BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM NDIYO KILICHOIBUA UOVU KATIKA OPERESHENI TOKOMEZA UJANGILI NA MAWAZIRI MIZIGO WATANG'OKA WENGI TU.


 

KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi (CCM), Bw. Nape Nnauye, amesema chama chake ndicho kilichoibua uovu uliofanyika katika "Operesheni Tokomeza Ujangili" na kusababishsa Bunge kuunda kamati teule ya kuchunguza jambo hilo.
 


Bw. Nnauye aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha "Tuongee Asubuhi", kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Star.
Alisema chama hicho kilibaini dosari hizo katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Bw. Abdulrahman Kinana, katika Jimbo la Kisesa, Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu. 



Aliongeza kuwa, katika ziara hiyo, Bw. Kinana alipokea malalamiko ya wananchi wa jimbo hilo kutoka kwa Mbunge wao, Bw. Luhaga Mpina kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika utekelezaji wa operesheni hiyo. 



Hata hivyo, baada ya kusikia kilio hicho chama hicho kilichukua uamuzi wa kulifikisha jambo hilo kwenye Kamati Kuu ya CCM na kuagiza operesheni hiyo isimamishwe ili kupisha uchunguzi wa vitendo hivyo. 



"Baada ya Mawaziri wanne kuwajibishwa bungeni wiki iliyopita, wale walioshindwa kusimamia wizara zao nao hawatapona...kazi hiyo itaendelea ili kuimarisha utendaji wa Serikali," alisema.
Alisema kutenguliwa uteuzi wa Mawaziri wanne na Rais Jakaya Kikwete, haimaanishi kuwa hoja ya mawaziri 'mizigo' itakufa bali lazima waendelee kuwajibishwa kwa udhaifu wao wa kushindwa kusimamia wizara zao na kusababisha malalamiko kwa wananchi.



Kwa mujibu wa Bw. Nnauye na Bw. Kinana, mawaziri ambao wanadaiwa kushindwa kusimamia wizara zao ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda pamoja na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa. 



Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza na Naibu wake, Bw. Adam Malima, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Celina Kombani. 



Mawaziri ambao Rais Kikwete alitengua uteuzi wao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. David Mathayo. 



Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Julius Mtatiro, alisema tatizo lililopo nchini ni ombwe la uongozi, hivyo lazima wananchi waikatae Serikali ya CCM kwenye sanduku la kura mwaka 2015.



Alisema ni jambo la kushangaza kuona Serikali inachukua hatua wakati tayari madhara makubwa kwa binadamu yameshatokea na kusisitiza kuwa, mfumo wa kulindana serikalini lazima wananchi waukatae na kukikataa chama tawala. 



Aliongeza kuwa, Watanzania wamechoka kushuhudia matukio mabaya ya kukatisha maisha yao na mateso ya kinyama wakati Serikali ikiendelea kulalamika na kusisitiza dawa ya kumaliza matatizo hayo ni kuiondoa madarakani kwa njia ya kura.



Naye Mkuu wa Idara ya Dola na Vyombo vya Uwakilishi kutoka Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. Faustine Sungura, alisema kazi iliyofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake, Bw. James Lembeli ambaye ni Mbunge wa Kahama, mkoani Shinyanga ni utekelezaji wa ilani ya CCM. 



"Ni jambo la kushangaza kuona CCM yenye uwakilishi hadi ngazi ya balozi wa nyumba kumi, ishindwe kubaini kasoro zilizojitokeza katika operesheni hii hadi ilipoundwa Kamati ya Bunge na kubaini uozo wa kutisha. 



"Ndio maana hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kunukuliwa akisema, 'Chama legelege huzaa Serikali legelege'...CCM ilipaswa kuwa macho wakati wote na kulinda rasilimali za nchi na si kuendesha mambo kwa njia ya operesheni," alisema.
Aliongeza kuwa ni jambo la aibu nchi kuendeshwa kwa matukio badala ya mipango mahususi ya muda mrefu. 



Lembeli apokelewa jimboni
Katika hatua nyingine, wakazi wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, juzi walimpongeza Mbunge wa jimbo hilo, Bw. James Lembeli kwa kufichua ukweli wa kilichotokea katika operesheni hiyo. 



Walisema operesheni hiyo ilikuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, mauaji ya watu, mifugo na ukatili mkubwa uliofanywa kwa wananchi wasio na hatia. 



Pongezi hizo zimetolewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya CDT, mjini humo baada ya Bw. Lembeli, kuandaliwa mapokezi makubwa akitokea mjini Dodoma. 



Taarifa iliyosomwa na Bw. Lembeli bungeni mjini Dodoma kuhusu tathmini ya kilichotokea katika operesheni hiyo, ilisababisha Rais Jakaya Kikwete atengue uteuzi wa Mawaziri wanne ambao wizara zao zinadaiwa kuhusika na unyanyasaji huo. 



Katika mkutano huo, wakazi hao walisema Bw. Lembeli aliifanya kazi hiyo kwa kutanguliza uzalendo na masilahi ya nchi badala ya kuficha ukweli wa manyanyaso na machungu waliyoyapata wananchi. 



Awali Diwani wa Kahama Mjini, Bw. Abas Omari (CHADEMA), alimpongeza Bw. Lembeli na kamati yake kwa uzalendo ambao wameuonesha katika taarifa yao ambapo operesheni hiyo imewafanya baadhi ya wananchi kupoteza maisha. 



Alisema wengine wamepata vilema vya kudumu, kuporwa mali zao na kuachwa maskini, kubakwa, mifugo yao kuuawa, kuibwa pamoja na kulazimishwa kufanya mapenzi na miti. 



Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Bw. Machibya Jidulamabambasi, alisema kazi iliyofanywa na Bw. Lembeli imewapa faraja waliotendewa mabaya, katika hiyo ukweli umefahamika. 



Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Lembeli alisema vitendo vya kinyama vilivyofanywa katika operesheni hiyo vilikiuka misingi ya haki za binadamu. 



Alisema mambo waliyoyabaini baada ya tume yao kumaliza kazi waliyopewa yanatisha na kuhuzunisha, hivyo Bunge lilifanya kazi nzuri ya kutaka mawaziri wanne wawajibishwe kwa kushindwa kuisimamia operesheni hiyo ambayo ilikuwa chungu kwa wananchi. 





"Ukiukaji wa haki za binadamu katika operesheni hii, ulisababisha Mawaziri wanne kuwajibika... nampongeza Rais Kikwete kwa kuridhia msimamo wa wabunge ambao waliguswa na mambo waliyoyasikia," alisema. MAJIRA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: