Tukio hilo la aina yake limetokea majira ya asubuhi ambapo Shekhe huyo
aliyetambuliwa kwa jina la Nuhu Mwafilango kushambuliwa akiwa katikati
ya sijida baada ya mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa shule ya
sekondari ya kutwa Kyela, Ally Mwangosi kumpiga Shekhe huyo na kitu
chenye ncha kali.
Taarifa kutoka msikitini hapo zinadai kuwa mara baada ya mwanafunzi huyo
kupita kibla na kumpiga shekhe huyo na kitu chenye ncha kali alipiga
ukelele wa kuomba msaada na hivyo kuibua taharuki miongoni wa waumini
waliokuwa wakiswali msikitini hapo.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Wilayani Kyela, Daudi Mwenda
alisema kuwa mara baada ya Shekhe huyo kuvamiwa na kupigwa waumini
walimuokoa na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya
kupatiwa matibabu.
Mwenda alisema kuwa Shekhe huyo ameumizwa vibaya eneo la kichwani
ambapo damu nyingi zilivuja mara baada ya kupigwa na kwamba mbali na
Shekhe huyo waumini wengine wawili waliokuwa wakijaribu kumuokoa
walijeruhiwa kwa kuchomwa na visu.
Wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo ni pamoja na mweka hazina wa
BAKWATA wilaya Ustadhi Khamis Husein aliyejeruhiwa kichwani na sikioni.
Baadhi ya waumini waliokuwepo katika ibada hiyo walisema kuwa tukio hilo
lilitokea wakati waumini wote wakiwa wamesujudu ndipo waliposikia
kelele na vurugu ambapo aliinuka mtu mmoja aliyekuwa na kitu mfano wa
nondo na kumpiga nayo Shekhe kichwani.
Mmoja wa waumini aliyejitambulisha
kwa jina la Idd Husein alisema kuwa wakati kijana huyo aliyekuwa na
kitu kinachofanana na nondo liliibuka kuundi la watu wengine
waliomsaidia na hivyo kuibuka vurugu kubwa iliyosababisha ibada ya swala
ya Idd kuvunjika.
Akizungumzia tukio hilo Katibu wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Shekhe Juma
Killah alisema kuwa vurugu hizo zimetokea katika swala ya Idd na
wahusika wa vurugu hizo ni waislamu ambao wanaipinga BAKWATA.
‘’Hiki ni kikundi cha waislamu waliotoka Jijini Dar es salaam kimekuja
huku na kimesambaa katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya kinashawishi watu
kuipinga BAKWATA na kinafanya mambo ambayo BAKWATA hatukubaliani
nayo,’’alisema Shekhe Killah.
Alisema kuwa kikundi hicho kilikuwa kikimtuhumu Shekhe wa Wilaya kuwa ni
mshirikina na kwamba kutokana na hali hiyo hakupaswa kuongoza ibada
msikitini na badala yake wao ndio waliopaswa kuongoza ibada msikitini
hapo.
Kwa upande wake Shekhe wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Mohamed Mwansasu alisema
kuwa kitendo hicho kimeudhalilisha Uislamu na kwamba kilichofanywa na
kundi hilo la watu si mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Hata hivyo Shekhe Mwansasu alienda mbali zaidi na kusema kuwa katika
kikundi hicho wapo baadhi ya waumini wanaodaiwa kuwa ni askari polisi
ambapo inadaiwa kuwa katika moja ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita
alivutwa kanzu yake na kutakiwa kutoka eneo la kuongozea ibada ili
kuwapisha wao waendeshe ibada hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Athumani Diwani amekiri kutokea kwa
tukio hilo ambapo alisema kuwa watu sita wanashikiliwa na Polisi
kufuatia vurugu hiyo iliyotokea majira ya saa 2:30 katika msikiti mkuu
wa Ijumaa wakati wa swala ya Idd el Fitri.
Kamanda Diwani alisema kuwa kundi la waislamu wanaojiita kuwa ni wenye
itikadi kali walivamia msikitini wakati waumini wengine wakiwa wameinama
wakisujudu na kumvaa imamu kwa kumpiga kwa mateke na ngumi huku wakiwa
na nondo, mikasi na visu.
Alisema waumini hao walikuwa na madai kuwa hawamtaki Shekhe huyo na kwamba uwezo wake ni mdogo katika dini.
Alisema kuwa Shekhe huyo aliokolewa na baadhi ya waislamu ambapo
aliwataja walioshikiliwa na polisi kuwa ni pamoja na Mashaka
Kassim (30) Issa Juma (37), Ahmed Kassim Magogo (35) Ibrahimu Shaaban (17)
ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela anayesoma
kidato cha Nne, Ambokile Mwangosi, (19) mwanafunzi wa kidato cha tatu shule
ya sekondari Kyela, Sadick Abdul (28).

0 comments:
Post a Comment