MBUNGE wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, amesema kitendo cha
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutengua maamuzi yaliyopitishwa na mawaziri;
Dk. John Magufuli (Ujenzi) na Balozi Khamisi Kagasheki (Maliasili na
Utalii), wakati ni wa serikali moja ni uthibitisho kwamba utawala wao
umefitinika, hivyo hauwezi kuwa na mipango mizuri ya kuliletea taifa
maendeleo.
Msigwa ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
alisema hayo jana wakati akichangia mjadala wa hoja ya Mapendekezo ya
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2014/2015 uliowasilishwa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, bungeni
juzi.
Alisema katika moja ya mikutano, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, aliwahi
kusema kwamba Waafrika wana kila kitu na kwamba hawana sababu yoyote ya
kuwa nyuma katika maendeleo isipokuwa tatizo walilonalo ni uongozi.
Msigwa alisema kinachojadiliwa na wabunge, kuanzia juzi ni mpango wa
maendeleo, ambao serikali ndiyo inayousimamia, lakini inashangaza kuona
mawaziri wengi hawapo bungeni.
“Angalia mawaziri wako wapi? Spika jana amezungumza hapa. Hawapo. Ambao
mnatakiwa mchukue mawazo yetu ili mkaya-accommodate (mkayaingize) kwenye
huu mpango. Hampo. Hatuelewi wako wapi. Wapo wawili watatu. Hamtoshi.
Hii inaonyesha kwamba hampo serious (makini),” alisema Msigwa na
kuongeza:
MAAMUZI YA MIGONGANO, HASARA
“Na ndiyo maana serikali hii hii leo anaondoka Magufuli anasema wenye
malori wasimamishe (malori) barabarani. Analeta hasara kwenye Taifa
karibu Sh. bilioni 20. Anakuja Waziri Mkuu anasimamisha (amri ya
Magufuli). The same government (Serikali ileile).”
Aliendelea kusema kuwa: “Anaondoka Waziri wa Maliasili anasema Loliondo
waondoke, anakuja Waziri Mkuu anasimamisha. The same government
(serikali hiyo hiyo). Utawala wenu umefitinika. Hatuwezi tukawa na
mipango mizuri wakati nyumba yenu haimjaiweka vizuri.”
Waziri Magufuli aliagiza kuondolewa kwa msamaha wa asilimia tano kwa
uzito wa magari yanaopita kiwango kiliochopo, msamaha ambao umekuwa
ukitumika nchini kwa zaidi kwa zaidi ya miaka saba sasa. Badala yake
aliagiza kuanzia Oktoba mwaka huu kila gari litakalozidisha uzioto
litatozwa faini ya mzigo uliozidi bila kujali msamaha huo.
Kutokana na maamuzi ya Magufuli ambayo yalianza kutekelezwa Oktoba mwaka
huu, wenye malori na mabasi walianza mgomo ambao uliendelea kwa siku
kadhaa hasa malori.
Hali hiyo ilitishia kuanguka kwa sekta ya usafirishaji nchini, hivyo
kumfanya Pinda kuingilia kati baada ya siku tano kwa kutengua agizo la
Waziri Magufuli na kuagiza kurudiwa kwa utaratibu wa zamani wa msamaha
wa asilimia tano ya ziada ua uzito ambao hautatozwa faini.
Aidha, Pinda alitengua tangazo la Waziri Kagasheki la kuligawa eneo la
Pori Tengefu la Loliondo, wilayani Ngorongoro, mkoa wa Arusha.
Katika uamuzi wa Kagasheki alikuwa ametenga kilomita za mraba 1,500
za pori hilo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,000 kwa ajili ya
kuendelea kuwa chini ya miliki ya serikali na kuachia vijiji kilomita za
mraba 2,500.
Tangazo hilo lilitolewa na Waziri Kagasheki, Machi 19, mwaka huu ili
serikali ihifadhi eneo la kilomita za mraba 1,500 ambalo alieleza kuwa
ni mapito na mazalia ya wanyamapori, pia kutunza ikolojia ya Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti. Tangazo hilo liliibua mgogoro mkubwa.
MAWAZIRI KIDUCHU
Mbali na Msigwa, wabunge wengine waliohoji sababu za kuwapo mawaziri
wachache bungeni wakati wa mjadala huo jana, kinyume cha agizo la Spika
wa Bunge, Anne Makinda, ni James Mbatia (Kuteuliwa-NCCR-Mageuzi),
Modestus Kilufi (Mbarali-CCM), Kombo Khamis Kombo (Mgogoni-CUF) na
Charles Mwijage (Muleba Kaskazini-CCM).
Hali hiyo ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),
Profesa Mark Mwandosya, kusimama na kusema kuwapo au kutokuwapo kwa
mawaziri bungeni bado wanathamini yanayojadiliwa na wabunge.
Alisema macho na masikio ya serikali wakati wa Bunge yanakuwa Dodoma na
kwamba, katika kila ofisi ya serikali kuna runinga, hivyo wanafuatilia
yanayojiri bungeni.
Alisema bungeni kuna maofisa wa serikali wanaorekodi kila
kinachozungumzwa na kwamba, mawaziri wanapokuwa hawapo bungeni, basi
kunakuwa na sababu.
Juzi wakati akiahirisha Bunge, Spika Makinda aliwataka mawaziri wote
kwenda bungeni jana kwa ajili ya majibu kwa kuwa hoja (Mpango wa
Maendeleo wa Taifa) inayojadiliwa inagusa wizara zote.
Awali, Msigwa alisema katika siku za hivi karibuni lugha ya viongozi
imekuwa ni kusisitiza kuomba amani na utulivu kila mahali wanaposimama.
Lakini akasema amani ni tunda la haki, ambayo ikiwekwa mahali pake watu hawahitaji kugombana na pia hakuwezi kutokea fujo.
“Amani ya nchi hii haitalindwa na vifaru vingi, haitalindwa kwa kuongeza
wanajeshi wengi. Amani ya nchi hii itatokana pale haki, wananchi
wanapopata haki zao, wananchi wanapotendewa haki, wananchi wanapopata
huduma zile ambazo wanastahili kuzipata,” alisema Msigwa.
Alisema kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa katika mfumo wa chama kimoja,
lakini pamoja kuwako kwa mabadiliko ya mfumo huyo kwa kuanzishwa vyama
vingi nchini, kuna watu kwenye fikra zao hawaamini hilo.
“Kwa hiyo, wanaona watu wengine ambao hawana imani kama yao, ni watu wanaoleta vurugu,” alisema Msigwa na kuongeza:
“Nilitaka niwakumbushe walioko madarakani kwamba we are here to stay
(tutaendelea kuwako). Tuko hapa kwa mujibu wa katiba, sisi siyo
intruders (wavamizi), ni Watanzania, watawala mnatakiwa mu-accommodate
(kuchukua) mawazo tunayoyaleta hapa kwa ajili ya mustakabali wa taifa
letu. Aidha, tuishi pamoja kama Watanzania na kujenga Taifa letu.”
Alielezea hali ya kuzorota kwa maendeleo kwamba kwenye majimbo mpaka leo
hata nusu ya fedha iliyotolewa mwaka jana haipo, serikali inathubutu
kuja na mpango mpya, ambao hauna jipya.
Msigwa alisema Wizara ya Maliasili na Utalii ni ya pili baada ya Wizara
ya Nishati na Madini kuiingizia serikali fedha za kigeni, lakini katika
mpango huo imewekwa kama Chuo cha Mkwawa, ambacho kimeelezewa kwa
uchache.
Alisema Mpango huo hauonyeshi mazingira ya kuiwekea maliasili ili
kuongeza utalii nchini, kama yale ambayo serikali imewawekea wawekezaji
wa madini, ambao wameondoka na kuwaachia Watanzania mashimo.
MWAIPOSA: VIPAUMBELE VICHACHE
Mbunge wa Ukonga (CCM), Eugen Mwaiposa, aliishauri serikali kuangalia vipaumbele vichache ili iwe rahisi kuvitekeleza.
MSHAMA: RAIS ANADANGANYWA
Mbunge wa Nkenge (CCM), Assumpter Mshama, alisema kuna watu, ambao
hawamwambii Rais ukweli hali ambayo imekuwa ikikwamisha mambo.
“Hivi kweli inafikia tarehe 30 wabunge hatujalipwa mishahara kama unafanya kazi kwa mhindi?” alihoji Mshama.
NTUKAMAZIMA: AIBU YA TANZANIA
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina, alisema ni aibu kwa nchi
kama Rwanda kuwa na ndege saba, lakini Tanzania isiwe na ndege hata
moja.
MBATIA: UMASIKINI WA MIPANGO
Mbatia alisema tatizo kubwa la serikali ni umaskini wa mipango
inayopanga na kushauri iwekeze kwa kiasi kikubwa kwenye bandari ili
kuepuka mazoea ya kukopa. CHANZO:
NIPASHE
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / MHE MSIGWA: KITENDO CHA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA KUTENGUA MAAMUZI YA MAWAZIRI DK MAGUFULI NA KAGASHEGKI NI UTHIBITISHO KUWA SERIKALI IMEFITINIKA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment