WARAKA WA SIRI WAZUA MTIFUANO JIJINI DAR ES SALAAM.
Wazungumzaji wakuu kwenye mdahalo wa Rasimu ya Katiba mpya uliopewa jina la Nani anakwamisha kupatikana Katiba mpya,? Prof. Ibrahim Lipumba (kushoto), Stephen Wasira (katikati) na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni Mwanasheria, Tundu Lissu (kulia), wakiwa mbele ya hadhira kwenye ukumbi ulikofanyika mdahalo huo, jijini Dar es Salaam jana.
Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiwa katika hati hati ya kuanza, waraka unaodaiwa kuandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ukitathmini mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba umetajwa kuwa moja ya kielelezo cha chama hicho kuchakachua mchakato wa katiba mpya nchini.
Kwa nyakati tofauti jana wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliurejea waraka huo kama moja ya mbinu ya kuendelea kuwahonga wajumbe wa kundi la 201 wa Bunge hilo kwa kuwa CCM wanataka rasimu yao ya Katiba ipitishwe na siyo iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Waraka huo ambao kwa mara ya kwanza ulitolewa hadharani na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, Julai 15, mwaka huu pamoja na mambo mengine unadai:
“Uwekwe utaratibu maalum wa namna ya kuendeleza ushirikiano mzuri na wajumbe wa kundi la 201 wakati huu wa Bunge la Bajeti, ili Bunge maalum litakaporejea tena waendelee kuziunga mkono hoja za Chama Cha Mapinduzi (CCM),”
Jana Dk. Slaa alisema waraka huo wa siri ulioandaliwa na CCM unaolenga kuwashawishi wajumbe wanaotoka kundi la 201 kukiunga mkono chama hicho.
Kadhalika, waraka huo unalenga kuwashawishi Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhakikisha wanaripoti habari zinazoegemea upande wa chama tawala.
Dk. Slaa ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Vijana wa Chadema (Chaso) jijini Dar es Salaam, alisema waraka huo unataka makundi hayo yasimame upande wa CCM ili kuhakikisha msimamo wao wa muundo wa serikali mbili unafanikiwa na kupitishwa katika Bunge Maalum la katiba kabla Rasimu ya Katiba ya kupelekwa kwa wananchi.
“Watu hawaelewi sababu za Ukawa kutoka nje ya Bunge na ndiyo maana wanasema warudi warudi, sababu ya wao kutoka bungeni ni kutokana na kukiukwa kwa misingi ya Rasimu ya Katiba,” alisema.
Alisema Ukawa watakuwa tayari kurudi katika Bunge la Katiba linalotarajia kuanza Agosti 5, mwaka huu iwapo CCM itakubali kujadiliwa kwa Rasimu ya Katiba yenye maoni ya wananchi.
“Nina waraka ulioandaliwa na CCM ambao utapelekwa kwa Rais na umeweka mikakati ya kuwashawishi wajumbe wa kundi la 201 na moja ni kuwaunga mkono pamoja na wahariri wa vyombo vya habari, ili kufanikisha mipango yao ya serikali mbili kabla ya kwenda kwa wananchi,”alisema.
Aliongeza kuwa waraka huo unaeleza namna CCM walivyoapa kuhakikisha mpango wao wa kutaka muundo wa serikali mbili unafanikiwa.
Kwake Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, akizungumza katika mdahalo wa ‘Nani anataka kuwazuia Watanzania kupata katiba mpya jijini Dar es Salaam’ na kurushwa na kituo cha ITV, alisema waraka huo unaeleza kuwa na changamoto katika kupata theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Visiwani na Tanzania Bara.
“Akina Sheikh Jongo (Thabit Norman) na Jongo mwenzake (Hamid Masoud), Askofu Muhagachi (Amos), Askofu Mtetemela (Donald) na Mchungaji Mgimwa wapo 166 wote hawa ni wana CCM na wameteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, wanaitwa kwa Waziri Mkuu, kwa mawaziri wanapewa hela, wanapewa chakula, vinywaji maana yake …” alisema.
Lissu alisema kuwalazimisha Ukawa kurejea katika Bunge Maalum la Katiba maana yake ni kwenda kubariki uchafu huo unaotaka kufanywa na CCM na wajumbe wake.
Alisema Ukawa wanataka katiba mpya ambayo Rasimu yake ipo mezani, lakini wanaojiita watawala wanataka katiba ya sasa kwa jina jipya kwa kuipaka rangi. “Ndiyo maana wanapendekeza mambo hayo ili mambo yawe yaleyale ya ki-CCM,” alisema.
Alisema Ukawa wakirudi katika Bunge Maalum la Katiba ni kwenda kutumia bure Sh. bilioni 20.
“Leo hii muulizeni Wasira (Steven), Rais wa Zanzibar anapigiwa mizinga 21 wakati hiyo ni kwa ajili ya Mkuu wa Nchi, kwa katiba ya Zanzibar ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Zanzibar ni Mkuu wa Nchi ya Zanzibar sasa tukiendelea na mambo ambayo yalipendekezwa na Wasira na chama chake, tunaelekea wapi?”alihoji.
WASIRA TUNA THELUTHI MBILI
Wasira akijibu hoja hizo za Lissu alisema suala la kupata theluthi mbili, wajumbe wanaotoka Tanzania Bara wapo 412, baada ya Ukawa kutoka idadi iliyobaki ni 346 na kanuni inasema wakiwapo wajumbe zaidi ya nusu bunge linaendelea.
Theluthi mbili ya wajumbe wote wanaotakiwa kupiga kura na katiba ipatikane ni 275, kwa hiyo ukitaka kupata katiba ambayo haina maridhiano inatakiwa iwe hivyo, lakini CCM inataka katiba yenye maridhiano.
Zanzibar wajumbe wote waliopo katika Bunge Maalum la Katiba ni 213 na walipotoka wanaounga Ukawa waliobaki ni 148 na sheria inasema ili theluthi mbili iweze kupatikana inatakiwa wajumbe kutoka Zanzibar wawe 145 .
Wasira alisema pamoja na takwimu hizo bado CCM imetaka maridhiano yafanyike kwa kuwaomba Ukawa warudi bungeni ili mambo wanayotaka yakazungumzwe na kufikia mwafaka wa kupata katiba mpya.
“Kama unaitwa ukazungumze unakataa halafu unakuja na uongo nyie ndiyo mnazuia katiba kwa kukataa kuzungumza, hayo masuala ya Rais wa Zanzibar na mizinga waje Dodoma tukayazungumze,” alisema.
Naye Prof. Ibrahim Lipumba alisema kama CCM haitachakachua kamwe theluthi mbili za Zanzibar haziwezi kupatikana, ila akaonya kama chama hicho kinataka kuchakachukua kiendelee na mpango huo.
Alisema inashangaza kuona kuwa baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kumaliza kazi yake na kukabidhi Rasimu, tovuti iliyokuwa na maoni ya wananchi imefungwa kitu ambacho kinaonyesha kuna agenda ya siri katika suala hilo.
Prof. Lipumba alisema habari ya kudharau maoni ya wananchi waliopendekeza muundo wa serikali tatu ni kuipeleka nchi kubaya kwani Tume ya Jaji Warioba ilifanya kazi kubwa.
“Wito wangu ni kwa mtani wangu Rais Kikwete, ndiye aliyeanzisha mchakato huu alifanya makosa kutoa maoni ambayo ni ya chama chake, na kama ananisikiliza atumie siku za mwisho za mwezi wa Ramadhani kumuomba ajirudi,” alisema. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment