BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TANZANIA YAJIONGEZEA SIFA DUNIANI KWA KUWA KINARA WA KUPITISHA KINYEMELA MADAWA YA KULEVYA ZAIDI YA TANI 60 BILA KUKAMATWA KWA NCHI ZA AFRIKA YA MASHARIKI.

Na Mwandishi Wetu.
RIPOTI mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Mihadarati na Uhalifu (UNODC), imesema Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa za kulevya katika nchi za Afrika Mashariki.

Ripoti hiyo, imesema jumla ya tani 64 za dawa za kulevya aina ya Heroine, zilisafirishwa bila kukam

atwa kwenda au kupitia Afrika Mashariki, ikiwamo Tanzania kati ya mwaka 2010 na 2013.

Ripoti hiyo, imesema nchini Tanzania mji wa Tanga, ndio kinara na njia kuu ya kusafirishia dawa hizo kwani tangu mwaka 2010, ukamataji uliongezeka kutoka kilo 145 hadi kilo 813 mwaka huu. 
Photo: Dawa za kulevya balaa, mamia wako jela nje

Dar es Salaam. Kasi ya kukamatwa kwa Watanzania wakiwa wamebeba dawa za kulevya nje ya nchi, imezidi kuchukua sura mpya baada ya kubainika kuwa maelfu ya Watanzania wanatumikia vifungo mbalimbali ikiwamo vifungo vya maisha nje ya nchi.

China pekee mpaka sasa ina Watanzania 176 wanaotumikia vifungo katika magereza za nchi hiyo, huku asilimia 99 wakiwa wamekamatwa na dawa za kulevya.

Kutokana na kuwapo ongezeko hilo la wafungwa wa dawa za kulevya, China imekataa ombi la Tanzania la kubadilishana wafungwa, ikieleza hatua hiyo itachochea watu wengine kujiingiza kwenye uuzaji wa dawa za kulevya nchini humo.Hatua hiyo imekuja baada ya nchi hizo mbili kutofautiana katika mfumo wa sheria, ambapo China mtu anayekamatwa

na dawa hizo hunyongwa hadi kufa wakati Tanzania mtu anayekutwa na dawa hizo anahukumiwa kifungo.

Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema: “Takwimu halisi tulizonazo kutoka China pekee zinaeleza kuwa Watanzania 176 wanatumikia vifungo na asilimia 99 ni kwa tuhuma za dawa za kulevya. Kawaida nchi hiyo adhabu yake ni kifo lakini kesi nyingi bado zipo katika uchunguzi ambao huchukua miaka miwili.”

Hata hivyo alisema kutokana na uhusiano mzuri wa nchi hizi mbili, kuna uwezekano mkubwa kwa Watanzania hao kufungwa kifungo cha maisha pamoja na faini.

Aidha, alisema juhudi za Tanzania kuwasiliana na China kuhusu uwezekano wa kuwa na mikataba ya kubadilishana wafungwa ziligonga mwamba, baada ya nchi hiyo kukataa ombi hilo kutokana na idadi kubwa ya wafungwa hao kutuhumiwa na dawa za kulevya.

“China imekataa kuwa na mkataba wa kubadilishana wafungwa kwani wanahofu kuwa inaweza ikachochea biashara hivyo. Hivyo kinachofanyika ni kuwatembelea wafungwa hao mara kwa mara na kuhakikisha wanapata haki zao na kuwasaidia mawasiliano wao na ndugu zao wanapotumikia vifungo vyao nchini humo.”

Wakati hayo yakibainika, Jumanne wiki hii Tanzania ilisaini mkataba wa kubadilishana wafungwa na Thailand, mkataba ambao utawafanya Watanzania waliofungwa nchini humo kuomba kutumikia vifungo vyao nchini.

Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, zinaeleza kuwa zaidi ya Watanzania 103 wamekamatwa nchini Brazil kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, huku 132 wakikamatwa katika nchi nyinginezo.

Hata hivyo, taarifa zaidi kutoka katika tume hiyo zinadai kuwa hiyo si takwimu halisi ya Watanzania wanaoshikiliwa nje ya nchi, bali imetokana na nchi hizo kutoa taarifa kuhusu Watanzania hao, kwani bado idadi kubwa ya Watanzania wanakamatwa lakini taarifa zao hazijaweza kuifikia tume.

Akizungumzia jana Kamanda wa Polisi Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema tatizo la dawa za kulevya linazidi kuwa kubwa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wasafirishaji na watumiaji hapa nchini.

Takwimu za watu waliokamatwa ndani ya nchi ambao ni raia wa kigeni na Watanzania zinaonyesha ongezeko kubwa kwa mwaka 2012, ukilinganisha na miaka miwili ya nyuma.

“Mwaka 2010 kitengo kilifanikiwa kukamata watu 496 wakiwa na kilo 191 za Heroin, watu 525 wakiwa na kilo 165 za Cocaine, watu watano wakiwa na kilo tano za dawa aina ya morphine, watu 9539 wakiwa na kilo 279,521 za bangi na watu 1351 wakiwa na kilo 10,318 za mirungi na walifanikiwa kuteketeza ekari 296 za bangi.

“Mwaka 2011 Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya kilikamata watu 40 wakiwa na kilo 265 za Heroine, watu 30 wakiwa na kilo 128 za Cocaine, watu 39 wakiwa na kilo 17,257 za bangi na watu 150 waliokamatwa na kilo 100 za mirungi pamoja na kuteketezwa kwa ekari 18 za bangi.

Nzowa anautaja mwaka 2012 kuwa ongezeko lilipanda mpaka kufikia watu 400 waliokamatwa na kilo 260 za Heroine, watu 138 walikamatwa na kilo 151 za Cocaine na wengine 5548 walikamatwa na kilo 48658 za bangi na wengine 847 walikutwa na mirungi yenye uzito wa kilo 2616.

“Katika watu hawa tuliofanikiwa kuwakamata si kwamba wote wanakutwa na shehena ya dawa hizi, tunaweza kukamata watu 20 wakiwa na gramu 200 tu, lakini tunaweza kukamata watu wachache wakiwa na shehena,” alisema Nzowa.

Anasema Februali, 2011 walimkamata mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Shirena akiwa na shehena ya kilo 176 ya dawa za kulevya ambaye alizipitisha kupitia bandari bubu.

“Bandari bubu hizi walio wengi wanapitisha dawa za kulevya kuingiza nchini kupitia majahazi na mitumbwi na wengi wao wanawatumia wavuvi. mfano tulishawahi kukamata kilo 81 za dawa za kulevya zilizokuwa zikisafirishwa na jahazi. Tulishakamata kilo 211 za dawa za kulevya huko Mchinga, Lindi zilizokuwa zikisafirishwa kwa kutumia njia bubu.”

Alisema mwaka 2011 raia wawili wa nje na Watanzania wawili walikamatwa Mbezi Jogoo wakiwa na kilo 176 za dawa za kulevya wakijiandaa kuzisafirisha, lakini taarifa ndizo zilizosaidia.

Taarifa zingine zilidai kuwa katika magereza za Hong Kong kuna Watanzania 200, ambapo 130 kesi zao zimekwishahukumiwa na wengine 70 kesi bado zinaendelea mahakamani.

Ukubwa wa mtandao ndani na nje ya nchi

Kamanda Nzowa anasema mawakala na matajiri wanaosambaza dawa za kulevya wapo ndani na nje ya nchi na wanashirikiana na kubuni mbinu mpya kila uchao.

“Hawa watu wanawasiliana, kwani Tanzania tunakamata watu wakitoka nje ya nchi wakiingia na dawa za kulevya hapa nchini, lakini hawa wamepita nchi kadhaa bila kugundulika, hivyo Watanzania wanavyokamatwa nje ya nchi si kwamba zinatoka kwa uzembe bali hawa watu wana njia nyingi wanazobuni kila siku,” alisema.

Alisema ushahidi unakuwa mgumu kuwang’amua baadhi yao kwani hukana na kutoa visingizio kwamba wanakwenda kufuata nywele, nguo au mazulia nchini Brazil ambako pia kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoshikiliwa na dawa za kulevya.

“Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiondoka hapa nchini kwenda nje ya nchi kuchukua mizigo yao ya kibiashara ambako pia wanabeba na dawa za kulevya, na hawa walio wengi wanameza kete. lakini wengi tunashindwa kuwakamata kwa kuwa hatuna vyanzo vya habari,” alisema Nzowa.

Akitoa mfano aliwataja raia wawili kutoka nchini Liberia Diaka Brama Kaba na Njane Abubakar Guinea waliokamatwa na kilo 17 na mwingine 14 uwanja wa ndege, wakitokea nchini Trinidad and Tobago ambao walisafiri kwa ndege wakipitia Brazil, Johannesburg, Afrika Kusini na kuja Tanzania, lakini taarifa ziliwasaidia kuwakamata.

Majina ya mtandao sugu hapa nchini

Nzowa alisema mpaka sasa hakuna mwanasiasa wala kiongozi wa Serikali anayetuhumiwa kuhusika na mtandao wa dawa za kulevya, bali kuna baadhi ya wafanyabiashara maarufu wanaochunguzwa wakiwamo baadhi waliofikishwa mahakamani, lakini wanakosa vidhibiti kwa kushindwa kuwakamata na chochote kile.

“Changamoto ni kubwa, mpaka sasa tayari Ayoub Mfaume Kiboko na Shikuba ambaye hupeleka watu wake China na tayari kuna Watanzania wameshatoa ushahidi huko Hong Kong kumhusu, huyu tulishamfikisha mahakamani ila pia tulikosa vielelezo na hii ndiyo changamoto,” alisema.

Aidha, Nzowa alisema ili kujidhatiti katika kukomesha biashara hiyo wafanyakazi wote wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wakiwamo TAA, Uhamiaji na wengineo washirikiana ili kuweza kuwabaini wale wote wanaopitisha dawa hizo kupitia kiwanja hicho.
“Tanga ni njia kuu ya usafirishaji wa dawa hizi, kumekuwa na ongezeko kubwa mno tofauti na miji mingine katika ukanda wa Afrika Mashariki,” ilisema ripoti hiyo. Wastani wa ukamataji wa shehena za dawa za kulevya eneo hilo, uko katika kilogramu 1,011 mwaka 2013 kutoka 145 kilo za awali.

Takwimu zinaonyesha kwa pamoja Watanzania na Wakenya, wanaongoza kwa utumiaji na usafirishaji dawa za kulevya aina ya Cocaine, huku wakitumia dola milioni 160 kila mwaka. Lakini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kati ya mwaka 2010 na 2013, shehena zilizokamatwa na maofisa husika nchini Tanzania, Kenya, Shelisheli na Mauritius zilikuwa tani 1.6 tu. 

Takwimu hizo za kushtusha, zinatoa picha kwamba sehemu kubwa ya shehena za dawa za kulevya hupitishwa bila kugundulika au kukamatwa na vyombo vya dola. Eneo la Afrika Mashariki, linaonekana kuwa kimbilio la wasafirishaji kutoka Asia hususani wa Afghanistan, Iran na Pakistan. 

Ripori hiyo, imesema Pwani ya Mashariki mwa Afrika imekuwa kitovu cha biashara na upitishaji dawa za kulevya, kwa sababu ya kukua kwa mahitaji ya ndani na kuchagizwa na hatua zilizochukuliwa kudhibiti dawa hizo katika eneo la Balkan, lililokuwa likiongoza kwa biashara hiyo.

Kwa mfano mwaka 2011, kilogramu 102 za dawa za kulevya zilikamatwa mjini Mombasa, lakini kufikia mwaka 2013, kiwango hicho kiliongezeka kuwa kilo 194.

Ripoti ililinganisha ukanda huo na njia ya Balkan, ambayo inaunganisha nchi za Pakistan, Iran na Uturuki kabla ya kuvusha kwenda kusini mashariki mwa Ulaya. Katika njia hiyo, ukamataji ulishuka hadi kilogramu 679 mwaka 2010, kutoka kilogramu 1,804 mwaka 2006 ikichangiwa pamoja na mambo mengine na kupungua kwa soko la Heroine barani Ulaya.

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa unasema wasafirishaji wamebuni njia nyingine ambazo bado hazijulikani kuingia Ulaya. “Mtiririko wa biashara mashariki mwa Afrika kwa hakika umeongezeka, kutokana na ukuaji wa mahitaji ya ndani au ukuaji wa matumizi katika ukanda huo kama soko au eneo la kupitisha mihadarati. 

Iwapo mashariki mwa Afrika itakuwa ‘Balkan mpya’ athari zake kwa ukanda huo, zitakuwa kubwa kama zile zilizoikumba Afrika Magharibi, ripoti ilionya.

“Hatua ya hivi karibuni ya kukamatwa kwa dawa za kulevya, zinachukuliwa uzito kimataifa, lakini pia ongezeko la matumizi ndani ya mashariki mwa Afrika si jambo la kupuuza.”

Wakati dawa za kulevya zinapoondoka Afghanistan, husafirishwa kwa njia ya barabara hadi Pwani ya Makran, ukanda wa jangwani uliotambaa kutoka Pakistan hadi Iran katika mwambao wa Bahari ya Arabu na Ghuba ya Oman ambako wakazi wake wengi ni Waafrika Magharibi na Waasia.

Wasafirishaji hao wana watu wao Mashariki mwa Afrika, ambao wengi wao ni Watanzania na Wakenya wanaoendesha shughuli mpakani.

Mwaka 2011, kwa mfano, Nyakiniywa Naima Mohamed maarufu kama Mama Lela, msafirishaji maarufu wa biashara hiyo raia wa Kenya kutoka kitongoji cha Majengo mjini Nairobi, alikamatwa nchini Tanzania baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama kumtaja kuwa mmoja wa vigogo wa ‘unga’. Vigogo wa ‘unga’, hata hivyo huajiri watu wanaowabebea kutoka mataifa mbalimbali yakiwamo Waafrika Kusini na Waafrika Magharibi.

Inaelezwa wabebaji huhusika wa kusafirisha dawa za kulevya, hupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole nchini Ethiopia. Lakini imekuwa kawaida kwa Waafrika Magharibi kutumia hati za kusafiria za Afrika Kusini, wanazopata kwa njia ya kuhonga au kufunga ndoa na raia. 

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, baada ya Watanzania na Wakenya, raia wa Nigeria wanashika nafasi ya pili kama wabebaji maarufu zaidi, huku idadi yao kubwa wakiishi nchini Kenya. Mmoja wa Wanigeria hao, Anthony Chinedu kutimuliwa kwake nchini Kenya, kidogo kusababishe mgogoro wa kidiplomasia baina ya Kenya na Nigeria.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: