BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DK SHEIN !!! AELEZA MAFANIKIO BAADA YA MAPINDUZI TANGY JANUARI 12/ 1964 BAADA YA ZANZIBAR KUTAWALIWA NA WAKOLONI KWA MIAKA 132.

MAPINDUZI ya Zanzibar jana yalitimiza miaka 50, huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akielezea mafanikio ya kupigiwa mfano, yaliyotokana na uongozi wa kizalendo katika muda huo.

Kutokana na mafanikio hayo, Dk Shein aliyehutubia Taifa jana kutoka Uwanja wa Amaan mjini hapa, aliwataka Wazanzibari kuyaenzi Mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964, kwani ndiyo yaliyowakomboa wananchi wa Unguja na Pemba na madhila ya wakoloni ya utawala wa miaka 132.

Alisema Mapinduzi yalifungua utawala wa kujenga heshima ya binadamu na kulinda utu na usawa wa kila mwananchi bila ya kujali ubaguzi wa rangi. “Tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar tukiwa huru katika nchi yetu na kufaidi matunda haya hatuna budi kuwaombea dua waasisi wa Mapinduzi haya hayati Abeid Amani Karume pamoja na wenzake,” alisema Dk Shein.

Aliwataka wananchi kuimarisha umoja na mshikamano wa Mapinduzi na kukumbusha kuwa hata kauli mbiu ya sherehe za Mapinduzi, imesisitiza umoja ndiyo nguvu ya mwananchi mzalendo. Dk Shein pia aliahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), itaendelea kulinda malengo na dhamira ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa faida ya wananchi wake. Alitoa mfano wa tamko la Serikali la Septemba 23, 1964 alipotangaza elimu bila ya malipo.

Kabla ya Mapinduzi, kwa mujibu wa Dk Shein, zilikuwepo shule 62 zilizokuwa zikitoa elimu kwa kubagua wananchi kwa makabila yao, lakini leo zipo zaidi ya shule 342 za msingi za kizalendo, shule za sekondari 252 na vyuo vikuu vitatu.

“Ndugu wananchi tumepiga hatua kubwa katika elimu na bado tunaendelea kutekeleza malengo ya Mapinduzi katika elimu...kabla ya Mapinduzi hatukuwa vyuo vikuu, sasa vipo vitatu,” alisema Shein.

Katika afya, Dk Shein alisema pia wamepiga hatua kubwa ambapo kwa sasa hakuna mwananchi anayetembea kilometa tano, kutafuta huduma za afya. Kabla ya Mapinduzi, vilikuwepo vituo vya afya 36 sasa vipo vituo vya afya 134, ambapo sasa mwananchi atatembea chini ya kilomita 3 kufikia huduma ya afya.

Mbali na kusogeza huduma za afya karibu na watu, Dk Shein pia alisema maradhi yaliyokuwa yakitishia afya za wananchi kama malaria, yamepungua na kufikia asilimia 0.3.

Pia, Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA), tayari kimeanza kutoa shahada ya kwanza ya udaktari, ambapo kwa kiasi kikubwa tatizo la upungufu wa madaktari litakuwa limepata ufumbuzi wake.

“Tumepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya afya… yalikuwepo maradhi yaliyokuwa yakitishia uhai wa wananchi kama malaria kwa kiwango cha asilimia 45 katika mwaka 1990 na sasa tumeyashusha hadi asilimia 0.3,” alisema Dk Shein.

Kuhusu uchumi, Dk Shein alisema umeimarika na kufikia ukuaji wa asilimia saba na lengo ni kufikia ukuaji wa asilimia 7.5 ifikapo mwakani. Pato la kawaida la mwananchi sasa limefikia dola 656, ambapo mfumuko wa bei umepungua kwa kiwango kikubwa baada ya kuwepo kwa udhibiti ikiwemo bidhaa muhimu za vyakula kupunguzwa kodi ili kutoa nafuu kwa wananchi.

Awali, Dk Shein aliwataka Wazanzibari kuendelea kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao ndiyo kielelezo cha Taifa la Tanzania. Alisema Muungano hivi karibuni, utafikia umri wa miaka 50 na wananchi wa pande mbili zilizoungana, wanayo kila sababu ya kusherehekea.

“Wazanzibari Muungano wetu karibuni utafikia umri wa miaka 50 tangu kuasisiwa kwake na viongozi wa Taifa hili, kwa hivyo nawaombeni mjitokeze kwa wingi kusherehekea,” alisema.

Dk Shein alisema Mapinduzi ya Zanzibar, yanakabiliwa na changamoto mbalimbali na moja ni kutunza mafanikio hayo kwa kudumisha amani na utulivu. Aliwataka wananchi pamoja na wanasiasa na watu wa dini, kujenga tabia ya kutii sheria za nchi ili kulinda Mapinduzi ya Zanzibar.

“Nawaomba wananchi tuige mambo yaliyofanywa na waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar.....kila mmoja atimize wajibu wake ikiwemo kufanya kazi kwa bidii na nidhamu na tuepuke kufanya kazi kwa mazoea,” alisema.

Dk Shein alisema mabadiliko ya kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 2010, yalisababisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ambayo inatokana na maridhiano ya kisiasa. Alisema Serikali hiyo imepata mafanikio kwa kutekeleza majukumu yake kwa kuimarisha amani, umoja, na mshikamano wa Taifa.

“Tumeanza vizuri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambapo amani na utulivu na mshikamano vimeimarika kwa nguvu zote,” alisema.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilali na Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Pia, walikuwepo marais wastaafu akiwemo Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Awamu wa ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Mara baada ya Dk Shein kuingia katika Uwanja wa Amaan akiwa katika gari la wazi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliwapungia wananchi mkono na kuwasalimia. Mizinga 21 ilipigwa kwa heshima yake ikiwa ishara ya kumkaribisha pamoja na kukagua gwaride linaloundwa na vikosi vya JWTZ, Jeshi la Polisi, vikosi vya SMZ vya Mafunzo, Jeshi la Kulinda Uchumi (JKU), Valantia na KMKM na Zima Moto.

Wageni waalikwa katika sherehe hizo ni pamoja na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye alishangiliwa wakati alipoingia katika Uwanja wa Amaan na kufuatiwa na Rais wa Jamhuri ya Comoro, Ikililou Dhoinine pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Miji na Vijijini wa Jamhuri ya Watu wa China, Jiang Weixin.

Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Museveni aliipongeza Tanzania kwa kusaidia uhuru wa Uganda, ambapo Jeshi la Tanzania lilishiriki kikamilifu kupambana na wavamizi. Museveni alizungumza Kiswahili kwa ajili ya kuienzi lugha hiyo, ya Afrika ya Mashariki na kusisitiza umoja na mshikamano wa Tanzania pamoja na Afrika ya Mashariki kwa ujumla.

“Nimeamua kuzungumza Kiswahili cha Afrika ingawa Kiswahili changu ni kibovu, lakini bora kuliko kuamua kuzungumza lugha ya wakoloni,” alisema Museveni huku akishangiliwa na mamia ya watu waliofurika.

Wazanzibari wanaendelea kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo utawala wa Sultani wa Oman ulipinduliwa na wazalendo kuchukua hatamu ya kuongoza dola baada ya kudumu kwa miaka 132.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: