CUF yaishauri Tume ya katiba kuzingatia maoni ya mabaraza ya katiba
Na Hassan Hamad OMKR.
Chama Cha Wananchi CUF kimeishauri Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania kuzingatia maoni ya mabaraza ya katiba, ili rasimu ya pili ya katiba itakayotolewa iweze kukidhi matakwa ya wananchi na taifa kwa ujumla.Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza hayo katika viwanja vya Kibanda maiti mjini Zanzibar, wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama hicho.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema Katiba ya nchi ni jambo kubwa, hivyo hakuna budi kwa Tume iliyopewa jukumu hilo kufanya kazi kwa uhakika, ili wananchi wa pande mbili za Muungano waweze kuiridhia.
Ametahadharisha kuwa iwapo Tume hiyo itaacha kuyafanyia kazi maoni ya wananchi sambamba na yale ya mabaraza ya katiba, kuna hatari kuwa Katiba mpya haitofikia vigezo na kupelekea wananchi kutoikubali.
Katika hatua nyengine Maalim Seif ameunga mkono hoja iliyotolewa na msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lisu, ya kutaka kuweko na idadi sawa ya wajumbe wa bunge la katiba kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Wakati huo huo Maalim Seif ametumia nafasi hiyo kumpa pole Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na wananchi wa nchi hiyo kutokana na maafa yaliyotokea katika Jumba la biashara Mjini Nairobi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 50 na wengine zaidi ya 150 kujeruhiwa.
Pia amelaani kitendo cha kumwagiwa tindikali kwa Padri Joseph Mwang’amba hivi karibuni, na kwamba kitendo hicho ni cha kinyama na hakikubaliki. CHANZO http://www.zanzinews.com
0 comments:
Post a Comment