Rais Kikwete amesema mara baada ya Rais Mandela kutolewa gerezani hofu ilitawala Afrika ya Kusini, watu wengi wakitambua kuwa atakapochaguliwa kuwa Rais badala ya kuijenga nchi ataanza kulipiza visasi kwa wale wote waliotumika kwa namna moja ama nyingine kumtesa yeye na watu wa nchi yake.
“Badala yake Mzee Mandela alitoa tamko la kuwasamehe wote waliohusika kuwabagua watu wa Afrika ya Kusini, na kisha aliunda tume maalumu ya maridhiano ili kujenga umoja kati ya watu wenye ngozi nyeupe na wenye ngozi nyeusi, jambo hili ni la ajabu sana” amesema Kikwete.
Amesema haya yote yanatafsiri ukaribu na undugu wa hali ya juu kati ya nchi zetu mbili na ndiyo maana katika kumuenzi leo hii kwenye shughuli za kutimiza miaka 52 ya uhuru hatutakuwa na vikundi vya kutumbuiza.
Ibada maalumu ya Mandela
Johannesburg. Afrika Kusini, jana ilitawaliwa na ibada na maombi yaliyofanyika katika makanisa mbalimbali kuliombea taifa, baada ya kifo cha Rais wa Kwanza mzalendo, Nelson Mandela.
Rais Jacob Zuma alikuwa miongoni mwa waumini wa Kanisa la Bryanston Methodist, Johannesburg katika ibada ambayo pia ilihudhuriwa na mtalaka wa Mandela, Winnie Madikizela pamoja na mjukuu mkubwa, Mandla.
Ibada za aina hiyo ziliendeshwa kila kona ya nchi, zikiwaweka pamoja Waafika Kusini ambao waliitikia wito wa Rais Zuma wa kuitumia Jumapili kuliombea taifa hilo.
Nyimbo za dini zilisikika katika kumbi za ibada na makanisa, ambako viongozi wa Serikali wakiwamo Naibu Rais wa Afrika Kusini, Kgalema Motlante na Rais Mstaafu, Thabo Mbeki walikuwa miongoni mwa waliopangiwa kushiriki katika ibada hizo.
Katika Kanisa la Baptist, baadhi ya waumini wakiwa katika mavazi rasmi walionekana wakiimba na kucheza, kabla ya Rais Zuma kupewa nafasi ya kuzungumza.
“Kwa nchi yetu, kifo cha Baba Madiba ni hasara ya aina yake. Waafrika Kusini tunapaswa kuomba tukikumbuka mambo mema ya kiukombozi na uhuru, amani, msamaha, haki na kujali ambayo Mandela aliyapigania na kuyasimamia,” alisema Zuma.
Kwa upande mwingine, mamia ya wafuasi wa Chama cha African National Congress (ANC), walifurika katika Ukumbi wa Benki ya Standard, Johannesburg kushiriki katika maombi, wakiitikia wito wa Rais Zuma.
Mwandishi wetu alishuhudia makada wa chama hicho wakiwa katika mavazi rasmi, wakicheza muziki wa Injili na baadaye wakishiriki maombi yaliyowahusisha waumini wa madhehebu ya Kikristo, Kiislamu, Kihindu, Kiyahudi, Bahai na wale wanaoamini katika imani za jadi.
Qunu kimya.
Wakati nyimbo na ngoma zikichezwa kwa ajili ya kusifu kazi alizofanya Mandela, katika Kijiji alichokulia Qunu, eneo la Mthatha kuliripotiwa kuwa kimya huku wakazi wake wakikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Mandela.
Wanakijiji hao wameamua kukaa nyumbani wakiomboleza na inaaminika kwamba wengi hawaamini kilichotokea na pengine wanasubiri kushuhudia mwili wa kiongozi huyo utakapofikishwa huko Jumamosi kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumapili.
Hata hivyo, hali ni tofauti katika Kijiji cha Mvezo alikozaliwa Mandela, ambako tangu Ijumaa, wakazi wake wamekuwa wakiamka asubuhi na kushiriki katika ibada na maombi hadi adhuhuri, kisha kurejea tena jioni.
Kitukuu wa Mandela, Mambui alisema hali katika kijiji hicho kilichopo umbali wa Kilometa 25 tu kutoka Qunu ni ya huzuni na kwamba watu wake wamekuwa wakiomboleza kwa kulia machozi hasa wanapokuwa katika nyumba zao.
“Ni machozi ya huzuni na maumivu moyoni, siyo machozi ya furaha hata kidogo,” alisema Mambui alipokuwa akihojiwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Afrika Kusini (SABC), jana asubuhi. MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment