Na Juma Mtanda, Morogoro.
MIKASA, vitimbwi na shida ya kila aina namna ilivyowakumba waathirika wa mafuriko inazidi kujitokeza kama baadhi ya familia, ikiwemo ya Mzee Saidi Salehe (63) ambaye ni mlemavu wa macho kusimulia namna walivyolala usingizi katika kiti kimoja cha miguu minne na mke wake Mwajuma Omari kwa siku nane baada ya maji ya mafuriko yaliyojaa kila aina ya uchafu kuvamia makazi yao na kubomoa nyumba tegemezi.
Ni kibanda cha jiko la kupikia kilichojengwa siku chache kabla ya kutokea mafuriko ndicho kiligeuka kuwa hifadhi kwao katika familia hiyo kabla ya serikali kuwanusuru na kuwatoa katika adhabu ya kulala katika kiti hicho huku miguu yao ikiogelea katika maji yaliyojaa yalitotuwama yakitoa harusi kali baada ya maji hayo kusomba kila uchafu kikiwemo kinyesi cha binadamu kufuatia vyoo vingine kubomoka na kutiririsha uchafu huo.
Serikali ilifanya tathimini ya haraka ya kutambua kaya zilizopoteza kabisa makazi kwa nyumba zao kubomoka, huku wengi wa waathirika wakihitaji msaada wa hali na mali kutoka kwa serikali, huku serikali yenyewe ikihitaji msaada kutoka serikali kuu, wadau na taasisi mbalimbali ilimradi kuweza kutoa hifadhi kwa waathirika hao wakiwemo zaidi ya watu 100 ambao walilala usingizi kando ya barabara kuu ya Turiani-Magole kwa siku mbili mpaka siku nne kabla ya baadhi yao kuhifadhiwa na ndugu, jamaa na mafariki.
Mtaro wa maji katika barabara kuu Dodoma-Morogoro eneo la reli ukiwa umeziba na takangumu.
Ni mahema 25 yanayotumika kuhifadhi waathirika hao huku hema moja likitumiwa na familia moja hadi nane kwa kutengewa wanawake na wanaume katika kambi ya waathirika wa mafuriko iliyopo eneo la shule ya sekondari ya Magole wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Mwajuma Omari aliyezaliwa mwaka 1954 anaeleza namna alivyojiokoa yeye na mume wake ambaye haoni kabisa na kushuhudia nyumba ikibomoka na kuanguka chini, mali zikisombwa na maji huku baadhi ya vijana wakitumia mafuriko hayo kuiba mali ikiwemo kumwibia kuku 15, bata saba na mali nyingine.
“Ni kweli haya mafuriko yamenifanya mimi na mume wangu kulala usingizi kwa siku nane katika kiti kimoja cha miguu minne huku miguu yetu ikiwa ndani ya maji kwa siku tatu na hii ilitulazimu kulala katika kibanda cha jiko letu ambacho kidogo kilionekana kuwa juu ya mwinuko lakini tufanya hivyo kwa sababu hatukuweza kupata msamalia mwema wa kutuhifadhi kutokana na majirani zetu nao kukumbwa na mkasa kama wetu”. Alisema Mwajuma.
Baada ya mafuriko kuzingira makazi yetu na majirani jambo la msingi ambalo aliona ni kumtoa mume ndani ya nyumba na kumkimbiza katika kibanda cha jiko la kupikia na kumkalisha katika kiti cha miguu minne kisha muda mchache akishuhudia vijana wakipiga mbizi kwenye maji hayo na kukamata kuku, bata na mali nyingine na kutoweka nazo na alipojaribu kuhoji jibu lililotoka kuwa wapo katika uokoaji kumbe ni wezi tu. Alisema Mwajuma.
Mwajuma alisema kuwa anashukuru kuwa salama yeye na mume wake baada ya kunusurika kifo na kuipongeza serikali kwa kuwapatia hifadhi katika kambi ya waathirika kwani sasa analala sehemu salama tofauti na mateso waliyokuwa wakiyapata ya kulala katika kiti kimoja kwa siku nane na mambo mengine ni majaliwa ya mwenyezi mungu.
“Hema letu tunalala familia mbili na hii serikali imetoa upendeleo kwa sababu mimi nipo na mlemavu wa macho na mwenzangu Pauleti Malogo anaishi na mwanaye ambaye ni mlemavu wa akili”. Alisema Mwajuma.
Mikasa na vitimbwi vya mifuriko hayo hayakuishia kwa familia ya Mzee Said Salehe (63) kwa kulala katika kiti kimoja kwa siku nane bali iliendelea kwa Mzee Hassan Changi (56) wa kitongozi cha Bwawani naye akikumbana na dhahama ya kujiwekea kumbukumbu katika maisha yake hasa baada ya kuteguka kifundo cha mguu na kumlazimu sasa hivi kutembea kwa msaada ya mti.
Akiongea kwa masikitiko katika kambi ya waathirika wa mafuriko hayo, Mzee Changi alisema kuwa kitu ambacho hataweza kusahau katika maisha yake ni kutengeana na mafamilia yake na hakufikilia siku moja ataishi maisha ya kupanga foleni kwa ajili ya kupata chakula cha msaada ilhali alikuwa mtu wa kufanya kila jambo yeye mwenyewe.
“Ninachosikitika kwa sasa ni kutengana na familia yangu, mke wangu na watoto wangu wao walipata hifadhi kwa mtoto wetu na mimi mwenyewe kulala chini kando ya barabara kwa siku mbili na kundi kubwa la wenzangu ambao nyumba zao zimemoka kutokana na maji ya mafuriko kabla ya mimi kupata hifadhi kwa rafiki yangu siku tatu tangu tukio kutokea”. Alisema Changi.
Alieleza kwa sasa familia yake ipo mkoani Dodoma katika kijiji cha Mlali wilaya ya Kongwa huku akiuelezea mkasa huo wa kutumbukia katika shimo na kutegua kifundo cha mguu na kufanya kazi ya kuokoa watoto ifanywe na majirani zake baada ya yeye kuumia.
“Ilikuwa siku ya kila mtu aliyevamiwa na mafuriko yale jambo la kwanza ni kuangalia namna ya kuokoa watoto kisha thamani ya mali iliyopo ndani ya nyumba yake na ndiyo kitu kilichonitokea mimi baada ya kuanguka chini na kutegua mguu hakuna aliyenijali zaidi ya kunipita nikihangaika na niliposimama sikuweza kuendelea na adhima yangu ya kusomba watoto kupeleka nchi kavu”. Alisema Changi.
Aliendelea kueleza kuwa aliteguka mguu wa kulia wakati yupo katika harakati za kukoa maisha ya familia kwa wale wakubwa kuwahimiza kutoka ndani ya nyumba na watoto wadogo waliokuwa wakihitaji msaada wa haraka kuepukana na maji yaliyokuwa yakiingia kwa kasi ndani jambo ambalo walifanikiwa kupata akili ya haraka na kupanda juu ya meza na kusimama juu yake lakini na wale majirani walifanikiwa kuwatoa eneo hilo na kuwafikisha nchi kavu.
“Nilichoshuhudia kingine na bado kinaniuma roho ni kuona vijana wakikata kuku wangu na kutoweka nao huku mahindi magunia mawili, mpunga debe mbili na pesa sh220,000 za maandalizi ya shamba kwa ajili ya msimu wa kilimo vikipotea katika maji hayo”. Alisema Mzee huyo.
Alisema pesa alihifadhi katika pochi na kuhifadhi katika sanduku lakini pengine katika harakati vijana waliokuwa wakiranda kila nyumba ana wasiwasi walikiona kikielea na kukichukua kwani maji yalikuwa na nguvu sana na kutokana na nguvu hiyo ilisababisha kudhoofisha matofali yaliyoshikilia msingi wa nyumba nyingi na kupelekea kubomoka.
Fatuma Mbonde (60) anasema mafuriko hayo yamemtia umasikini kubwa hasa baada ya nyumba yake aliyokuwa akiitegemea na aliyojengwa kwa shida kubomoka nusu huku upande uliobomoka ukishikiliwa na sehemu ya mbao mbili zilizosimikwa ardhini na kushika paa zilizoezekwa bati ya nyumba hiyo.
Bi Mbonde anasema umasikini alionao kwa sasa ni ule wa kuhangaika na malazi ya watoto yatima sita alioachiwa na watoto wake kufariki dunia akiwemo Ally Rajabu (17), Shabaan anayesoma kidato cha pili sekondari ya kata Magole, Mfaume Kitemo (16), Shani Magari (8) anayesoma darasa la pili shule ya msingi Magole, Shaff Iddi (18) na Hussein Iddi anayesoma shule ya Muungano.
“Mvua ilinyesha kuanzia saa 8 usiku januari 21 mwaka huu na saa 12 asubuhi ilinyamaza na saa 1 nilipata taarifa kutoka kwa wenzangu kuwa kuna maji yanakuja kwa kasi na majira ya saa 2 maji hayo yalianza kutapakaa kila sehemu na kuingia ndani na hakuna kitu ambacho tulifanikiwa kuokoa, nguo, madaftari, magunia 10 ya mahindi, magodoro matatu, mpunga gunia nne, kuku watatu, bata 10 na vifaranga vyao 12 pamoja na vyombo vya ndani vingi vimepotea katika mafutiko hayo”. Alisema Bi Mbonde.
Baada ya nyumba kujaa maji na kuanza kubomoka, Mbonde alisema kuwa hakuwa na sehemu nyingine ya kulala zaidi ya kulala siku mbili kando ya barabara jirani na nyumba yake akilinda usalama wa mabati ya nyumba yake yasije kuibwa na vijana kufuatia sehemu kubwa ya kuku, bata na magodoro kupotea kwa kuibwa hivyo jambo pekee la kuokoa bati ni kulala jirani na nyumba hiyo.
“Wale vijana kwa haraka haraka niliona kama wanasaidia kuokoa mali katika mafuriko yale lakini wakiopoa kitu cha maana walikuwa wanatokea nacho mbali na mhusika, sasa hebu fikiria wenyewe walikuwa wanaogelea kwenye maji na mwenzangu na mimi nipo nchi kavu kwani walichokuwa wanafanya wakikamata kuku wanasogea nao mbali na kadhalika magodoro nayo hivyo hivyo”. Alisema kuwa watu wengi wamepoteza mali nyingi kwa mfumo huo.
Fatuma anasema shida iliyojitokeza katika kulala eneo la nje kando ya barabara ni kupata shida wakati wa kulala kutokana na eneo hilo kujaa kokoto, baridi kali na kung’atwa na mbu kwani kama ulibahatika kuwa na khanga mbili ndizo hizo hizo zilikuwa zinatumika kujifunika lakini hazikusaidi kuondokana na adhabu hiyo ya mafuriko kwani hakuna wa kumlaumu ni mipango ya mwenyezi mungu.
Kwa upande wa wafanyabiashara wakubwa wa vipuli vya pikipiki, Gasper Lyimo anaeleza hasara aliyopata katika mafuriko hayo kuwa ni kupoteza mali yenye thamani zaidi ya sh75 milioni kwa vipuli kuharibika na maji ya mafuriko huku bidhaa zinyingine zikiwa hazifai kwa mauzo.
Lyimo anasema siku ya tukio yeye aliondoka majira ya saa 12 kasoro na kuelekea mji mdogo wa Dumila ambako nako kuna duka ndogo la vipuli vya pikipiki na alifanikiwa kupita eneo la daraja la mto Magole huku likiwa na dalili za nyufa kuonyesha ishara ya kingo za daraja hilo kubomoka na kumpa ishara ya kwenda haraka na kurudi aktumia usafiri wa pikipiki.
“Nilipita daraja la mto Magole majira ya saa 12 hivi wakati nikienda Dumila na niliona dalili za kingo za daraja kutoa ishara ya kubomoka na maji yakipita kwa kasi mtoni tena kwa uwingi ikisomba kila aina ya uchafu na nilienda na kupita salama na wakati nafika Magole nilianza kuwajulisha wenzangu juu ya maji kuelekea kijijini kwetu kwa kasi”. Alisema Lyimo.
Aliendelea kwa kusema kuwa safari ya kwenda Dumila na kurudi Magole aligundua mengi juu ya mafuriko hayo na moja ya sababu ya kijiji cha Magole kukumbwa na mafuriko ni kuziba kwa makaravati yote ya eneo la feri yaliyochangia maji kushindwa kupita kwa kiwango kilichohitajika katika makaravati hayo na badala yake yalisaka mwelekeo na kupata mwaya wa kufuata kingo za barabara inayojengwa na wachina na kuvamia makazi yao.
Kampuni ya ujenzi ya wachina ya china Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) ndiyo iliyochukua kandalasi ya kutengeza barabara kwa kiwango cha lami kutoka eneo la barabara kuu ya Dodoma hadi Turiani kujenga tuta linalodaiwa kuwa chanzo cha maji kushindwa kuondokana kutokana na tuta hilo na maji kutuwama kwa masaa kadhaa kabla ya uamuzi wa kubomoa barabara na kuwa ahueni kwa wananchi waliokwama juu ya mapaa, miti na dali za nyumba kujiokoa katika siku ya tukio.
Kuna zaidi ya wafanyabiashara 25 wenye maduka makubwa mali zao vikiwemo vipuli, bidhaa kuharibika na maji ya mafuriko hayo yakiwa yale ya vifaa vya umeme, baiskeli, pikipiki, maduka ya dawa baridi za binadamu, mashine za kusaga nafaka na vinywaji mbalimbali.
Lyimo anasema kuwa waathirika wa mafuriko hayo wengi wameibiwa mali na vibaka waliokuwa wanajidai wanasaidia kuokoa lakini badala yake hawakutekeleza adhima ya uokoaji na badala yake kugeuka sehemu ya kuwaongezea machungua waathirika wa mafuriko hayo na kutokemea na mali kwani hawakuwa na huruma na wenzao.
“Baada ya kutoa taarifa kwa ndugu, jamaa na mafariki juu ya ujio wa maji ya mafuriko nilirejea dukani kwangu na kwa sababu maji yalikuwa bado hayajafika nilimsaidia rafiki yangu kuhamisha mali na kuhifadhi nyumba ya mama yake ambayo baadaye maji hayo yalivamiwa nyumbani kwa mama yake na uhamishaji wetu mali katika duka lake ikawa kazi ya bure tena haukusaidia kitu”. Alisema mfanyabiashara huyo.
Anasema aliridi dukani kwake na kukuta hali ni mbaya duka limejaa maji na hakuwa na namna tena ya kuokoa chochote zaidi ya kufunga mlango na dirisha na kukaa kando ya barabara na kuangalia tu maji hayo ambayo yalikuwa yanakaribia kuvuka kingo ya barabara kijijini hapo na kwenda ng’ambo ya pili.
Sehemu kubwa ya mafuriko hayo yalikuwa na kimo cha urefu wa futi nane hadi 10 kutokana na maeneo jambo hilo ndilo lililopelekea nyumba nyingi kubomoka kutokana na maji kukaa kwa muda mrefu na yalikuwa na acid kali iliyopelekea salafu za sh50, sh100 na sh200 kubadilika rangi na hilo limeshuhudiwa na mfanyabiashara huyo kwa kiasi cha pesa za salafu zenye thamani ya sh100,000 kuathirika na acid hiyo.
Anataja sababu nyingine kuwa kama maji ya mafuriko hayo yasingebomoa kingo za daraja la mto Magole na kubomoa barabara eneo la mahakama basi mafuriko hayo yangekuwa na maafa makubwa sana kwani kama kingo za udondo zingekuwa imara maji hayo yangeikia kwa kasi kijiji hapo tofauti na kasi iliyojitokea na kuleta madhala yaliyojitokeza.
“Kukaa kwangu eneo la duka kuliwapa mwaya vibaka kusomba kila kitu cha thamani ndani ya nyumba yangu ninakoishi kwani familia ilikuwa haina uwezo wa kukabiliana na maji yale na kutoa furusa kwa vijana wasioa waaminifu kufanya uhalifu, nimepoteza hasara ya bidhaa dunikani lakini na nyumbani nako nikakuta hasara nyingine”. Alisema Lyimo.
Aziz Fagie ambaye ni mjumbe wa kamati ya mafuriko kijiji cha Magole anasema kuwa kwa upande wao wamekuwa wakilalamikiwa na tatizo la mgao wa chakula waathirika kukaa kutwa mzima wengine wakipata na hata kukosa mgao huo.
“Tatizo lililojitokeza hasa kwetu wanakamati ya mafuriki ni kulalamikiwa juu ya baadhi ya wananchi kukosa mgao kwa siku husika huku wengine wakipata na wengine kusubiri mpaka siku inayofuata kutokana na foleni”. Alisema Fagie.
Fagie alisema kuwa tayari suala hilo amelifikisha kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro aweze kuangalia namna ya kupunguza foleni ya ugawaji wa chakula na kuweka utaratibu wa kugawa vitongoji vilivyokumbwa na mafuriko hayo kwa kugawanya makundi mawili mawili ili kurahisisha ugawaji wa chakula hivyo na kuondoa minung’uniko.
“Vitongoji vilivyoaathirika kwa wananchi wake kukumbwa na mafuriko hayo vipo sita hivyo kama serikali ya wilaya ikigawa vitongoji viwili viwili na kuna na makundi matatu ya ugawaji wa chakula itakuwa jambpo jemba na foleni itapungua tofauti na hivi sasa vitongoji vyote vinachukua chakula kwa kusomwa majina na mtu mmoja na kundi la watu ni kubwa”. Alisema Fagie.
Vitongoji hivyo ni Bwawani, Zizini, Gengeni, Manyata, Mjimkuu na Kichangani ambako kwa tathimini ya awali ni waathirika.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera hali ya waathirika hao alisema kuwa kwa sasa asilimia kubwa serikali imejitahidi kurejesha hali ya utulivu kwa maana ya huduma muhimu za kijamii zimetengemaa ikiwemo maji safi, vyoo na mahema ya kulala waathirika hao katika kambi ya kijiji cha Magole na kijiji cha Mbigili kitongoji cha Mateteni.
Bendera alisema kuwa kazi ilipo mbele yao ni namna ya kugawa chakula cha kutoka kwa kila kaya ikiwezekana kupatika chakula cha kuanzia cha kuanzia wiki tatu hadi mwezi mmoja ili wale wenye mashamba waendelee na shughuli za kilimo.
“Katika suala kama hili huwezi kukosa malalamika kwa wananchi na pengine lawama kabisa lakini cha msingi ni namna gani unaweza kuwahudumia watu katika jambo unaloliona lipo sahihi na mambo mengine ndiyo yanafuata”. Alisema Bendera ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa.
Kuhusu tathimini ya waathirika hao bendera alisema kuwa awali palikuwa na tathimini iliyokuwa na mapungufu na mapungufu hayo aliyaona na yalikuwa yanafanyiwa kazi katikati na ujio wa rais Jakaya Kikwete kuingia ambapo aliagiza kufanyika tathimini upya ya kuhakiki majina, jinsia na nyumba zilizoboka kabisa na zile ambazo hazijaathirika kwa maana ya kuingia maji na kutoka.
Tathimini hiyo ndiyo itatoa majibu sahihi na ukweli kwani ilishirikia watu wanne katika kundi ikiwa na mjumbe mmoja wa kamati ya mafuriko, askari jeshi, mjumbe wa nyumba 10, Mwenyekiti wa Kitongoji na askari polisi juu ya wananchi waliokumbwa na mafuriko hayo katika tarafa ya Magole ikihusisha vijiji vya Mbigili (kitongoji cha Mateteni), Magole, Berega na Wami Dakawa. CHANZO MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment