Spika wa Bunge, Anne Makinda amemzuia Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) kuendeleza sakata la tishio la kukatwa kichwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema.
Makinda, amefikia hatua hiyo jana baada ya Kafulila, kuomba mwongozo wa Spika kuhusu hatma ya shutuma za ufisadi unaoihusu kampuni ya Escrow, kufuatia hatua yake (Kafulila) na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuwasilisha ushahidi wao bungeni.
Wakati akiomba mwongozo huo, Kafulila alikumbushia namna alivyonusurika kutwangwa makonde na Werema, kisha tisho la Mwanasheria Mkuu huyo kutaka kuondoka na kichwa chake, ikiwa Kafulila hatamuomba radhi.
Pia, Kafulila alitumia fursa hiyo kuujulisha umma hususan wapiga kura wake, kwamba ikiwa jambo baya lolote litamtokea, mshukiwa wa kwanza anapaswa kuwa Werema.
Tayari Kafulila amewasilisha malalamiko yake kwa Spika Makinda na nakala zake kusambazwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu na Werema mwenyewe.
Pia amewasilisha nakala hiyo kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Hata hivyo, kabla ya kutoa mwongozo, Makinda, alimlaumu Kafulila kwa kuwasilisha barua hiyo kwake, kisha taarifa zake kuchapishwa na kutangazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari jana.
Kuhusu hatma ya ushahidi wake (Kafulila) na Mnyika, Makinda alisema vielelezo hivyo vimefikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Makinda akatoa rai kwa wengine wenye vielelezo kama hivyo kuviwasilisha Takukuru na kwamba mjadala huo haupaswi kuendelezwa bungeni.
Kuhusu vitisho vya Werema kwa Kafulila, Makinda alisema Mbunge huyo wa Kigoma Kusini ndiye aliyeanza ‘kumchokoza’ Werema na Mwanasheria Mkuu ‘akachokozeka’.
“Kafulila wewe uli-mprovoke (ulimkasirisha) na mwenzako ‘akaprovokika’, hivyo kila mtu alikuwa na jazba zake,” alisema.
Makinda, alisema kwa vile ofisi yake imeshapokea barua ya Kafulila kuhusu suala hilo, anapaswa kuwa na subira kwa vile lipo mahali panapohusika, kisha akahoji, “sasa unataka majibu yatolewe hapa bungeni, kama una vielelezo zaidi peleka panapohusika.”
Jumatano iliyopita, Werema alitaka kumfuata Kafulila kwa kile kilichoaminika kutaka kumpiga, lakini akazuiwa na baadhi ya wabunge.
Habari zaidi zilieleza kuwa, juzi, Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azzan Zungu, alitaka kuwapatanisha lakini hakufanikiwa baada ya pande zote kutokubaliana.
Mzozo kati ya wawili hao ulianza baada ya Kafulila, kutaka ufafanuzi kuhusu Sh. bilioni 200 ‘zilizochotwa’ katika akaunti ya Escrow zikihusishwa na njama za kifisadi.
Habari hii imeandikwa na Isaac Kijoti, Dodoma na Mashaka Mgeta, Dar es Salaam. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment