BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA LATOA WITO KWA ISRAEL NA PALESTINA KUSITISHA MAPIGANO UKANDA WA GAZA.

MATUKIO YA KISIASA. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa wito wa kukomeshwa mapigano baina ya Israel na wapalestina katika Ukanda wa Gaza, na kufufuliwa mazungumzo ya amani kutafuta suluhisho litakaloleta amani ya kudumu.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yameendelea licha ya miito ya kimataifa kutaka yakomeshwe

Tangazo hilo lililoungwa mkono na wanachama wote 15 wa baraza hilo limezitaka pande hizo mbili kurejea katika makubaliano ya kusitisha uhasama ya Novemba, 2012 ambayo yalisimamiwa na Misri, ambayo hata hivyo hayaweki muda maalum wa utekelezwaji wake. 


Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Riyad Mansour amesema kulingana na tafsiri yao kuhusu makubaliano hayo, usitishwaji wa mapigano unapaswa kuanza mara moja.

''Tunafuatilia kwa makini iwapo Israel itauheshimu wito huu (wa Baraza la Usalama) na tunatarajia kwamba itafanya hivyo, ikiwa watakwenda kinyume, basi tunazo hatua mbadala, na hatutalipa Baraza la Usalama muda wa kupumua'' Amesema Mansour, na kuongeza kuwa ni jukumu la baraza hilo kushughulikia mchakato wa amani duniani, na kusimamisha ukandamizaji dhidi ya wapalestina.

Raia ndio wanaoumia

Zaidi ya robo tatu ya waliouawa katika mashambulizi hayo ni raia wa kipalestina.

Idadi ya vifo kwa upande wa wapalestina kutokana na mashambulizi ya Israel imepanda na kufika watu 157, na Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya robo tatu ya wahanga ni raia. 


Katika kile kinachoonekana kama kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa kutaka vita vikomeshwe katika Ukanda wa Gaza, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague pia ametoa wito wa kusimamishwa kwa mapigano, na kusema atakutana na wenzake wa Marekani, Ufaransa na Ujerumani mjini Vienna leo Jumapili kuzungumzia suala hilo.

Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa amesema mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa ya kiarabu watakutana Jumatatu, katika kile alichokiita ''juhudi zinazoendelea kukomesha ukandamizaji dhidi ya watu wetu''.

Tangazo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo hata hivyo halina uzito kisheria, ndio tamko la kwanza kutoka baraza hilo lenye nguvu zaidi katika Umoja wa Mataifa, ambalo linakumbwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina.

Marekani bega kwa bega na Israel.

Baraza la Usalama: Marekani inasisitiza Israel inayo haki ya kujilinda

Marekani ambayo ni mshirika mkubwa wa Israel, imeitetea mashambulizi ya Israel kama jibu kwa maroketi yanayorushwa kwenye ardhi yake kutoka Ukanda wa Gaza ambao unadhibitiwa na chama cha Hamas. 



Wanachama wengine wote wa baraza hilo wamepinga mashambulizi ya Israel, ambayo mwakilishi wa Palestina amesema yameuwa watu 1000. Hakuna mtu yeyote aliyekufa kwa upande wa Israel kutokana na mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza.

Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema nchi yake inasimama pamoja na Israel na haki yake ya kujilinda, na kuongeza lakini kwamba hata Marekani inatiwa wasi wasi na kuzidi kuongezeka kwa mvutano, na ingependa juhudi zote zifanyike kuepusha vifo zaidi vya raia.

Tangazo la Umoja wa Mataifa haliyataji bayana mashambulizi ya maroketi yanayofanywa na Hamas, wala mashambulizi ya Israel kama jibu kwa maroketi hayo.DW
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: