NI BAADA YA POLISI KUMSAKA USIKU, MCHANA.
BAADA ya
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma kumsaka kwa siku mbili bila mafanikio
mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu (CHADEMA),
akidaiwa kumpiga na kumjeruhi mmoja wa askari wa Bunge, hatimaye
alijisalimisha mwenyewe jana jioni.
Taarifa
zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni, Sugu alikwenda polisi
akiongozana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, na wabunge Tundu
Lissu (Singida Mashariki), John Mnyika (Ubungo) na Joshua Nassari
(Arumeru Mashariki).
Akizungumza
na gazeti hili, Mnyika alisema kuwa Sugu hakukamatwa bali alijipeleka
mwenyewe polisi kwa hiari yake na kwamba jioni hiyo majira ya saa 1:10
alikuwa akiandikisha maelezo yake.
Wakati Sugu
akijisalimisha, wanasheria wa Bunge nao walikuwa wamejifungia kuangalia
namna ya kumkabidhi mbunge huyo mikononi mwa sheria.
Juzi na jana
viwanja vya Bunge vilitawaliwa na idadi kubwa ya polisi waliotumwa
kumkamata Sugu lakini mpaka Bunge linaahirishwa jioni haikujulikana ni
wapi alikokuwa mbunge huyo.
Mbunge huyo
juzi baada ya kubebwa mzobemzobe na askari wa Bunge na kisha kutolewa
nje ya ukumbi, inadaiwa kuwa alimpiga ngumi mmoja wa askari aliyemtuhumu
kuwa alikuwa amempia ngumi wakati wakimtoka nje.
Askari hao
juzi jioni walikuwa kwenye vikundi vikundi nje ya ukumbi wa Pius Msekwa
ambako kulikuwa kukifanyika mkutano wa wabunge wa upinzani ambapo Sugu
pia alikuwa miongoni mwao.
Kutokamatwa
kwa Sugu kumewashangaza wengi waliokuwa karibu na askari hao kwa kuwa
alikuwa amekaa jirani nao akizungumza na wenzake kabla ya kuanza kwa
kikao chao.
Tanzania
Daima lilidokezwa kuwa askari hao walishindwa kumkamata Sugu kwa kuwa
hapakuwepo na amri ya kukamatwa kwake na hata ilipotolewa alikuwa
ameshaondoka katika viwanja vya Bunge.
Mpaka Bunge
linaahirishwa juzi jioni, idadi kubwa ya askari walikuwa nje ya milango
na korido zilipo ofisi za kambi ya upinzani wakimsubiri Sugu bila
mafanikio.
Hata hivyo
taarifa zinaeleza kuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia askari kusuasua
kukamatwa kwa Sugu ni kutokana na kinga ya kibunge aliyonayo na pia kosa
analotuhumiwa kulifanya alilifanya akiwa kwenye viwanja vya Bunge.
“Tulipata
mtanziko wa kumkamata haraka haraka, ilibidi lazima tuwasiliane na ofisi
ya Spika kujua taratibu za kumkamata kiongozi huyo hasa kwa kuwa
alifanya kosa hilo akiwa bungeni,” kilisema chanzo kimoja.
Wakati
askari wakihaha kumtafuta Sugu, mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole
Sendeka (CCM), jana aliomba mwongozo wa Spika kuhusu tukio la vurugu
zilizotokea juzi bungeni hasa tukio la Sugu kumpiga askari.
Sendeka
alisema tukio hilo limelidhalilisha Bunge na askari wanaowalinda, hivyo
akataka liweke wazi ni hatua gani zitakazochukuliwa dhidi ya mbunge huyo
ili kulinda heshima ya chombo hicho.
“Nataka nijue ibara ya 100 ambayo humpa kinga mbunge na uhuru wa mawazo akiwa ndani ya Bunge inatumikaje katika tukio hili?
“Je, Bunge litalindaje heshima yake dhidi ya tukio hili lililofanywa na mbunge mwenzetu?” alihoji.
Akijibu
mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alisema tukio hilo
ni geni hivyo Bunge limeshindwa kutoa jibu la mara moja.
“Jambo hili
halijawahi kutokea katika historia ya Bunge, sasa nami nitalifikisha kwa
wanasheria wa Bunge wanishauri namna ya kulishughulikia na baada ya
hapo nitatoa mwongozo,” alisema.
Akitoa
mwongozo huo muda mfupi kabla ya Bunge kuahirishwa jana jioni, Naibu
Spika, Job Ndugai, alisema kuwa bado wanashauriana na wanasheria kuona
kanuni zinawaelekezaje.
Alisema kuwa
licha ya tukio hilo kutokea katika eneo la Bunge bado kitendo hicho ni
cha jinai na hivyo, mtuhumiwa atashughulikiwa kisheria.
“Ni sawa na
jaji yuko mahakamani ambapo kuna kinga kama za Bunge halafu jaji
mwenzake ampige ngumi. Huyo lazima achukuliwe hatua hawezi kuachwa.
Kinga zetu ziko kwenye uhuru wa mawazo tu,” alisema.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, juzi lilitangaza kumsaka Sugu kwa tuhuma za kufanya vurugu na kumjeruhi askari wa Bunge.
“Lakini tuna
mashaka sana na hatua yake aliyoifanya nje ya ukumbi ambapo alimvamia
na kumpiga ngumi nzito Koplo Nikwisa Nkisu ambaye alijeruhiwa jicho,”
alisema mmoja wa askari ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Ofisa
Upelelezi wa Wilaya ya Dodoma ASP Jumanne Kim, juzi jioni alithibitisha
kusakwa kwa mbunge huyo aliyeondoka maeneo ya Bunge mchana akiwa ndani
ya gari la kiongozi mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman
Mbowe. http://chademablog.blogspot.com/
0 comments:
Post a Comment