WABUNGE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA WAJUTIA POSHO DODOMA
BAADHI ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanajutia posho wanayoendelea kupata wakati bunge likivurugika mara kwa mara na kusababisha kuahirishwa, hivyo kuzua wasiwasi wa kutotekelezwa malengo yaliyowapeleka.
Makundi yenye uwakilishi ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, katika kujiengua na shutuma yamenyooshea wanasiasa vidole na kusema wanavuruga mwenendo wa Bunge hilo kwa maslahi ya vyama vyao.
Pamoja na madai hayo, makundi hayo yamepinga uwapo wa makundi yasiyo rasmi ndani ya Bunge hilo kama vile Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na Umoja unaounda kundi la Tanzania Kwanza na kushauri yapigwe marufuku.
“Sisi tunaotoka nje ya makundi ya siasa tusiposimama imara, mchakato huu utakuwa ni wa kisiasa zaidi na hakuna kitakachofanyika zaidi ya kula fedha za wananchi masikini wa Tanzania,” ulisema Umoja wa Watumiaji wa Ardhi, Dk Masele Maziku. Umoja huo wa watumiaji wa ardhi unajumuisha wafugaji, wavuvi na wakulima ndani ya Bunge Maalumu.
Aidha umoja huo ulilaani kile kilichodaiwa ni mkakati unaofanywa na makundi ya wanasiasa kuhujumu mwenendo wa bunge hilo. Dk Maziku alisema jana kuwa umoja huo umegundua kwamba makundi ya siasa yanaendekeza itikadi zao za kisiasa katika mchakato huo, hatua ambayo itafanya kupatikana Katiba isiyo na maslahi kwa Watanzania.
Alisema katika hali ya kushangaza wanasiasa wamekuwa wakijadiliana na kufikia maridhiano kwa mambo mbalimbali na hivyo kuonesha ukomavu wa kisiasa na nia njema ya upatikanaji wa Katiba ya Watanzania, lakini baadaye hugeukana na kufanya mchakato kuanza upya, jambo ambalo haliwezi kuendelea kuvumilika. “Tamko letu ni kwamba tumechoshwa na kuwa na Bunge lenye kulemewa na makundi ya siasa.
“Wanasiasa watambue kuwa hatukuja hapa kwa ajili ya mabishano ya kuoneshana umwamba, bali tumekuja kufanya kazi tuliyotumwa na Watanzania ya kuhakikisha Katiba mpya yenye uwakilishi wa maslahi mapana ya wananchi inapatikana,” alisema. Wamemwomba Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuliongoza kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na si vyama vya siasa kwa vile makundi ya Bunge hilo yanawakilisha maslahi ya wananchi.
Vikundi visilelewe Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Peter Mziray alisema baraza limeangalia na kufuatilia kwa makini mchakato mzima na mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba.
Limebaini wanasiasa ambao ni wadau wakubwa, wanaweza kukwamisha mchakato kwa malumbano yasiyo na tija na matendo yasiyokubalika.
“Wanasiasa ndio wanaolalamikiwa sana katika mchakato mzima ndani ya Bunge Maalumu la Katiba. Matendo hayo ndio yatakayofanikisha au kukwamisha mchakato mzima wa Bunge hili la Katiba kutengeneza katiba mpya ya nchi yetu,” alisema Mziray.
Alisema Kamati ya Uongozi ya Baraza hilo imebaini uwepo wa makundi yasiyo rasmi ndani ya bunge hilo na kwa bahati mbaya inaonekana bunge limetambua makundi hayo kuwa rasmi.
“Kamati inaona kuwa uwepo wa makundi haya na kutambuliwa kwake na bunge kunachochea mgawanyiko na kujenga uhasama baina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kudhoofisha dhana ya kufanya kazi pamoja na kufikia maridhiano kwa masuala ambayo wajumbe wanatofautiana kimtazamo.
Alisema Kamati ya Uongozi ya Baraza inatoa mwito kwa wajumbe wote wa bunge hili kuacha kujihusisha na makundi haya na badala yake wachambue na kuunga mkono hoja kwa uzito wa hoja na kwa kuzingatia masilahi ya taifa badala ya kuzingatia mtazamo au msimamo wa kundi fulani,” alisema.
Wajutia posho Mjumbe Stella Manyanya ametaka wajumbe wenzake kuweka maslahi ya taifa mbele badala ya kulumbana.
Alisema malumbano yanachangia bunge kuahirishwa mara kwa mara wakati wao wakiendelea kulipwa posho huku Watanzania wakikosa huduma muhimu.
Manyanya ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alisema hayo jana wakati wa mahojiano na gazeti hili. Alisema fedha nyingi zimekuwa zikiteketea kulipa posho wajumbe.
Alisema kama kunakuwa na mkanganyiko wa kutoelewana hasa upande wa kanuni, ni vyema wanaohusika wakatoka nje kujadiliana wakiacha vikao vikiendelea badala ya kuviahirisha.
"Wanaoahirisha bunge kila wakati huku watu wengi wakifa kutokana na kukosa huduma muhimu, nikiwa kama binadamu wa kawaida napenda fedha lakini sipendi fedha ya dhuluma kama hii," alisema.
Alishauri wajumbe kuweka utaifa mbele. Manyanya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, alitaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta kuwa na subira kwa kuwa ndani ya bunge yamo makundi ya watu mbalimbali.
Uchu wa madaraka Mjumbe Hamad Rashid Mohammed ambaye ni Mbunge wa Wawi (CUF) alisema suala la muundo wa muungano limekuwa likizungumziwa zaidi na wanaohitaji madaraka.
Alishutumu kitendo cha kuacha kuzungumzia masuala ya msingi juu ya namna ya wananchi kuondokana na umasikini. Alisema muhimu kuweka mbele maslahi ya walio wengi na si kujadili mambo yanayoonesha wazi watu wanataka madaraka kutokana na kile wanachokuwa wanakipendekeza.
Wanaharakati wakerwa Mkufunzi wa Mafunzo ya Jinsia kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Dorothy Mbilinyi amekosoa akisema wajumbe wanatakiwa kuwa na mjadala mpana zaidi katika mada zinazogusa wananchi.
Alisema kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba kutumia muda mwingi kutengeneza kanuni na kulumbana kuhusu muundo wa muungano, kimekera wanaharakati .
Alisema hayo jana mjini Dodoma katika mahojiano kwenye mafunzo ya jinsia, demokrasia na katiba yanayoshirikisha washiriki kutoka mikoa ya kanda ya kati ya Tabora, Singida,Tabora na Dodoma.
Alisema majadiliano ndani ya bunge yaliyotokana na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete na ya Jaji Joseph Warioba juu ya muundo wa muungano, hayana tija ikizingatiwa mahitaji ya watanzania katika katiba hiyo.
"Inasikitisha kuona bunge hilo linaloendelea linazungumzia habari za ibara moja ya muungano wakati kuna mambo muhimu kama vile ya kijinsia na demokrasia,” alisema.
Ukawa yashauriwa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) limeeleza kusikitishwa na mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba. Limetaka wajumbe wanachama wa Umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa) kutafuta maridhiano yenye nia ya kuipata katiba mpya bila kuburuzwa.
Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratias Munishi alisema jana Dar es Salaam mwenendo wa sasa wa Bunge maalumu unawachukiza wananchi wengi.
Alidai inaonesha mpango wa CCM kuhakikisha wanaliteka bunge hilo kwa lengo la kurahisisha mawazo ya chama hicho kutawala kwenye katiba hiyo mpya.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment