BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WABUNGE WATAKA VIGOGO WA UJANGILI WA MENO YA TEMBO WATAJWE MAJINA YAO, WAMO WABUNGE, WAZIRI NA WANASIASA.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola akiomba mwongozo kwa Naibu Spika, Job Ndugai wakati wa kikao cha kwanza cha Mkutano wa 13 wa Bunge, mjini Dodoma jana. PICHA/EDWIN MJWAHUZI. 

DODOMA. 
WABUNGE jana walichachamaa na kushinikiza kutolewa kwa orodha ya vigogo wanaojihusisha na ujangili wakati wa kikao cha kwanza cha mkutano wa 13 wa Bunge unaofany
ika mjini Dodoma.

Wabunge hao walitaka kutajwa kwa majina ya mawaziri, viongozi wa Serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara hiyo.

Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo, akiitaka Serikali kuwataja hadharani na kuwachukulia hatua viongozi wake na wanasiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge, ambao wanatajwa kuhusika na vitendo vya ujangili nchini.

Lugola aliomba mwongozo wa Naibu Spika baada ya kutoridhishwa na jibu lililotolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli.

Katika jibu hilo, Nyalandu alilieleza Bunge kuwa Operesheni Tokomeza inayolenga kukomesha vitendo vya ujangili nchini bado inaendelea, lakini alishindwa kulieleza Bunge ni nani hasa wamebainika kuhusika na vitendo hivyo.

Lugola, hata hivyo, aliitaka Serikali kuwasilisha ripoti bungeni kuhusiana na utekelezaji wa operesheni hiyo.

“Tangu Aprili tumekuwa tukipewa majibu mepesi kuhusiana na operesheni hii, wakati suala hili si la masihara,” alionya Lugola.
Lugola alisema kuwa taarifa zimewataja watu wanaohusika na vitendo hivyo wakiwamo viongozi serikalini, mawaziri pamoja na wabunge, lakini tangu operesheni hiyo ilipoanza hakuna yeyote miongoni mwa hao wanaotajwa ambaye amekamatwa isipokuwa wananchi wa kawaida.

Alisema operesheni hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa unyama kwani wanaokamatwa hupigwa na kuteswa bila ya ushahidi unaoonyesha kuhusika kwao na vitendo vya ujangili.

“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao wakichukuliwa hatua,” alisema.

Kabla ya Naibu Spika kutoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Lugola, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kukiri kuwapo kwa vitendo vya utesaji wa watu wanaokamatwa katika operesheni hiyo.

Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa msaidizi wake jimboni ambaye alipigwa na kuteswa na askari hao kabla ya kuachiwa baada ya kushikiliwa kwa siku moja, huku akionyesha kuwa ushahidi wa tukio hilo anao kwenye simu yake. MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: