BONIFACE NJOHOLE KUZIKWA KESHO KIJIJI CHA MCHOMBE KILOMBERO MOROGORO
Na Mtanda Blog, Morogoro.
MCHEZAJI wa zamani wa klabu ya Reli ya Morogoro na taifa Stars Boniface Njohome aliyefariki dunia jana majira ya saa 5:30 asubuhi katika kijiji Mchombe anatarajiwa kuzikwa kesho jumanne (leo) katika makaburi ya misheni yaliyopo eneo la Ipapa tarafa ya Mng’eta wilayani Kilombero mkoa wa Morogoro.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili dada mkubwa wa marehemu Boniface Njohole, Devotha Njohole alisema kuwa mpaka sasa maandalizi ya mazishi yanaendelea vizuri na ndugu yao atazikwa katika makaburi ya Ipapa ambayo baba yake mzazi Yustine Njohole alizikwa eneo hilo.
Devotha alisema kuwa muda wa mazishi mpaka sasa bado haujapangwa kwa vile anasubiriwa shangazi yao mkubwa Juliana Njohole anayetokea jijini Dar es Salaam ili kuweza kukaa kikao cha familia na kupanga muda wa mazishi pamona na ngudu wengine.
“Njohole atazikwa kesho (leo jumanne) katika makaburi ya misheni eneo la Ipapa lakini muda wa kuzika bado hatupanga kwa sababu tunamsubiri shangazi mkubwa ili tuweze kukaa kikao na ndugu wengine akiwemo mdogo wangu Doris njohole anayetokea Arusha pamoja na ndugu wengine wakitoke Morogoro mjini na sehemu nyingine”. Alisem Devotha.
Naye Karibu mkuu Mtendaji wa chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) Hamis Semka alisema amepokea salamu za pole kutoka kwa shirikisho la soka la Tanzania (TFF) Jamal Malinzi, Chama cha makocha Morogoro kupitia kwa Mwenyekiti wake, John Simkoko na klabu ya Polisi Morogoro inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania bara na kutoa fedha za ubani sh100,000.
Semka alisema kuwa baadhi ya viongozi na wachezaji wa zamani akiwemo yeye, Mwenyekiti wa chama cha makocha Morogoro, John Simkoko, Mratibu wa damu salama kanda ya mashariki, Willy Mathew, mchezaji wa zamani wa Reli Morogoro, Mohamed Mtoni, Hamis Malifedha wataambatana na ndugu, jamaa na marafiki katika mazishi hayo hapo kesho.
Kocha John Simkoko ambaye aliwahi kucheza soka na marehemu Boniface Yustin Njohole katika klabu ya Reli miaka ya 1985 hadi 1988 alisema kuwa Njohole ameacha pengo kubwa katika medani ya soka ukizingatia kuwa alikuwa na nyasfa mbalimbali ndani ya chama cha soka mkoa wa Morogoro (MRFA) na kituo cha Aspare cha Mzumbe kwa kuibua vipaji vya soka kwa vijana.
Simkoko alisema kuwa Njohole licha ya kucheza naye soka klabu ya Reli Morogoro na baadaye kumfundisha kama kocha mkuu katika klabu hiyo alikuwa kiongozi katika chama cha soka Morogoro kama Mjumbe wa kamati na mashindano na Mratibu kituo cha Aspare Mzumbe akiwa na kazi ya kusaka na kuibua vipaji vya soka kwa vijana ameaga dunia wakati Tanzania ikihitaji mchango wake katika harakati za kuendeleza soka hapa nchini.
“Mambo yote ukiniuliza utakuwa umekosa nini kwa Bony baada ya kufa ?, jibu ni majonzi makubwa kwa sababu ni mtu ambaye tulikuwa naye karibu katika soka na mambo mengine na sitaweza kumuona tena, pili alikuwa na kumbukumbu kiasi wengi wetu ambao tupo naye karibu hasa katika michezo ya soka ya Tanzania iwe ya Reli Morogoro ama mingine yeye ndiye alikuwa stoo ya kuhifadhia kumbukumbu”. Alisema Simkoko.
Simkoko akimzungumzia juu ya uwezo wake ndani ya uwanja alisema kuwa marehemu alikuwa na sifa zote za kuwa kiungo katika timu ambapo alikuwa na uwezo wa kunyang’anya mpira, kugawa na kufunga jambo ambalo kila timu alizoweza kuzichezea walifaidikana nazo kwa uwepo wake uwanjani.
Boniface Yustin Njohole ameacha mke na watoto mmoja suzana Njohole ambapo anataraji kuzikwa kesho jumanne katika makaburi ya Ipapa yaliyopo katika kijiji cha Mchombe huku wakati wa uhai wake akizichezea klabu za Milambo ya Tabora, timu ya mkoa wa Morogoro, Reli Morogoro, timu ya mkoa wa Tabora na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na Kiongozi wa chama cha soka Morogoro kama Mjumbe katika kamati na mashindano na Mratibu wa kituo cha Aspare Mzumbe akiwa na kazi ya kuibua vipaji vya soka, mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi-AMINA
0 comments:
Post a Comment