MAPINDUZI MATAKATIFU YA ZANZIBAR JANUARI 12, 1964 KUADHIMISHWA LEO
LEO ni Siku ya Mapinduzi, ambapo Wazanzibari na Watanzania kwa jumla wanajumuika kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matakatifu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa katika Uwanja wa Amaan, ambako pamoja na mambo mengine, gwaride rasmi la majeshi ya Ulinzi na Usalama, litakaguliwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Rais Dk Ali Mohamed Shein ambaye pia atahutubia Taifa.
Vyanzo hivyo vilisema hotuba hiyo itarushwa moja kwa moja na vyombo vya habari nchini, kwa maana ya televisheni na redio, ili kutoa fursa kwa Watanzania wote wa Bara na Visiwani ambao hawatakuwa uwanjani hapo kufuatilia.
Mazoezi ya kile kitakachofanyika uwanjani hapo siku ya kilele leo yalikuwa yakiendelea uwanjani hapo na kushuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho Kitaifa, Balozi Seif Ali Iddi, wajumbe wa Kamati hiyo, maofisa wa vikosi vya Ulinzi na Usalama na baadhi ya wananchi.
Mambo yanayotazamiwa kuoneshwa leo ni pamoja na ndegevita za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambazo zitapita kwa ustadi katika anga la Zanzibar na kutoa heshima uwanjani hapo.
Vifaa mbalimbali vya kijeshi vitaoneshwa sambamba na kikosi maalumu cha makomandoo ambacho kitapita na kuonesha ukakamavu na utayari wao wa kukabiliana na maadui.
Kutakuwa pia na onesho maalumu la magari ya kivita yakiongozwa na gari maalumu lenye baadhi ya silaha za kivita, kwa lengo la kuonesha umakini na umadhubuti wa Jeshi hilo.
Pia kutakuwa na onesho la vikosi maalumu vya askari Polisi vinavyoshiriki mapambano dhidi ya uhalifu na uvunjifu wa amani vikiwa na mbwa, farasi na magari ya kutoa maji ya kuwasha.
Askari wastaafu kwa mujibu wa vyanzo vya habari hawatabaki nyuma, kwani waliokuwa wa Jeshi la Ukombozi la Unguja (JLU) wanatazamiwa kuwa kivutio kikubwa kwa wananchi watakaoshuhudia maadhimisho hayo, kwani nao watapita mbele ya jukwaa la wageni rasmi kwa ukakamavu kutoa heshima zao.
Wanafunzi wa shule mbalimbali nao wataonesha ustadi wao katika maonesho ya halaiki maalumu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwani nao watajimwaga uwanjani kuonesha sura mbalimbali za maendeleo ya Zanzibar baada ya Mapinduzi.
Inakadiriwa watoto zaidi ya 2,000 wameandaliwa kwa ajili hiyo kutoka Visiwani na Bara. Watoto hao ambao inaelezwa wamejiandaa barabara, watakonga nyoyo za watakaoshuhudia maadhimisho hayo kwa kucheza sarakasi.
Mapinduzi ya kuung’oa utawala dhalimu wa kisultani yalifanyika usiku wa Januari 12 na baada ya hapo nchi iliongozwa na Shehe Abeid Amaan Karume na baada ya miezi takribani mitatu, ilipotimia Aprili 26, Zanzibar na Tanganyika ziliungana chini ya Shehe Karume na Mwalimu Julius Nyerere na kuzaliwa Tanzania.
HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment