DK SLAA.
KIGOMA/DAR ES SALAAM.
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa leo atakuwa na ziara ya siku moja katika Jimbo la Kigoma Kaskazini ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku tisa mkoani Kigoma kwa ajili ya kuimarisha chama.
Jana jioni, Dk Slaa alifanya mkutano wa hadhara
Mjini Manyovu na kusema kuwa hatishwi na waandamanaji wala vitisho vya
kuuawa na kusisitiza kuwa ataendelea na ziara yake kama kawaida hadi
Kigoma Mjini.
Awali, akihutubia katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kijiji cha Malumba wilayani Kasulu, juzi Dk Slaa
alisema siyo mara yake ya kwanza kutishwa na kusema analindwa na Mungu.
Licha ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi
ya wanachama wanaodai kupinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake
zote, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe alisema ataendeleza
kazi kuimarisha uhai wa chama kama ratiba ilivyopangwa.
Akiwa katika jimbo hilo linaloongozwa na Zitto, Dk
Slaa atatembelea Vijiji vya Nyarubanda na Kidahwe na kufanya mikutano
ya hadhara inayosubiriwa kwa hamu na wadau wa siasa nchini kutokana na
mzozo huo uliokikumba chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kigoma Kaskazini,
Ally Kisala alisema maandalizi ya mikutano hiyo yamekamilika na kwamba
hakuna hofu yoyote ya kutokea vurugu katika mikutano hiyo.
“Tumedhibiti aina yoyote ya vurugu iliyokusudiwa
licha ya kuwapo baadhi ya watu wanaotamani hayo yatokee kwa lengo lao
binafsi, sambamba na kunufaisha masilahi ya makundi binafsi, lakini
hayatatokea,” alisema.
Juzi, wanachama na wafuasi wa Chadema wanaomuunga
mkono Zitto waliandamana kupinga ziara ya Dk Slaa katika jimbo lao
kupinga hatua ya kumvua mbunge wao madakara.
“Tunaamini mikutano yote ya kesho (leo Jumanne)
itafanyika vizuri na watu watapata ujumbe kutoka kwa Katibu Mkuu wetu
(Dk Slaa), na pengine wale wanaopiga kelele na kutaka kuleta mgawanyiko
ndani ya chama watapata fursa ya kuujua ukweli wa mambo ndani ya chama.
“Vita yetu si kukigawa chama, bali ni kuhakikisha tunaingia Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Kisala.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Zedekia
Makunja alisema jeshi lake limejipanga kuhakikisha usalama unakuwapo
katika ziara hiyo.
“Tunawajibika kuhakikisha usalama unakuwa vizuri
na kila jambo linaendelea kama lilivyopangwa. Mwito wangu kwa viongozi,
wanachama na wapenzi wa Chadema ni kuhakikisha wanamaliza tofauti zao
mapema ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, hatupendi kuona
askari wetu wakilazimishwa kutumia nguvu kudhibiti hali ya usalama,”
alisema Makunja. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment