DAR ES SALAAM.
SIKU moja baada ya Serikali kutangaza kupunguza viwango vya ufaulu kwa mtihani ya kidato cha nne na sita, baadhi ya wasomi na wadau wa elimu wameponda uamuzi huo na kusema una malengo ya kisiasa.
Baadhi ya wadau hao wakizungumza na gazeti hili
jana, walisema Tanzania imeweka rekodi kwa nchi za Afrika kwa kuwa na
kiwango kidogo sana cha ufaulu cha alama F kuanzia 0 mpaka 19.Waziri wa wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa.
Walisema, Serikali imechukua uamuzi huo kisiasa
ili kuhakikisha kuwa, wanatimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa
Sasa (BRN), ambalo ni kuhakikisha matokeo ya ufaulu kwa Mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka huu yanafikia asilimia 60 kutoka 33 ya mwaka jana.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Herme Mosha alisema kuwa kilichofanywa na Serikali ni
kupanua wigo wa watu kufaulu.
“Wanataka watu ambao walikuwa wanapata daraja la
nne wapate daraja la tatu, daraja la tatu wapate la pili na la pili
wapate la kwanza.
Hata hivyo, kwa muda wote, wadau wa elimu ambao
wanataka siyo kuona tu watu wanafaulu, wanataka elimu iliyo bora. Kwa
hatua hii waliyoichukua haitasaidia lolote katika kuongeza ubora wa
elimu ambao umekuwa kilio cha muda mrefu,” alisema Profesa Mosha.
Alisema kuwa, washikadau wengi wangependa kuona ubora wa elimu umeongezeka na siyo kuongeza wigo wa ufaulu.
“Huku ni kujidanganya, jambo la kwanza wangetakiwa
waende katika shule mbalimbali waone ni nini walimu wanataka, tatizo
lipo wapi halafu wachukue hatua kwa sababu ukiangalia sasa ni kama kuna
mgomo fulani hivi,” alisema.
Kwa upande wake Dk Kitila Mkumbo ambaye ni Mkuu wa
Idara ya Saikolojia ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema tatizo la elimu Tanzania
halijawahi kuwa ni viwango vya ufaulu.
“Wanataka tu kuona hiyo asilimia 60 waliyojipangia
inafikiwa. Walijiwekea lengo hilo wakijua kabisa kwenye elimu hakuna
miujiza, lazima mtu ufanye kazi ndiyo matokeo yaonekane,” alisema.
Alisema kiwango cha kufeli kilichowekwa kinaifanya Tanzania kuwa nchi yenye viwango vidogo sana vya elimu kwenye bara hili.
“Burundi wenyewe mtoto akipata 50 ndiyo anakuwa
amefeli, sisi huku tumeweka mpaka 19 ndiyo tunasema amepata hiyo F,
lakini bado tunaita amefaulu, huu ni utani,” alisema. MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment