SERIKALI imekanusha taarifa zilizoandikwa katika baadhi ya magazeti ya jana yakiwemo gazeti la Uhuru na Tanzania Daima. Habari hizo ni ile ya gazeti la Uhuru inayosomeka: “Bila kupitia JKT hakuna ajira serikalini” na iliyoandikwa na Mtanzania Daima yenye kichwa cha habari “Ikulu:Rushwa ya ngono imekithiri serikalini”
Kwa mujibu wa Idara ya Maelezo, Magazeti yote haya yameandika habari za kupotosha Umma kuhusu hotuba ya Katibu Mkuu Kiongozi aliyoitoa Juni 26,2014 katika mkutano wa Mwaka wa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Makatibu Tawala uliofanyika mjini Dodoma.
Taarifa hiyo imefafanua kwamba Magazeti hayo yamejenga taswira kwamba Katibu Mkuu Kiongozi alitoa taarifa kwamba “Hakuna ajira bila kupitia Jeshi la Kujenga Taifa” na “Rushwa ya ngono imekithiri Serikalini”.
Kutokana na upotoshaji huo, Serikali inapenda kutoa ufafanuzi kwamba taarifa hizo siyo za kweli wala hazielezi taarifa halisi aliyoigusia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Taarifa ilisema kwamba katika hotuba yake alisema:
“Aidha, ningependa mjue kuwa kuanzia sasa tutaweka mkazo mkubwa sana kwenye sifa ya uzalendo kwenye ajira Serikalini. Hatuwezi kuwa na Watumishi wa Umma ambao hawana uzalendo.
“Pale ambapo waombaji kazi kwenye Utumishi wa Umma wana sifa zote sawa, lakini wakawepo wale ambao wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa watapewa kipaumbele. Lakini narudia, kipaumbele hicho kitumike pale tu ambapo sifa zingine zote ziko sawa, na si vinginevyo”.
Kuhusu suala la rushwa ya ngono lililoripotiwa na gazeti la Tanzania Daima, taarifa hiyo imesema si kweli kwamba Katibu Mkuu Kiongozi alisema kumekuwa na ongezeko au kukithiri kwa rushwa ya ngono katika utoaji wa ajira serikalini. Taarifa ilisema kwamba, alichokisema Katibu mkuu kiongozi ni kwamba:
“Lakini bado malalamiko yanasikika kuwa ati huwezi kuajiriwa kwenye Utumishi wa Umma isipokuwa kama unajulikana au unatoa rushwa, ama ya fedha au ya ngono. Jambo hilo linanisononesha sana. Mimi naamini mambo hayo yamepungua sana.
“Lakini kama yanafanyika, ni kinyume kabisa na Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma na lazima tulio katika ukumbi huu tuyapige vita kwa bidii zote, bila kuoneana haya, hadi wananchi waone kuwa kweli hayapo.
“Tusipuuze hata kidogo malalamiko ya wananchi, bali tujichunguze na tuchunguzane, ili kama mambo hayo bado yapo, kwa pamoja tuazimie kuyakomesha kabisa kwenye Utumishi wa Umma”.
Aidha taarifa hiyo imetaka wananchi kusoma hotuba halisi ya Katibu Mkuu Kiongozi kwenye tovuti ya “http://www.chiefsecretary.go.tz” www.chiefsecretary.go.tz kuona makosa yaliyofanywa na vyombo hivyo vya habari wao wenyewe.HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / IKULU YAKANUSHA HABARI YA "BILA KUPITIA JKT HAKUNA AJIRA SERIKALINI" NA ILE YA "IKULU:RUSHWA YA NGONO IMEKITHIRI SERIKALINI".
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment