DAR ES SALAAM.
Wakati Ikulu ikitangaza kwamba Rais Jakaya Kikwete amevunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tume hiyo imetoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo ya Rasimu ya Katiba.
Wakati Ikulu ikitangaza kwamba Rais Jakaya Kikwete amevunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tume hiyo imetoa ufafanuzi wa baadhi ya maeneo ya Rasimu ya Katiba.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilieleza kuwa
Tume ya Jaji Joseph Warioba ilivunjwa tangu Machi 19, ikiwa ni siku moja
baada ya kuwasilisha Rasimu ya Katiba bungeni mjini Dodoma.
Wakati taarifa ya Tume ya Warioba ilitolewa jana
jioni, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilikuwa imeshatoa taarifa
ya kuvunja tume hiyo mapema jana ikieleza kuwa shughuli za tume hiyo
zilikoma tangu Jumatano iliyopita.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano alivunja rasmi Tume ya
Mabadiliko ya Katiba tarehe 19 Machi, 2014 kwa Tangazo la Serikali
Na.81 la tarehe 21 Machi, 2014,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Hata hivyo, Jaji Warioba aliliambia gazeti hili
jana kuwa hadi wanakutana juzi kwenye kikao cha mwisho cha tathmini
walikuwa hawajapokea barua ya kuvunjwa kwa tume yake.
“Barua ya Ikulu tumeipokea leo. Tulikuwa hatuna
taarifa kwamba tume yetu imevunjwa hadi tulipopokea barua leo (jana).
Tulifanya kikao chetu cha mwisho cha tathmini jana (juzi),” alisema
Warioba alipozungumza na Mwananchi jana jioni.
Warioba pia alithibitisha kwamba taarifa ya ufafanuzi (imechapishwa ukurasa wa 37) ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Taarifa hiyo ya Tume ya Warioba imetaja baadhi ya
sababu za kupendekezwa kwa muundo wa serikali tatu kuwa, ni pamoja na
Serikali ya Muungano kutokuwa tena na nguvu upande wa Zanzibar na Rais
kupokwa baadhi ya madaraka aliyopewa kikatiba.
Ufafanuzi wa Tume
Taarifa hiyo ya tume ilisema: “Waasisi walituachia
mambo 21 (ukiacha usajili wa vyama) kwenye orodha ya Muungano. Katika
kipindi cha miaka ishirini iliyopita yamepunguzwa. Mambo yote yaliwekwa
kwa utaratibu uliowekwa na Katiba lakini yameondolewa kinyume na
Katiba.”
Iliongeza: “Sehemu zote mbili ziliamua kuachia
baadhi ya mambo yake kuwa chini ya Serikali ya Muungano, sasa sehemu
moja inaondoa mambo yake. Kwa hiyo Serikali ya Muungano itakuwa
inashughulikia zaidi mambo ya upande mmoja.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment