MADIBA NAMNA ALIVYOMSHANGA NYERERE MSASANI JIJINI DAR ES SALAA.
Na Maggid Mjengwa.
Ndugu zangu.
Leo tuendelee na simulizi za Mzee wetu Madiba. Kwenye simulizi hizi tumeona, kuwa Mandela kwenye safari yake ya kuelekea Addis Ababa alifika Dar es Salaam na hadi Msasani , nyumbani kwa Julius Nyerere, Rais kijana wa Tanganyika Huru.
Wakati huo pale Msasani kwa Mwalimu ilikuwa ni kijiji kidogo. Julius Nyerere aliamua kuhama Ikulu na kwenda kujenga nyumba yake Msasani.
Inasimuliwa, kuwa wakati mwingine nyakati za jioni, Julius Nyerere alionekana akicheza bao na majirani zake. Baadhi yao walikuwa ni wa asili ya mikoa ya kusini, hususan Mtwara na Lindi.
Naam, majirani wa Nyerere pale Msasani walikuwa ni wananchi wa kawaida kabisa, kwa wakati huo ni wenye kumudu kuishi kwenye nyumba zao za udongo. Hakika, Julius Nyerere alikuwa kiongozi wa watu na alitaka kuishi miongoni mwa watu wake. Wajifunze kutoka kwake, naye ajifunze kutoka kwao.
Na hili la Nyerere kuishi maisha ya kawaida na yasiyo na anasa linathibitishwa kwenye simulizi hii ya Mzee Madiba kwenye kitabu chake kuhusu maisha yake. Mandela anasimulia alivyomwona Nyerere pale Msasani, anasema;
" I recall that he drove himself in a simple car, a little Austin. This impressed me, for it suggested that he was a man of the people.
" ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg. 347)
Tafsiri ya alichosema ni hii- "Nakumbuka kumwona ( Nyerere) akiendesha gari ndogo ya kawaida aina ya Austin, jambo hili lilinivutia, ilionyesha kuwa alikuwa mtu wa watu." Anasimulia Mzee Madiba. Mandela anasema pia, kuwa Nyerere aliamini katika Afrika na Ujamaa wa Kiafrika.
Akiwa na Nyerere pale Msasani, Mandela alimweleza Nyerere juu ya hali waliyo nayo ( ANC). Juu ya harakati zao za kujikomboa na walipofikia kwa wakati huo. Kisha Mandela akamuomba Nyerere msaada wa hali na mali kwa harakati zao.
Mandela anasema, kuwa Nyerere alionekana kuwa ni mtu aliyekuwa akifuatilia kinachoendelea kwao ( Afrika Kusini). Alimsikiliza kwa makini na alipoongea, Nyerere aliongea kwa kutulia. Hata hivyo, Mandela alishangazwa na mtazamo wa Nyerere juu ya hali waliyokuwa nayo.
Nyerere alipendekeza kwa Mandela, kuwa ( ANC- African National Congress) wasitishe mipango ya harakati zao kwa njia ya mapambano ya silaha hadi hapo Sobukwe atakapotoka gerezani. Sobukwe alikuwa kiongozi wa PAC- Pan African Congress.
Tofauti ya ANC na PAC ilikuwa kwenye mitazamo ya rangi na itikadi. PAC iliamini katika kuikomboa Afrika Kusini bila kushirikiana na weupe kwenye chama cha Kikomunisti cha Afrika Kusini na wala Wahindi. PAC waliamini kuwa Afrika ya Kusini ni ya weusi tu na itabaki kuwa hivyo.
Wakati ANC waliamini katika kuikomboa Afrika Kusini kutoka kwenye minyororo ya ubaguzi, na katika harakati hizo, ANC walikuwa tayari kushirikiana na watu wa Afrika Kusini wenye nia njema katika harakati hizo, bila kujali rangi, dini wala itikadi. Na ndio sababu ya ANC kushirikiana na Chama Cha Kikomunisti kilichokuwa kikiongozwa na weupe.
Ndipo hapa Mandela kwa mara nyingine alibaini, kuwa PAC wamefanikiwa kuwashawishi viongozi wa nchi za Kiafrika kwa kujipa sura ya kuwa wao, PAC, ndio wakombozi halisi wa Afrika Kusini na wakati huo huo, kwenye macho ya viongozi wa Kiafrika, kuwaonyesha ' Wapinzani' wao ANC , kuwa ni chama kinachowakumbatia ' maadui' na kuwa si cha kuaminika.
Akiwa na Nyerere pale Msasani, Mandela alijitahidi sana kujenga hoja kwa kuelezea udhaifu wa PAC, na kuwa, kusitisha harakati za mapambano ya silaha ingekuwa pigo na kurudisha nyuma harakati zao za mapambano ya kuikomboa Afrika Kusini.
Nyerere baada ya kumsikiliza Mandela akashauri; kuwa Mandela akamwone Mfalme Haille Selassie wa Ethiopia. Na Nyerere akamuahidi Mandela kuwa yeye mwenyewe ( Nyerere) angemfanyia utambulisho kwa Mfalme Selassie kabla hajakutana nae.
Je, Mandela atandokaje Tanganyika kwenda Ethiopia wakati hana hata hati za kusafiria kutoka nchi aliyozaliwa ?
Hii ni simulizi endelevu...
0 comments:
Post a Comment