MWENYEKITI WA CHADEMA TAIFA FREEMAN MBOWE AKIMBILIA MAHAKAMANI, LENGO NI KUMBURUZA KORTINI MBUNGE WAKE WA JIMBO LA KIGOMA KASKAZINI.
DAR ES SALAAM.
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe anapanga kumchukulia hatua za kisheria Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutokana na kile alichodai kuwa ni kuzusha tuhuma zenye lengo la kumchafua yeye binafsi na chama hicho.
Tuhuma hizo ni zile zilizowekwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuanzia Januari 6 mwaka huu, zikimnukuu Zitto akieleza kuwa Mbowe amewahi kuhongwa mamilioni ya fedha na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono.
Tuhuma dhidi ya Mbowe ziliibuka baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kumtuhumu Zitto kuwa amehongwa magari mawili na Mkono.
Hata hivyo, Mkono katika taarifa yake alikanusha madai ya Zitto kuhusu kuwapa fedha Chadema, pia alitoa ufafanuzi kwamba hakuwahi kumhonga mbunge huyo magari kama ilivyodaiwa na Lissu bali alimuuzia gari moja na kumkodisha gari la pili.
Taarifa ya kusudio la Mbowe kumburuza Zitto mahakamani ilitolewa jana na Ofisa Mwandamizi wa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, huku ikikanusha tuhuma zote zilizotolewa dhidi ya Mbowe.
“Mbowe ameshawasiliana na mawakili walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria. Mwenyekiti wa chama hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo hata hivyo haikumtaja Zitto moja kwa moja.
Jana gazeti hili lilimtafuta Zitto ili aweze kuzungumzia suala hilo lakini hakupatikana.
Msingi wa taarifa
Taarifa hiyo ilieleza kuwa tuhuma hizo zinasambazwa na watu wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama hicho.
Kauli hiyo ni dhahiri inamlenga Zitto, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, kwani walivuliwa nyadhifa zao kutokana na kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, uliolenga kufanya mapinduzi ya uongozi ndani ya Chadema.
Taarifa hiyo imesema tuhuma zinazoshughulikiwa ni zile zinazodai kwamba Mbowe alichukua Sh40 milioni mwaka 2005 kutoka kwa Mkono ili asifanye kampeni katika Jimbo la Musoma Vijijini.
Tuhuma nyingine ni kuwa 2008 Mkono alimpatia Mbowe Sh20 milioni kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime, kwamba Mbowe alizitoa fedha hizo kwenye chama kama mkopo na akalipwa.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment