BENARD MEMBE.
SAMWEL SITTA.SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa msimamo wa Tanzania, akisema haina mpango wa kujitoa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), bali itaendelea kuwepo licha ya kutengwa na baadhi ya nchi wanachama, wadau wamempongeza huku wakiwabeza mawaziri wake.
Wakizungumza na gazeti hili, wadau hao wakiwemo wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida, walisema kuwa msimamo wa Rais Kikwete una nia njema japo ulipaswa kutolewa mapema kabla mgogoro huo kufikia hapa.
Wadau hao walibeza kauli za kejeli zilizotolewa awali na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afirika Mashariki, Samuel Sitta, kwamba zililenga kukuza mgogoro.
Membe ndiye alikuwa wa kwanza kutoa kauli kuhusu mgogoro huo, akisema kuwa Tanzania inangojea talaka kutoka kwa wanachama wenzake, kisha Sitta akaliambia Bunge kuwa Tanzania ndiyo itatoa talaka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisifu hotuba ya Rais Kikwete, lakini akasema kuwa kauli za mawaziri hao zilikuwa za kuwachanganya Watanzania.
Alisema mawaziri hao kabla hawajatoa matamko yao, walitakiwa kuwasiliana na rais ambaye ana uwezo mkubwa wa kuzungumza na marais wenzake ili kujua sababu ni nini.
Hata hivyo, Dk. Bana alisema alichokifanya Rais Kikwete ni cha kupongezwa, kwa kuwa kawaweka Watanzania sawa na kuelewa nini kinachoendelea.
“Rais ana uwezo wa kukutana na marais wenzake hawa watatu, na pia anatakiwa kuwaambia wanachokifanya sasa wanakiuka katiba ya jumuia kama makubaliano yanavyosema,” alisema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu na Sheria (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema rais kulihutubia Bunge na Watanzania ni jambo zuri maana anakaa kimya muda mrefu.
Mwanaharakati huyo alimshauri Rais Kikwete kuitisha vikao halali na kuwahoji marais hao sababu za kuitenga Tanzania na kisha kufanya uamuzi halali.
Kuhusu suala la ujangili, Bisimba alisema kuwa ameona furaha kwa rais kugundua kasoro zilizojitokeza kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili na kuahidi waliohusika kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Hapa rais amesema na ni bora kagundua kuwa operesheni hiyo ilikumbwa na dosari kadhaa kwa watu kuuawa, mali kuibiwa na hata kuharibiwa, hivyo ni vyema kama alivyoagiza sheria ikachukuliwa kwa walioharibu operesheni hii kwa maslahi yao,” alisema.
Mratibu wa Mtandao wa Kutetea Haki za Binadamu (THRD-Collition), Onesmo Olengurumwa, alisema rais amefanya vizuri, lakini katika mambo ya kitaifa makubwa na ya hatari, alitakiwa kujitokeza mapema.
Olengurumwa alisema katika suala la ujangili, rais amechelewa kujitokeza kwa kuwa walianza kulipigia kelele tangu awali kasoro zilipoanza kujitokeza ila ilichukuwa muda kuchukua hatua.
“Rais amezungumza vizuri sana jana, lakini mambo magumu, mazito ya kitaifa alitakiwa kujitokeza mapema maana tayari operesheni imedhuru, watu kuuawa na hata kuharibiwa mali zao,” alisema.
Viongozi wa dini
Baadhi ya viongozi wa dini nao walipongeza hotuba ya Rais Kikwete, wakisema imeonyesha namna kiongozi huyo alivyokomaa katika siasa za kimataifa na uwezo mkubwa wa kuongoza nchi.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, walisema kuwa ujasiri alioonyesha ni wa kujivunia kwa kila Mtanzania.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kuwa Rais Kikwete hakukurupuka katika uwasilishaji wa hotuba hiyo, kwa kuwa imeonyesha namna alivyojaa hekima, busara na ukakamavu juu ya masuala yanayoikabili nchi kwa sasa.
Alisema kuwa baadhi ya makundi walifikiria juu ya suala la kujiondoa katika jumuiya, lakini Rais Kikwete hakuja na wazo hilo kwa kuwa anajua wazi bila Tanzania umoja huo usingeweza kufikia hatua hiyo.
Skeikh Salum alisema kuwa Tanzania ndiyo msingi wa umoja huo, na hivyo suala la kutaka kujiondoa lingeweza kuchangia kutupa hasara kutokana na kuwa waanzilishi wa jumuiya hiyo.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Ubungo Kibangu (GRC), Anthony Lusekelo, alisema kuwa hotuba imejaa ukomavu wa kisiasa, na imeonyesha wazi namna Tanzania inavyohakikisha inatetea majirani zake.
Alisema kuwa suala la Afrika Mashariki ni la muhimu kwa kuwa Tanzania ndiyo mwanzilishi wa umoja huo kuliko nchi nyingine yoyote katika jumuiya hiyo.
Lusekelo alisema kuwa hotuba hiyo imeonyesha Rais Kikwete alivyo mvumilivu na si kiongozi wa kukurupuka katika kutoa uamuzi wake kama alivyolizungumza suala la katiba ya nchi na la jumuiya.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, alisema kuwa Rais Kikwete ameonyesha ukomavu wa hali ya juu.
Alisema kuwa ameweza kuzungumzia mambo muhimu na nyeti ambayo yanagusa mtima wa kila Mtanzania kwa wakati wote wa maisha na maendeleo ya jamii kutokana na kila eneo kubeba umuhimu unaojitegemea.
Wananchi
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam walimtaka Rais Kikwete kuacha kung’ang’ania kwenye jumuiya hiyo kwa kuwa Tanzania inaweza kujiendesha bila kuwamo.
Wakizungumza na gazeti hili, wakazi hao walisema hakuna sababu ya kuendelea kuwepo kwenye jumuiya iwapo baadhi ya nchi wanachama zinaitenga Tanzania kwa sababu zisizo na mashiko.
Stella Meero mkazi wa Wazo Hill, alisema taifa hili lina fursa nyingi hasa kwenye ardhi, hali inayowafanya majirani kutamani kuimiliki.
“Nimefika Rwanda na Kenya, nafahamu vizuri, yaani najua jinsi wanavyotamani kuja Tanzania, hasa unapozungumza nao kuhusu kilimo udenda unawatoka.
“Mimi naona bora tukae pembeni, Watanzania tunajijua tulivyo wazembe kwenye utekelezaji wa mambo muhimu. Pia hatuwezi kuchangamkia fursa hadi tusukumwe, tukikubali kila kitu kwenye jumuiya tutaumia,” alisema.
Michael Kimaro alisema hakuna umuhimu wa kuungana na watu wasiotaka, hivyo alishauri kuangalia uwezekeno wa kujitoa kwenye jumuiya hiyo.
“Kama hawatutaki na sisi tukilazimisha watukubali tutanyanyasika mbele ya safari baada ya hapo, Wakenya ndio watakaoonja joto ya jiwe maana Tanzania ni soko kubwa la bidhaa zao, hasa kwa Afrika Mashariki na Kati.
“Tazama ajira za Wakenya na Waganda kwenye shule za watu binafsi, ifike wakati tukubali hatutakiwi, tukae chini tujipange. Mbona tuna rasilimali ambazo hakuna nchi yoyote kati ya Kenya, Uganda na Rwanda wanaweza kusogelea,” alisisitiza Michael.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (Bavicha), John Heche alisema katika jumuiya, Tanzania inaongoza kwa kuwa na rasilimali nyingi kama ardhi, mbuga za wanyama na mito, hivyo zingetumiwa vizuri kuna soko la kutosha ukilinganisha kuna bandari.TANZANIA DAIMA.

0 comments:
Post a Comment