BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DK SHEIN KUWAONGOZA MAELEFU ZANZIBAR KUSHEREHEKEA MIAKA 50 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, RAIS JAKAYA KIKWETE, MUSEVENI NA IKILILOU DHOINIME WA COMORO NI SEHEMU YA WAGENI MASHUHURI.


RAIS wa Zanzibar,Dk.Ali Mohamed Sheni (kulia) akimtunuku Dkt.Salim Ahmed Salim nishani ya Mapinduzi ya Zanzibar jana katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar jana.Picha na Michael Matemanga

RAIS wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein atawaongoza maelfu ya wananchi wa Zanzibar, kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya visiwa hivyo leo.

Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine kutoka nchi mbalimbali akiwamo Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Ikililou Dhoinine wa Comoro na maseneta kutoka miji ya Lamu na Mombasa nchini Kenya, pamoja na mwakilishi maalumu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga mjini Unguja jana, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd alisema kuwa sherehe hizo ambazo ni kilele zitaanza saa 3.00 asubuhi baada ya viongozi wa kitaifa kuwasili, ambapo pamoja na mambo mengine Dk Shein atalihutubia taifa hilo.

Uchunguzi unaonyesha kuwa, wananchi wa visiwa hivyo wanamtarajia Rais Dk Shein kuzungumzia hali ya kiuchumi, kisiasa na kudumisha usalama wa raia kutokana na vitendo vya watu kumwagiwa tindikali, pia harakati za viongozi wa dini na wanasiasa kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.(P.T)


Alipoulizwa kuhusu kualikwa kwa aliyekuwa Sultan wa mwisho wa Zanzibar, Jamsheed Bin Abdullah, alisema kuwa sherehe hizo zilikusudia kuwaalika watu mashuhuri kutoka nchi za SADC na Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), lakini bahati mbaya viongozi hao hawataweza kushiriki kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine.

Hata hivyo, alikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Salmin Amour Juma, iliwahi kutoa msamaha kwa sultani wa mwisho wa Zanzibar ikieleza kuwa mlango uko wazi na anaweza kuitembelea Zanzibar kama mwananchi wa kawaida.

Maadhimisho ya leo yanafanyika ikiwa ni miaka 50, baada ya Mapinduzi yaliyofanywa na Chama cha Afro Shiraz Party (ASP), Januari 12, 1964 chini ya hayati Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ).

Mji wa Zanzibar umepambwa kwa picha za viongozi kuanzia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tangu awamu kwanza hadi ya saba, Bendera za Taifa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku mji ukiwa katika hali ya usafi.

Sherehe hizo zinatarajiwa kupambwa na mambo mbalimbali, ikiwamo vikundi vya ngoma za asili na michezo mbalimbali ya kijadi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: