Mshambuliaji wa timu ya soka ya vijana ya Morogoro Joseph John katikati akitafuta mbinu ya kuwatoka walinzi wa Temeke ya jijini Dar es Salaam, John Kayanda kulia na Omari Abdallah wakati wa mashindano ya copa coca cola chini ya umri wa miaka 15 kituo cha Morogoro ambapo katika mchezo huo Temeke ilifanikiwa kuwafunga wenyeji Morogoro kwa bao 2-0. PICHA JUMAMTANDA.BLOGSPOT.COM
Na Juma Mtanda, Morogoro.
KIUNGO mshambuliaji wa timu ya soka ya vijana ya Morogoro, Omari Abdallah ameiwezesha timu yake kuibuka kidedea katika mchezo dhidi ya vijana wenzao wa Dodoma kwa kuikung’uta bao 2-1na kufufua matumaini ya kus
onga mbele baada ya kupoteza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Temeke kwa kulala bao 2-0 katika mchezo mkali wa mashindano ya Copa coca cola kituo cha Morogoro katika uwanja wa jamhuri mkoani hapa.
Dalili za ushindi kwa Morogoro zilianza mapema baada ya kuanzisha mashambulizi katika lango la wapinzani wao na dakika ya tatu kipindi cha kwanza Morogoro walifanikiwa kupata kona iliyochingwa na kiungu huyo Abdallah na kumkuta mshambuliaji, Clavery Hassan aliyetuliza mpira gambani na kufumua shuti kati lililojaa wavuni na kumfanya kipa wa Dodoma, Glanville Aidan asijue la kufanya na kuandika bao la kwanza.
Dakika ya 17 kipindi hicho cha pili kiungo huyu Omari Abdallah aliifungia timu yake bao la pili na ushindi akifunga shuti safi akiwa eneo la hatari kufuatia krosi iliyomiminwa na Shafii Ramadhani huku Dodoma wakipata bao pekee kupitia kwa Issa Abdi aliyeunganisha vema kona iliyopigwa na Rajab Mwilava na kumshinda kipa wa Morogoro Juma Shabaan na kufanya mchezo huo kumalizika kwa Dodoma kulala kwa bao 2-1 dhidi ya wenyeji Morogoro.
Katika mashindano hayo tayari kumeibuka manung’uniko kwa waalimu na wadau wa soka wakishutumu baadhi ya timu kuchezesha vijana waliovuka umri wa miaka 15.
Kocha mkuu wa Dodoma, Mussa Furutuni alisema kuwa timu ya Morogoro imechezesha vijana waliovuka umri wa miaka 15 huku wadau wa soka mkoa wa Morogoro nao akiwemo, Boniface Mapunda alisema timu ya Morogoro endapo itashindwa kufuzu katika hatua inayofuata basi lawama zote zitaelekezwa kwa Katibu Mkuu wa chama cha soka Morogoro (MRFA) Hamis Semka kwa kitendo chake cha kukusanya na kuunda timu ya copa coca cola mkoa huo huku akijaza vijana wengi wenye umri wa chini ya umri wa miaka 15 tofauti na timu ngingine.
Mapunda alisema kuwa wadau wa soka mkoa wa Morogoro walikaa kikao kujadili mwenendo wa mashndano hayo kufuatia kutandikwa bao 2-0 na Temeke hali ambayo iliwastua wadau hao baada ya kuwaona wachezaji wa Temeke wengi wao wakionekana kuvuka umri wa miaka 15.
Katika mchezo mwingine vijana wa Temeke walioibuka na ushindi katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Morogoro watashuka dimbani kucheza na Tanga ambayo katika mchezo wa awali ilipoteza kwa bao 1-0 kutoka kwa Dodoma katika mchezo utaofanyika saa 10 jioni katika uwanja huo wa jamhuri.
0 comments:
Post a Comment