JK AUNGWA MKONO NA AHAMADIYA YA KUWA BUNGE MAALUM LA KATIBA LIMEKUMBWA NA MAPEPO.
RAIS KIKWETE.
Viongozi wa dini mkoani hapa wameunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa Bunge Maalum la Katiba limekumbwa na mapepo yanayokusudia kukwamisha upatikanaji wa Katiba mpya ya Tanzania.
Kiongozi wa Jumuiya ya Ahamadiyya katika Mikoa ya Singida na Dodoma, Bashart ur Rehman Butt, alilieleza NIPASHE jana kuwa wananchi wanatakiwa kuungana kuombea kazi hiyo huku wanasiasa wakitakiwa kufikia mwafaka utakaoliwezesha taifa kupata Katiba Mpya.
Alisema ikiwa Rais Kikwete aliyeasisi mchakato huo wa kulipatia taifa Katiba Mpya, ametamka hadharani kuwa kinachokabili Bunge hilo ni mapepo kuna kila sababu kwa jamii yenye kuamini katika maombi kutekeleza jukumu lao.
“Mtu mzima mwenye mke au mume na watoto na hata kama hajaoa au kuolewa ana wazazi, ndugu na jamaa zake wanaomfahamu kuonekana hadharani akitoa lugha za kukera wenzake, yakiwamo matusi ni dhahiri mapepo yapo kazini,” alisema Rehman Butt.
Alisema wananchi walifikia hatua ya kudharau Bunge hilo na ikaonekana hapakuwa na hofu ya Mungu miongoni mwa wajumbe wake waliopewa dhamana ya kujadili suala hilo nyeti la kihistoria.
Alisema jambo la msingi, pamoja na maombi pande mbili zilizotokana na Bunge hilo zisikilizwe na madai yenye mantiki yafanyiwe kazi ili kuokoa jahazi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma, Askofu Dk. Eliah Mauza aliliambia NIPASHE kuwa kauli hiyo ya Rais Kikwete imeonyesha dalili tofauti matarajio ya wengi waliodhani mchakato huo unaweza kuendelea bila wajumbe waliosusia vikao vya Bunge hilo kurejea bungeni.
Dk. Mauza aliihakikishia Serikali kuwa viongozi wa dini wanaendelea kuliombea Bunge hilo kukomesha mapepo huku wananchi wakielezwa kuwa watarajie kupata majibu ya mapendekezo yao katika Katiba ijayo.
Aliongeza kuwa pamoja na viongozi hao wa dini kuombea Bunge hilo, wanaendelea na maombi dhidi ya mapepo mengine yanayokera Watanzania.
Alitoa wito kwa Rais Kikwete kutambua kuwa afahamu kuwa hata ndani ya serikali kuna maovu mengi yanayohitaji maombi.
“Kuna baadhi ya wizara zinanyooshewa kidole kwa kuendekeza matendo yasiyofaa ambayo ni kiini cha maendeleo ya taifa kukwama, hayo nayo ni mapepo na tunaendelea kuyaombea,” alisema.
Wiki iliyopita Rais Kikwete akiwa kwenye maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 75 tangu kuanzishwa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) mkoani Mbeya aliwaomba viongozi wa dini nchini kuombea Bunge hilo ili liondokewe na mapepo aliyosema yanasababisha vyama vinne vya siasa kuvurugana na kutishia mchakato wa Katiba Mpya. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment