
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia atachuana vikali na Charles Makofila kuwania uenyekiti wa taifa katika uchaguzi utakaofanyika wiki ijayo. Uchaguzi huo utafanyika kwenye mkutano mkuu wa Januari 18, mwaka huu, jijini Dar es Salaam ukishirikisha wajumbe 289.
Kaimu Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Mosena Nyambabe, alisema Mbatia alishika wadhifa huo mwaka 2000 na anaendelea kuwania nafasi hiyo kwa kuwa Katiba ya chama hicho, haina ukomo kwa uongozi wa ngazi yoyote.
“Tunafahamu kuwa taasisi nyingi hasa za kiraia hapa nchini, zinasisitiza juu ya umuhimu wa nafasi za uongozi kupewa ukomo, lakini ukweli Katiba yetu haijaweka suala hilo la ukomo, labda kwenye mkutano wetu huu mkuu, wakati tukijadili marekebisho ya Katiba huenda likazungumziwa,” alisisitiza Nyambabe.
Alisema mbali na Mwenyekiti wa Taifa, mkutano huo utawachagua Makamu Mwenyekiti kutoka Zanzibar na Makamu Mwenyekiti kutoka Tanzania Bara. Pia, utawachagua wajumbe wanane wanaume wa Halmashauri Kuu kutoka Bara na wajumbe wanne wanaume kutoka Zanzibar ambapo jumla ya wajumbe wote itakuwa ni 24.
Alisema hali ya mwamko wa kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ni kubwa. Alisema wagombea wengine waliibuka kuwania nafasi ya uenyekiti na kushindwa kupita, kutokana na kukosa sifa, hivyo kufanya wagombea halali wa uenyekiti kubaki wawili ambao ni Mbatia na Makofila.
Aidha alisema katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara, wagombea wanne wamejitokeza wakiwamo Leticia Gati, Anyimike Mwasakalali na Rukia Abubakari.
“Ofisi yangu inawatakia wajumbe safari njema na kuwakaribisha jijini Dar es Salaam. Pia, tunaomba vyombo vya Ulinzi na Usalama kutupatia ushirikiano mzuri kwa ajili ya usalama wa vikao hususani kwa wageni wetu” alisema Nyambabe.
Alisema pamoja na uchaguzi huo, Mkutano Mkuu huo pia utapitia Katiba ya NCCR na kuifanyia marekebisho, kama utaona kuna haja ya kufanya hivyo.
Alisema mkutano huo unafanyika baada ya kukamilika kwa uchaguzi katika ngazi za matawi, kata na majimbo.
Alisema Halmashauri Kuu mpya ya chama hicho, itaketi Januari 19, mwaka huu na itawachagua Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na Baraza la Wadhamini.HABARILEO

0 comments:
Post a Comment