CHAMA kikuu cha wafanyakazi nchini Tunisia UGTT kimekuwa mpatanishi katika mazungumzo ya mzozo nchini humo jana (27.09.2013) ambapo chama tawala cha Ennahda kimekubali mpango wa mazungumzo ya kuunda serikali mpya.
Baraza la kutunga sheria la Tunisia.
Chama hicho kikuu cha wafanyakazi nchini humo kiliitisha mkutano kati ya
chama hicho kinachofuata nadharia za dini ya Kiislamu pamoja na
upinzani usiopendelea dini kuwa msingi wa maadili ya jamii ili
kukubaliana juu ya tarehe wiki ijayo ambapo kutafanyika mjadala wa
kitaifa, wenye lengo la kumaliza mzozo uliozushwa na mauaji ya mbunge
maarufu wa upande wa upinzani Julai mwaka huu.Nchi hiyo ambayo ni chanzo cha vuguvugu la mapinduzi katika mataifa ya Kiarabu mwaka 2011 imetumbukia katika mzozo wa kisiasa , wakati upande wa upinzani usiopendelea dini kuwa msingi wa maadili ya umma ukikishutumu chama cha msimamo wa wastani cha Ennahda kwa kushindwa kuwadhibiti watu wenye itikadi kali ya dini ya Kiislamu.
Katika taarifa iliyochapishwa katika tovuti yake chama hicho cha wafanyakazi cha UGTT, ambacho kimekuwa na uhusiano usiokuwa mzuri na chama cha Ennahda na hapo kabla kukishutumu chama hicho kwa kuburuza miguu katika hatua za mageuzi nchini humo, kimesema kuwa chama hicho tawala kimekubali mpango wake wa mpito.
Chama cha wafanyakazi cha UGTT hapo kabla kimetoa wito wa kufanya kampeni ya upinzani kuhakikisha kuwa chama cha Ennahda kinakubaliana kikamilifu na mpango wake huo wa mpito.
Shutuma
Chama hicho kimekishutumu chama cha Ennahda kwa kufanya kila kiwezacho kuhakikisha kushindwa kwa mpango huo, ambao kimeutayarisha pamoja na chama cha waajiri Utica, shirika lisilokuwa la kiserikali la kutetea haki za binadamu nchini humo la Tunisia League for Human Rights , pamoja na chama cha wanasheria.
Ennahda imekataa mabadiliko, na inaushutumu upinzani ambao kwa kiasi kikubwa unapinga dini kuwa msingi wa maadili, kwa kuvuruga mapendekezo ya wapatanishi kwa kudai serikali ijiuzulu mara moja.
Mpango huo umeweka muda wa wiki tatu kwa kuundwa baraza la mawaziri litakalokuwa na wajumbe ambao si wanasiasa litakalochukua nafasi ya serikali ya sasa, baada ya kuanzishwa kwa majadiliano na vyama vya upinzani.
Msemaji wa chama cha Ennahda Lajmi Lourimi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa chama chake "kiko tayari kuingia katika majadiliano na vyama vyote ambavyo vitapenda". "Mjadala wa kitaifa unaweza kuanza wiki ijayo, lakini hakuna tarehe iliyokwisha pangwa." DW
0 comments:
Post a Comment