CCM YAWACHIMBA MKWARA NZITO MAKADA WALIOONYESHA NIA YA KUGOMBEA URAIS 2015.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye
MAKADA sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopewa onyo Februari mwaka huu wamekalia kuti kavu, baada ya chama hicho kusema kitapitia upya mienendo yao na baadhi yao wanaweza kupoteza sifa za kuwania urais mwakani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema endapo Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho inayotarajiwa kukutana Agosti mwaka huu ikibaini kama makada hao walikiuka mwenendo wa utekelezaji wa adhabu waliyopewa watapoteza sifa.
Pamoja na adhabu nyingine, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mienendo yao ya kisiasa ikifuatiliwa.
Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
Jana Nape alisema Kamati Kuu ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais.
“Baada ya kutafakari kwa kina, kamati kuu inapenda kuwakumbusha kuwa ili wasipoteze nia ya kugombea ni muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo,” alisema Nape.
Alisema kama itabainika makada hao waliopewa adhabu hawakutekeleza masharti ya adhabu zao kama zilivyotolewa na CC, kuna hatari ya kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji wa masharti ya adhabu husika.
“Kila mmoja anafuatiliwa mwenendo wake, kuhusu wale waliopewa adhabu na Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za Chama kwa suala hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya mwenendo wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo.
Kama watakuwa hawajatekeleza adhabu zao kamati itapeleka mapendekezo CC ili waweze kuongezewa adhabu kulingana na ukubwa wa makosa yao na taratibu za chama,” alisema Nape.
Alisema ni muhimu kwa wanachama wote kukumbuka chama ni pamoja na katiba, kanuni na taratibu zake, hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga jambo ambalo halivumiliki.
Alisema nia ya CCM ni kusimamia na kuhakikisha chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu sana, hasa katika kuelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya Kamati Kuu, zinasema aliyetoa hoja kuendelea kufuatiliwa kwa makada hao ni Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula aliyesema amefungua faili kwa ajili ya makada hao.
Alisema suala jingine alilowasilisha Mangula ni ripoti ya ziara yake aliyoifanya katika mikoa ya Tabora na Kigoma.
“Alisema watafuatiliwa na kama itabainika kuwa wamevunja masharti wataongezewa adhabu nyingine ya miezi sita.
“Wakati Mangula akisema hivi, tunajua kuwa kuna mmoja kati ya hao makada waliopewa adhabu wakati wa maadhimisho ya miaka 50 alialika makatibu wa mikoa nyumbani kwake na wengine alikutana nao kwenye hoteli waliyofikia, alikula nao chakula na akawapa posho,” kiliendelea kupasha chanzo chetu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya viongozi walimuita kada huyo kimya kimya na kumuuliza juu ya suala hilo na yeye kuwajibu kuwa hakujua kuwa ni kosa kuwakaribisha viongozi hao wa chama nyumbani kwake.
Kilisema pia kuwa kada mwingine alikutana na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali kwenye Hoteli ya Matilapia jijini Mwanza.
Februari 18, mwaka huu CCM kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa makada wake ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.
Uamuzi huo ulibarikiwa na Kamati Kuu iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Mazungumzo na Ukawa
Nape alisema katika kikao hicho cha Kamati Kuu kilichoketi juzi Julai 16, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, pamoja na mambo mengine kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa upande mmoja na CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa upande wa pili.
Alisema mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi yana lengo la kuangalia kwa kina ni kwanini baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba walisusia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo na kuangalia namna watakavyorudi ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini.
“Kwa ujumla Kamati Kuu ya CCM imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo na kupongeza juhudi hizo zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa na vyama husika.
“Kamati Kuu inapenda kueleza imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda kwa wajumbe wachache waliosusia Bunge Maalumu la Katiba, kurejea bungeni na kumalizia sehemu ya mchakato uliobakia. Kamati Kuu inayatakia kila la kheri mazungumzo hayo,” alisema.MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment