nchi nzima ikiwa
ni hatua ya kukabiliana na machafuko ya dini yaliyokuwa yanalinyemelea
taifa.
Uamuzi huo ulichukuliwa siku chache baada ya baadhi ya waumini wa
dini ya kiislamu kujiandaa kuandamana kwenda Ikulu kutaka atolewa
rumande Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa
Ponda.
Katika kongamano la juzi, Chagonja aliwaasa viongozi hao kuwa na
mfumo mpya wa dhana ya uhalisia ya kutangaza dini na kuacha kukejeliana
kati ya dini moja na nyingine kuepuka vitendo vya chuki za dini.
Kiongozi wa Mihadhara ya Kiislam, Naibu Amir, Shekh Rajabu Salum,
alisema mihadhara ya pande zote mbili ijulikanayo kama ‘mihadhara
linganishi’ haijawahi kuwa tishio la amani nchini.
Naye Mwenyekiti wa mihadhara ya Kikristo, Mwinjilisti Daniel
Mwankemwa alisema mihadhara yao imetoa mchango mkubwa kwa waumini wao
kuimarika kiroho baada ya kupata ufafanuzi sahihi wa hoja mbalimbali
zilizokuwa zikiwasumbua.
-Mtanzania
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment