AFANDE SELE.
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kuwavuta wasanii
kujiunga na chama hicho, ambapo sasa wasanii wanne wa muziki wa kizazi
kipya, maarufu Bongofleva na filamu, wanatarajiwa kutangazwa kuhamia
chama hicho wiki hii.
Wasanii
hao wanadaiwa tayari kukubali kuingia kwenye chama hicho na
wanatarajiwa kutangazwa rasmi hadharani katika mkutano wa hadhara
utakaofanyika jijini Dar es Salaam.
Kukubali
kwao kuingia katika siasa, kunatajwa kutokana na ushawishi mkubwa
uliofanywa na wabunge vijana wa chama hicho, pamoja na Diwani wa CCM
kutoka kata moja ya Wilaya ya Kinondoni, ili chama hicho kivune kura za
vijana katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Wabunge
hao wa Chadema na majimbo yao katika mabano ni Halima Mdee (Kawe);
Kabwe Zitto (Kigoma Kaskazini); John Mnyika (Ubungo) na Joseph Mbilinyi,
jina la kisanii Sugu (Mbeya Mjini).
Habari
kutoka kwa watu wa karibu na wasanii hao pamoja na ndani ya Chadema,
zinawataja wasanii hao kuwa ni wanamuziki Judith Wambura maarufu Lady
Jaydee na wa miondoko ya Hip hop, Selemani Msindi ama Afande Sele.
Taarifa
zinawataja wengine kuwa ni mwanamuziki Fredy Maliki maarufu Mkoloni na
mwigizaji wa filamu, Jacob Steven kwa jina la kisanii JB.
Inadaiwa
wasanii hao lengo la kuingia katika siasa kupitia chama hicho, ni
kuwania ubunge ambapo Jaydee anatajwa kutaka kugombea wilayani Musoma;
Afande Sele Morogoro Mjini; Mkoloni Jimbo la Tanga na JB Jimbo la Mkoa
wa Dar es Salaam.
Hata
hivyo gazeti hili lilipowatafuta kuzungumzia taarifa hizo wote walikana
ingawa wapo waliokiri kushawishiwa kuingia kwenye chama hicho na
viongozi wa Chadema na wananchi, ili wagombee ubunge.
Afande
Sele alikana kujiunga na chama hicho na kusema hana taarifa hizo
isipokuwa ni kweli ameshawahi kufuatwa na viongozi wa Chadema wa Mkoa wa
Morogoro, wakimtaka ajiunge na chama hicho na agombee ubunge Morogoro
Mjini.
“Nimeshafuatwa
na viongozi wa Chadema wa mkoa na kata nijiunge na chama hicho na
nigombee ubunge …tena hata vijana wengi na baadhi ya wazee wamenitaka
nigombee ubunge kwa kupitia Chadema lakini nimekataa.
“Pia
Sugu ni mshikaji wangu na anapokuja Morogoro, vijiwe vyake ndio vyangu
naye vijana wameshamfuata wakimwambia anishawishi nigombee ubunge
kupitia Chadema, amekuwa akiniambia vijana wananitaka lakini mimi
sitaki, sijawahi kujiunga na chama chochote na naona mbunge wa sasa
(Abdulaziz Aboud) anafanya kazi nzuri.
“Mimi
sio mwanasiasa, lakini ni mwanaharakati kupitia muziki na mtandaoni na
nimekuwa nikitoa maoni mengi na kukosoa lakini narudia si mwanasiasa na
sijawahi kujiunga na chama chochote,” alisema Afande Sele.
Vilevile
amekanusha kushawishiwa na viongozi wa kitaifa wa Chadema au wabunge,
ingawa amekiri kuna wabunge wa chama hicho kuwa ni marafiki zake
wakiwemo Mbilinyi na Zitto.
Kwa
upande wa Jaydee alisema hafuati itikadi ya chama chochote cha siasa na
hapendi siasa kutokana na imani kuwa siasa ni uongo na yeye hapendi
uongo. Alisema hana nia ya kujiunga na chama chochote cha siasa wala
kugombea ubunge kupitia chama chochote.
Hata hivyo alipoulizwa iwapo atagombea baada ya Katiba kuruhusu mgombea binafsi, alisema kwa wakati huo atajua.
Hata
hivyo, Licha ya kuwaona wanasiasa ni waongo, anakiri wapo wanasiasa
anawaamini kutokana na kazi zao na kumtaja miongoni mwao ni Mwenyekiti
wa UDP, John Cheyo na Mbunge wa Afrika Mashariki, Shy-rose Bhanji.
Mwanamuziki
huyo alisema licha ya kuwa na marafiki wa Chadema na CCM kama Sugu na
Profesa Jay wa Chadema na Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige na
Bhanji wa CCM, hawajawahi kumshawishi kujiunga na vyama vyao.
Mkoloni
Akizungumzia taarifa hizo za kujiunga na Chadema, JB alikana na kusema;
“mimi na siasa ni vitu tofauti, sijawahi kufuatwa na mtu wa Chadema na
angalau kungekuwa na dalili basi uniulize, hiyo ni taarifa ya
kutengenezwa na wewe ndiye uliyetengeneza hakuna aliyekupa ni udaku
huo.”
Kwa
upande wa Mkoloni, alisema hajawahi kufuatwa wala kushawishiwa kujiunga
na chama chochote, isipokuwa ni mwanachama wa muda mrefu wa Chadema na
amekuwa akishiriki kampeni, mikutano ya hadhara na matukio yote ya
uhamasishaji ndani ya chama hicho.
Alisema
kuhusu kuombwa kuwania jimbo mkoani Tanga kwa tiketi ya chama hicho,
alisema hajawahi kuombwa na chama hicho kufanya hivyo.
“Sijawahi
kuombwa nigombee jimbo, na kuhusu nia ya kugombea, ni mapema mno
kuzungumzia suala hilo sasa na hata kanuni za chama changu haziruhusu
labda uniulize swali hilo mwakani naweza kuwa na jibu,” alisema Mkoloni.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alikataa
kuzungumzia taarifa hizo akidai yuko barabarani na masuala yote
yanayohusu chama hicho aulizwe Msemaji wa chama hicho.
Hata
hivyo msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema hana taarifa
kuhusu kufanyika kwa mkutano wa chama hicho Dar es Salaam na kutaka
apewe muda afuatilie taarifa hizo. Habari leo
0 comments:
Post a Comment