FANYA FUJO UONE KARAHA YAKE KUTOKA KWA ASKARI WA JESHI LA POLISI KATIKA SIKUKUU YA IDD EL FITR.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Makao Makuu,jijini Dar es Salaam, Advera Senso.
Jeshi la Polisi nchini limesema limeimarisha ulinzi katika maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu katika kipindi cha Sikukuu ya Iddi El Fitr, hasa sehemu za kuabudia na kumbi za starehe.
Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alisema hayo katika taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana.
Alisema uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hiki cha sikukuu kama mwanya wa kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko ya watu.
“Jeshi la Polisi linapenda kuwaondoa hofu wananchi wote kuwa limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi kote nchini wanasherehekea sikukuu hii kwa amani na utulivu,” alisema Senso.
Alisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote yatakayokuwa na mikusanyiko ya watu.
Senso alisema katika kuhakikisha usalama katika kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wake.
Aliwataka wazazi kuwa makini na watoto wao, hasa disko toto ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.
Aliwatahadharisha watumiaji barabara kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment