KIKUNDI cha Al Shabaab kimetishia
kumwaga damu zaidi Kenya kwa kufanya mashambulizi mapya na safari hii
wanatamba kupiga patakapouma zaidi.
Kundi hilo limesema kwamba
litaongeza idadi ya watu katika kikosi cha mashambuzi nchini humo
kutok
ana na Kenya kukaidi kuondoa majeshi yake Somalia.
“Tutaishambulia Kenya sehemu
itakayowauma zaidi, tutageuza miji yao makaburi na mito ya damu
itatiririka Nairobi nzima,” al Shabaab ilisema katika taarifa yake na
kuongeza:
“Uamuzi wa Serikali ya Kenya kuendelea
kuyaacha majeshi yake Somalia ni ishara ya wazi kwamba, hawajataka
kujifunza kutokana na yaliyotokea katika shambulizi la Westgate,”
ilieleza taarifa hiyo huku ikijigamba kuwa, Kenya itakuwa eneo
litakalogubikwa na wingu la damu na vurugu.
Wakati kikundi hicho kikitoa tishio
hilo, takriban miili isiyopungua tisa imepatikana katika eneo la ndani
ya kifusi kwenye jengo hilo, na sehemu ya eneo liliunguzwa kwa moto
wakati wa shambulio hilo la Westgate.
“Baadhi ya miili haiwezi kutambuliwa
kabisa na utambuzi wa vinasaba (DNA) utafanywa ili kutambua, mingine
imeharibiwa na inatisha,” taarifa kutoka Polisi ilieleza.
Hata hivyo haikuwekwa wazi kama idadi ya
miili hiyo tisa imejumlishwa na watu 67 wakiwemo wanajeshi sita
waliokufa katika shambulizi hilo. Rais Kenyatta ajibu Hata hivyo Rais wa
Kenya, Uhuru Kenyatta, juzi alikaririwa akisema majeshi yake
yataendelea kubaki Somalia hadi hapo amani na usalama wa nchi nchi hiyo
vitakapotengamaa.
Septemba 21 Shambulio la Westgate
lililotokea Septemba 21 mwaka huu katika jengo hilo la maduka ya bidhaa
mbalimbali za watu wenye maisha ya juu, wanadiplomasia na
wafanyabiashara wakubwa wa ndani na nje ya Kenya.
Mbali ya vifo hivyo vilivyofahamika hadi
sasa, watu zaidi ya 170 walijeruhiwa vibaya huku wengine wakipata
matatizo ya kisaikolojia.
Miongoni mwa waliouawa ni watoto waliokuwa
kwenye tamasha la mashindano ya kupika kwenye jengo hilo.
Baadhi ya manusura wa shambulio hilo
walieleza namna walivyokutana uso kwa uso na magaidi hao.
Kupitia
taarifa mbalimbali, magaidi hao walisikika wakidai wanawasaka Wakenya na
Wamarekani ingawa waliouawa na kujeruhiwa katika shambulio hilo ni
pamoja na raia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Ufaransa, Canada,
Australia, Marekani, Uingereza, Ghana na kwingineko.
Pamoja na majeshi na polisi wa Kenya
kuzingira jengo hilo tangu saa chache baada ya tukio, taarifa zinadai
baadhi ya magaidi waliokuwa katika jengo hilo, walitoroka kupitia mtaro
wa maji machafu uliokuwa chini ya jengo hilo na huenda watu wengi zaidi
wakawa wamepoteza maisha ikiwemo mateka waliodaiwa kushikiliwa na
magaidi hao ndani ya jengo hilo.
Shambulio hilo ni la pili kwa ukubwa
nchini humo likihusisha kikundi cha al Shabaab chenye ushirika na al
Qaeda ambao wanadaiwa kuhusika na shambulizi kubwa lililotokea mwaka
1998 katika Ubalozi wa Marekani nchini humo na kusababisha vifo vya
zaidi ya watu 220. HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment