JOHANNESBURG.
RATIBA inayoonyesha namna siku kumi za maandalizi ya mazishi ya kitaifa ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela atakayezikwa kijijini kwake Qunu, Eastern Cape, imetolewa.
RATIBA inayoonyesha namna siku kumi za maandalizi ya mazishi ya kitaifa ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, marehemu Nelson Mandela atakayezikwa kijijini kwake Qunu, Eastern Cape, imetolewa.
Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma akizungumza na
waandishi wa habari juzi, alisema kuwa Desemba 8 itakuwa siku ya sala na
kukumbuka mambo aliyoyafanya Mandela.
“Tunawaomba watu wetu wote wakusanyike kwenye
kumbi za mikutano, makanisa, misikiti, mahekalu, masinagogi na nyumba
zao kwa ajili ya sala na kutafakari kuhusu maisha ya Madiba na mchango
wake kwa taifa letu na dunia, “ alisema Zuma.
Kwa mujibu wa CNN, siku hiyo itatumiwa na viongozi
wa kitamaduni kukutana, nyumbani kwa Mandela au chumba cha kuhifadhia
maiti kwa ajili ya kufanya sherehe ya kimila ijulikanayo kama ‘kufumba
macho.’
Viongozi hao watakuwa ‘wakiongea’ na Mandela na mababu zake wakiwaelezea namna mambo yalivyotokea katika kila hatua.
Inaaminika kuwa baada ya sherehe hiyo, mwili wa
Mandela utahifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye hospitali ya jeshi
ya Pretoria.
Ibada rasmi ya kumwombea Mandela itafanyika
Jumanne, Desemba 10 katika uwanja wa michezo wa FNB wenye uwezo wa
kuchukua watu 95,000 uliopo Soweto, mahali ambapo Madiba alionekana
hadharani kwa mara ya mwisho alipokwenda kuangalia Kombe la Dunia Julai
2010.
“Kuanzia tarehe 11 hadi 13 Desemba, mwili wa
mpendwa wetu Madiba utapelekwa katika majengo ya Muungano, yaliyopo
Pretoria, mahali ambako alifanya kazi kama rais wa kwanza katika
demokrasia changa baada ya kuapishwa Mei 10, 1994,” alisema.
Mwili wa Mandela utawekwa kwa siku tatu katika
majengo hayo ili watu waweze kutoa heshima za mwisho. Siku ya kwanza
imetengwa kwa ajili ya watu mashuhuri pekee.
“Katika kipindi chote hicho, ibada za kumwombea zitakuwa zikiendelea kwenye majimbo na mikoa yote,” alisema.
Maelfu ya waombolezaji wanatarajiwa kujitokeza
barabarani Desemba 14 kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mithatha kushuhudia
wanajeshi wakisafirisha mwili wa Mandela kuelekea Kijiji cha Qunu,
mahali atakapozikwa Desemba 15.
Mwili wa Mandela ukifikishwa kijijini kwake,
utakabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi, ambapo
bendera ya taifa itaondolewa kwenye jeneza na kufunikwa kwa blanketi la
kitamaduni la Xhosa kuashiria kurudi kwa mmojawao. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment