BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ELIMU YA AFYA KWA WASICHANA: WASICHANA WAELIMISHWE ILI KUKWEPA MIMBA ZA UTOTONI.

WANAFUNZI.
WANAFUNZI mabinti wanapopata mimba hulazimika kukatiza masomo na ndoto zao za kufanikiwa kupitia elimu huzimika. Mimba za utotoni ni matukio yanayoelekea kuzoeleka na kuchukuliwa kuwa ni ya kawaida.

Hakuna mikakati makini ya kudhibiti hali hiyo zaidi ya utekelezaji wa sheria kwamba anayepata mimba lazima afukuzwe shule. Wasichana zaidi ya 55,000 wamekuwa wakifukuzwa shule kwa sababu ya ujauzito au nyinginezo katika kipindi cha muongo
mmoja, kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka Kituo cha Haki za Uzazi (the Centre for Reproductive Health).

Ripoti hiyo iitwayo Forced Out: Mandatory Pregnancy Testing and The  Expulsion of Pregnant Students In Tanzanian School ilizinduliwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Evelyn Opondo, Mkurugenzi wa Kanda ya Africa wa Kituo hicho. 
 
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa masuala ya afya, afya ya uzazi na waandishi wa habari Miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa kukabiliana na tatizo hilo ni wasichana kupimwa ujauzito na kufukuzwa shule ambayo ni matokeo ya utekelezaji wa sera inayokiuka Haki za Binadamu.

“Kuwalazimisha wasichana wadogo kupimwa mimba katika shule za Tanzania ni ubaguzi na ukiukaji wa haki za binadamu za taifa na kimataifa- bila ya kujali kama wasichana hawa ni wajawazito au la,” alisema Lilian Sepulveda,mkurugenzi wa Global Legal Program katika kituo cha Haki ya Uzazi.”Kukiuka haki za wasichana wajawazito ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu,” alisema.

Mambo mengi yamebainishwa katika ripoti hiyo, ikiwamo mfumo huo unaotumiwa na maofisa wa shule kuwa ni aibu na udhalilishaji licha ya kuchukuliwa kuwa unalenga kuwazuia wasichana kufanya ngono na kupata mimba.

Wakati hayo yakifanyika, hakuna utaratibu wa kutoa elimu ya afya ya uzazi au huduma ambazo zinaweza kutoa kinga kwa wanafunzi ikiwamo kuwapa taarifa muhimu ili wasipate mimba bila ya kupanga. Matumizi ya vidonge vya kupanga uzazi kwa wanafunzi nchini Tanzania ni kama hayapo kwa sababu ni asilimia 15- 19 ya wanawake wenye uwezo wa kufanya mapenzi ndiyo wanatumia njia za mpango wa uzazi.

“Wasichana hao, wanastahili haki za binadamu kama ilivyo kwa wakubwa, na kwa hiyo wanahitaji kuwa na zana wanazozihitaji ili kuwapa taarifa na kuweza kuwafanya kuwa na uchaguzi kuhusu afya ya uzazi,” alisema Dk. Julius Mashamba, Wakili na Makamu wa tatu wa Kamati ya Wataalamu wa Afrika wa Haki na Jamii kwa watoto (the African Committee of Experts on
the Rights and Welfare of Child.)

“Kwa kuwazuia wasichana kupata vidonge vya uzazi na elimu ya afya ya uzazi, shule ni kama zinawalazimisha wasichana kubeba mimba mapema na kuwafanya washindwe kupata elimu na kushindwa kutimiza ndoto za maisha yao,” alisema.

Ripoti hiyo Forced Out imebainisha kuwa, licha ya kuwapo upungufu wa elimu ya afya ya uzazi na huduma, serikali ya Tanzania imeshindwa kukabiliana na kiwango kikubwa cha matokeo ya ngono na ndoa za mapema nchini- masuala mawili ambayo yana mchango mkubwa kwa mimba za utotoni.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Taifa ya uchunguzi ya mwaka 2009 iliyofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Watoto (UNICEF), wanawake watatu kati ya 10 wenye umri kati ya miaka 13 na 14 Tanzania Bara angalau katika tukio moja wamekabiliwa na ukatili wa kijinsia kabla ya kufikia umri wa miaka 18 ambao wengi wao kwa mujibu wa ripoti wamelazimishwa
kufanya ngono.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na Kituo hicho ni kuishauri serikali ya Tanzania kukomesha mara moja kufanya mambo kinyume cha sheria kuwalazimisha wasichana kupima mimba shuleni na kuhakikisha kuwa wasichana wadogo wanapata fursa ya kuendelea na elimu wakati na baada ya kupata mimba.

“Kama serikali ya Tanzania inataka kweli kukabiliana na tatizo kubwa la mimba za utotoni, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iandae na kutekeleza sera za kuwalinda wasichana kutokana na ukatili wa mapenzi na kuendelea na elimu shuleni” alisema Evelyn Opondo.

Pia alisema kuwa” shule zinatakiwa kutoa elimu bora kuhusu ngono na afya ya uzazi na sheria za Tanzania lazima zifanyiwe marekebisho ili kuendana na sheria za kimataifa za haki za binadamu kwa kupandisha umri wa wasichana kuolewa hadi miaka 18,”

Ripoti hiyo imeeleza matukio mengi ya wasichana waliolazimishwa kupimwa mimba katika shule za msingi au sekondari, wengi wao walielezea zoezi hilo kuwa ni la aibu na lenye maumivu na kwa wale waliofukuzwa shule walielezea kuwa walinyanyaswa na familia zao, marafiki na kubwa kuliko yote ni kwamba nafasi zao za kupata elimu na hali zao za baadaye zimevurugwa. http://www.manyandahealthy.blogspot.com
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: