Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli
Alikuwa akizungumza jana na wananchi wa wilaya ya Chato kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya stendi ya mabasi, huku akisema CCM kitaendelea kutawala milele kwa kuwa kina mizizi ya kutosha.
“Ndugu zangu wananchi, niwahakikishieni kuwa CCM kitaendelea kutawala milele... hatuwezi kushindwa wakati wakuu wa wilaya ni wa CCM, wakurugenzi wote ni CCM, madiwani wengi nchini ni CCM, wenyeviti wa vijiji wengi ni CCM, wenyeviti wa vitongoji wengi ni CCM... wote hao mpaka kuja kuwaondoa madarakani siyo kazi rahisi,” alisema Magufuli.
“Wapinzani hata kama watageuza majina vipi haitawasaidia. Hata wajiite Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) watabaki wasindikizaji tu,” alisema na kuongeza:
“Na niwahakikishie jimbo hili (Chato) sitakubali lichukuliwe na wapinzani wakati wilaya nimeileta mimi, umeme nimeleta, barabara ya lami nayo nimeileta mpaka na Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema) alikuja hapa na magari yake, akapita kwenye barabara yangu.”
Mpaka mwaka 1995, Tanzania ilikuwa na wabunge wanaotoka chama kimoja cha CCM pekee.Hata hivyo, tofauti na tambo za Dk. Magufuli, kuanzia uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ulioruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, CCM ilipata wabunge 186, CUF 24, NCCR-Mageuzi 16, Chadema watatu, UDP watatu na TLP mmoja.
Mwaka 2000, CCM walipata wabunge 202, CUF 17, NCCR-Mageuzi mmoja, Chadema wanne, UDP watatu na TLP wanne.Mwaka 2005, CCM walipata wabunge 208, CUF 19, NCCR-Mageuzi hawakupata mbunge hata mmoja, Chadema wanne, UDP mmoja na TLP mmoja.
Mwaka 2010, CCM ilipata wabunge 262, Chadema 49, CUF 35, NCCR-Mageuzi watano, TLP mmoja na UDP mmoja.Waziri Magufuli aliendelea kusema kuwa wananchi wengi wa Wilaya ya Chato awali walikuwa hawajui hata inavyofanana transifoma ya kufua umeme, wala mabasi ya kutoka Dar es Salaam ambayo hupita hapo kuelekea Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.
“Bila mimi kujipendelea kutengeneza barabara hiyo mngeyaona wapi mabasi ya kutoka Dar kwenda Bukoba...uliona wapi nani akashindwa kujipendelea...ukweli lami nilipindisha...na ninajua waandishi wa Chato kesho wataandika Magufuli akiri kupindisha barabara...mkitaka andikeni na nyie mpindie huku huko,” alisema.
Pamoja na Mambo mengine, kauli hiyo ya Dk. Magufuli ilisababisha baadhi ya wananchi kuguna huku wakidai ni sawa na kuwakashifu.
Kadhalika, alitumia nafasi hiyo kuwaonya baadhi ya wanachama wa CCM ambao wameanza mbio za kulinyemelea jimbo la Chato kwa kile alichodai wanapita kwa wananchi na kuwaeleza kuwa hatagombea tena nafasi hiyo huku akisemna taarifa hizo siyo za kweli.
“Inanishangaza sana baadhi ya watu wameshaanza kupita kwa wananchi wanataka wapewe ubunge wa jimbo la Chato kwa madai eti mimi sigombei tena...ni nani aliyewaeleza kuwa sitogombea ubunge?” alihoji Dk. Magufuli.
Wakati akieleza hayo, Mkuu wa wilaya hiyo, Rodrick Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, Clement Berege, walikuwa wameketi upande wa jukwaa kuu wakimshagilia Dk. Magufuli.
Waziri Magufuli alionekana kushindwa kukata kiu ya wananchi ambao walitaka kujua tatizo la maji safi na salama linatatuliwa lini licha ya Waziri wa Maji kuwaahidi kuwa yangepatikana tangu Oktoba mwaka 2013, pamoja na hatima ya wananchi kutapeliwa zaidi ya Shilingi milioni 34 na Asasi ya utoaji mikopo midogo vijijini ya Vicoba tawi la Chato.
Kauli ya Magufuli kwamba wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ni makada wa CCm inadhihirisha madai ambayo yamekuwa yakitolewa na vyama vya upinzani na makundi mengine ya jamii kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa kukipendelea chama tawala.
Vilevile, kauli yake kwamba alipindisha miradi ya barabara kwenda jimboni kwake inadhihirisha madai ya baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) ambaye aliwahi kuvutana na Waziri huyo mbele ya Rais Jakaya Kikwete akimtuhumu kupeleke mradi wa barabara Chato uliotakiwa kwenda Kigoma. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment