BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BARAZA LA HABARI TANZANIA LAAMURU GAZETI LA RAIA MWEMA KUMWOBA RADHI MBUNGE WA KINONDONI KUTOKANA NA KUMPAKWA MATOPE YA KUUZA MADAWA YA KULEVYA NDANI YA WIKI MBILI NA KUMLIPA FIDIA.

Mbunge wa Kinondoni, Idd  Azzan  akieleza malalamiko yake mbele ya Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari (MCT), kuhusiana na madai ya kukashifiwa na gazeti la Raia Mwema  na Mwanahabari kwa kumhusisha na biashara ya dawa za kulevya, jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema, Godfrey Dilunga. Picha na Joseph Zablon.  

DAR ES SALAAM. 
GAZETI la Raia Mwema limetakiwa kumwomba radhi ndani ya wiki mbili, Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan na kumlipa fidia ya gharama alizotumia katika shauri la madai ya kutotendewa haki na gazeti hilo, baada ya kuandika habari ambazo zilizomuhusisha mbunge huyo na biashara ya dawa za kulevya bila kumpa nafasi ya kujieleza.



Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari (MCT),kilichofanyika makao makuu ya baraza hilo jana, Mwenyekiti wa MCT, Jaji Thomas Mihayo alisema, baada ya kamati hiyo kusikiliza pande zote mbili imebainika kuwapo kwa upungufu wa kitaaluma katika habari hiyo.


Gazeti la Raia Mwema katika toleo namba 309 la Julai 31, mwaka huu kulikuwa na habari ambayo kichwa chake cha habari kilisomeka  ‘Idd Azzan Mbunge au muuza madawa ya kulevya’ na ndani ya habari hiyo kulikuwa na tuhuma kuwa anajihusisha na biashara ya dawa hizo huku baadhi ya vifungu vikimkariri mbunge huyo.


Mbunge huyo alidai kuwa, hakuwahi kuzungumza na mwandishi wa habari hizo kabla haijatoka na alimwandikia barua mhariri wa gazeti hilo Agosti 3, mwaka huu akitaka aombwe radhi kwa kukashifiwa na kwa kuhusishwa na habari ambayo haikuwa na ukweli wowote pamoja na kuifanya masahihisho habari hiyo lakini ombi hilo alidai Azzan kuwa lilipuuzwa.



  
Jaji Mihayo alisema,gazeti hilo halikumpa nafasi mbunge huyo katika habari hiyo yenye tuhuma nzito hivyo pamoja na mambo mengine,limetakiwa kufanya naye mahojiano ya kina ili kumpatia nafasi stahiki na pia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wahariri wa habari kuwa makini na kuchukua tahadhari zote za kitaaluma wanaposhughulikia habari ambazo vyanzo vyake ni mitandao.


“Kamati imeona hakukuwa na sababu ya kuchapa stori hiyo haraka kabla ya kuongea na muhusika hata kama liliona habari hiyo inaendelea,kwa kuwa taarifa yenyewe ni nyeti na hakukuwa na dalili ya kusubiri kungeleta madhara kwa jamii,” alisema Jaji Mihayo.


  Katika shauri jingine kamati ya maadili ya baraza hilo imeahirisha kusikiliza shauri la mbunge Azzan dhidi ya gazeti la Mwanahabari kutokana na mhariri wake mtendaji,Ramadhan Semtawa kupata udhuru muda mfupi kabla ya kuingia katika kikao cha kamati hiyo.


“Tutalipanga siku nyingine lakini pia kama mkipata nafasi ya kujadiliana wenyewe mkalimaliza haina tabu mtatufahamisha,” alisema Jaji Mihayo na kuongeza kuwa mawasiliano yatafanyika na siku itapangwa baada ya kukubaliana pande zote mbili. MWANANCHI.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: