WABUNGE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUTOJADILI HOTUBA YA RAIS NA JAJI WARIOBA DODOMA.
Na Magreth Kinabo – Maelezo, Dodoma.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum Katiba ,Mhe .Samwel Sitta amesema Bunge halitajadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete na ile ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kama alivyokuwa ametangaza awali kwa kuwa kufanya hivyo kutaingilia mchakato wa mjadala wa Rasimu ya Katiba Mpya.Mhe. Sitta ametangaza uamuzi huo leo mapema asubuhi katika kikao cha bunge hilo mjini Dodoma , ambapo alisema kazi ya msingi ya bunge hilo ni kujadili rasimu hiyo,na baada ya kushauriana na makundi mbalimbali Mwenyekiti alidai kuendelea kujadili hotuba ya Mwenyekiti wa Tume pamoja na ile ya Rais ni kuwahisha shughuli za kujadili Rasimu ya katiba wakati tayari kanuni zimeweka msingi wa namna ya kujadili ikiwa ni pamoja na kujadili sura mbili kwa siku.(P.T)
Akizungumzia kuhusu suala hilo mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo, Yusuf Manyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU)alisema anaunga mkono uamuzi huo na kwamba kazi iliyowaleta katika Bunge hilo ni kuchambua rasimu hiyo na si hotuba hizo.
Kwa upande wake mjumbe mwingine wa Bunge hilo Natunjwa Mvungi alisema uamuzi huo uko sahihi kwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo amefuata kanuni ambazo kimsingi zimeweka utaratibu wa kujadili Rasimu ya Katiba.
Naye Paul Makonda ambaye pia ni mjumbe wa Bunge hilo amesema hotuba ya Rais Kikwete haina cha kujadili kwa kuwa ilitoa maelekezo na majukumu ya kazi ya Bunge hilo na kuwataka kuisoma rasimu hiyo kwa umakini.
Awali kabla ya kuahirisha Bunge na kuipa nafasi kamati ya Kanuni ya Bunge Maalum kumalizia kazi yake ya kuandaa mapendekezo mbalimbali katika mabadiliko ya Kanuni Mhe. Sitta aliwaapisha wajumbe watatu wa Bunge hilo, ambao ni Suzan Lyimo, Devota Likokola na Mwanamrisho Juma Ahmed.
0 comments:
Post a Comment