Mshambuliaji wa Simba, Haruna Chanongo (jezi nyekundu) akizuiwa na
wachezaji wa Mbeya City, Peter Mapunda (kushoto) na Paul Nonga (wapili
kushoto), katika mchezo wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya. Timu
hizo zilitoka sare 1-1. Picha na Michael Matemanga.
MBEYA City wamepoteza nafasi ya kukalia usukani wa Ligi Kuu baada ya kulazimishwa sare 1-1 na Simba jana kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mbeya City walikuwa wa kwanza kupata bao
lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na nahodha Deogratius Julius, kabla
ya Mrundi, Amis Tambwe kuisawazishia Simba dakika ya 50, likiwa ni bao
lake 15 msimu huu katika Ligi Kuu.
Kwa matokeo hayo, Mbeya City imefikish pointi 35,
sawa na Yanga (35), Simba imebaki nafasi ya nne wakiwa na pointi 32,
huku Azam wakiendelea kuongoza kwa pointi 36.
Kocha wa Simba, Zdavko Logarusic alimwanzisha kipa
Yaw Berko badala ya Ivo Mapunda pamoja na viungo Henry Joseph na
William Lucias wakicheza katika nafasi za beki wa pembeni.
Simba walianza mchezo huo kwa kasi ambapo katika
dakika ya 6, Ramadhani Singano alikosa bao akishindwa kumalizia krosi
ya Haruna Chanongo.
Wenyeji Mbeya City walipata penalti dakika ya 12
baada ya beki Joseph Owino kushika mpira uliopigwa na Deus Kaseke na
mwamuzi Mathew Akrama.
Nahodha wa City, Julius aliwainua mashabiki wao kwa kufunga mkwaju huo wa penalti kwa kumwacha kipa Berko asijue la kufanya.
Baada ya bao hilo Simba walirudi uwanjani na
kutawala sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini mashuti ya Singano, Tambwe
na Chanongo yaliokolewa na kipa wa City, David Burhan.
Benchi la ufundi la Simba, likiongozwa na Kocha wa
Logarusic, Seleman Matola, Idd Pazi na Nico Nyagawa walimvamia mwamuzi
Akrana baada ya mapumziko wakipinga penalti aliyowapa City.
Simba walisawazisha bao hilo dakika ya 50, kupitia
Tambwe aliyepokea pasi nzuri ya Chanongo ndani ya eneo la hatari na
kupiga shuti la juu na kumwacha kipa David Burhani asijue la kufanya.
Awali mashabiki wengi waliruka ukuta kuingia uwanjani katika jukwaa lililokaliwa na mashabiki wa Mbeya City.
Pia, wachezaji wa Simba walizuiwa kuingia uwanjani
kwa muda kutokana na vurugu za mashabiki zilizotokea kwenye mlango wa
kuingia uwanjani hadi polisi walipoingilia kati na kutuliza hali hiyo. MWANANCHI.

0 comments:
Post a Comment