WAHAMIAJI HARAMU 56 KUTOKA ETHIOPIA WAKAMATWA WAKATI WAKIELEKEA KWA MZEE NELSON MADIBA MANDELA MKOANI KILIMANJARO.
Wahamiaji haramu wakiwa katika ofisi za kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro muda mfupi baada ya kufikishwa wakitokea wilayani Same ambako walikutwa wakijiandaa kutaka kusafirishwa kwenda Afrika kusini.
WAHAMIAJI haramu 56, Raia wa nchini Ethiopia, wamekamatwa katika Kijiji cha Jiungeni, Kata ya Ruvu, wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisini Kwake, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz alisema Wahabeshi hao walikamatwa majira ya saa sita usiku, usiku wa kuamkia Juzi, wakiwa katika Lori aina ya Fuso, yenye namba za usajili, T188 AYU, mali ya kampuni ya E.Lyimo ya Mjini Moshi.
Kamanda Boaz alisema baada ya kupata taarifa ya uwepo wa watu wanaotiliwa mashaka kijijini hapo, polisi walianza kufuatilia na kuwahi Gari hilo likiwa na Wahamiaji hao ambao hata hivyo bado haijafahamika walikuwa wakielekea wapi.
“Polisi waliwahi baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi na kukamata wahabeshi 56, walikuwa wanasafirishwa kwenye Lori aina ya Fuso, namba za usajili T188 AYU mali ya E.Lyimo ya mjini Moshi, bado hatujafahamu walikuwa wanaelekea wapi lakini uchunguzi unaendelea,” alisema Boaz.
Kamanda Boaz alisema mbali na Wahabeshi hao 56, Polisi walifanikiwa kuwakamata Watanzania Watatu akiwemo Dereva wa Lori hilo, aliyetambulika kwa jina la Daniel Mfinanga pamoja na wenzake wawili ambao majina yao yanahifadhiwa kutokana na sababu za kiupelelezi.
Aidha Kamanda Boaz aliongeza kuwa Utingo wa Lori hilo, aliyemtaja kwa jina la Ismael Juma, alifanikiwa kutoroka na kwamba jeshi hilo kwa sasa linaendelea na msako ili kumtia mbaroni.
Kundi la wahamiaji haramu zaidi ya 40 wanaodhaniwa kuwa ni wa kutoka Ethiopia na Somalia wakishuka kwenye Lori aina ya fuso katika kituo kikuu cha muda baada ya kukamatwa wilayani Same wakijiandaa kusafirishwa kwenda nchi ya Afrika kusini.
Gari aina ya Fuso lililokutwa likiwa limebeba wahamiaji haramu tayari kuwasafirisha kwenda Afrika kusini.
0 comments:
Post a Comment