
BAADHI ya wanawake walioolewa na wale wanaoishi kinyumba wakiwa wakazi wa mji wa Sumbawanga, wameshukuru fainali za Kombe la Dunia zinaelekea ukingoni. Ujerumani na Argentina watapambana katika mchezo wa fainali Jumapili.
Furaha ya wanawake hao imekuja baada ya kukerwa na fainali hizo tangu zilipoanza wakidai kuwa wenzi wao hawaonekani nyumbani nyakati za usiku, kwa madai ya kufuatilia mechi za kombe hilo la dunia.
Utafiti uliofanywa na gazeti hili katika viunga vya mji huo, unaonesha kwamba baadhi ya wanawake wamekerwa na michuano hiyo, wakidai imesababisha kwa kiasi kikubwa wenza wao kurudi nyumbani usiku wa manane wakifuatilia mashindano hayo.
“Mie sipendi kabisa kusikia lolote linalohusu fainali za Kombe la Dunia amani imetoweka kabisa ndani ya ndoa yetu … napunjika sana kwa mumewe wangu, sasa ameanza kukesha nje ya nyumba yetu kwa kisingizio eti anafuatilia michuano hiyo,” alisema mmoja wa wanawake hao.
Mkazi wa Sumbawanga mjini, Maria Mkosamali, yeye anakiri bila ya kuwa fainali hizo licha ya kufikia sasa ukingoni zimesababisha baadhi ya wanaume kuwasaliti wake zao.
“Mie sifurahii chochote kile katika michuano hii, kwa kuwa furaha niliyokuwa nayo baada ya kuolewa miezi saba iliyopita, imeyeyushwa kabisa na kombe hili kwangu niwe mkweli ni nuksi kabisa ….. sasa nimekuwa nakesha macho meupee usingizi sipati roho yangu juu nikimsubiri mume wangu arejee kutoka kwenye majumba ya starehe anapoangalia michuano hii,” alisema.
“Niwe mkweli sasa maji yamezidi unga siamini kabisa kama anakwenda huko nimeanza kuhisi anakwenda pahala pengine maana kombe hili sasa limekuwa ni kisingizio tu amepata sasa mwanya wa kutoka nje ya ndoa ….. ingawa sijawahi kumfumania lakini ujumbe mfupi wa maneno niusomao katika simu yake umenifanya nihisi hivyo,” alisema Maria.
Baadhi yao wanadai kuwa wanazo seti za televisheni nyumbani mwao ambapo wenza wao wangeweza kutazama fainali hizo lakini ukifika usiku huomba wakaangalie na rafiki zao ili ushabiki wa soka unoge.
"Fainali hizi hakika zinaniumiza kichwa sana kwani tangu fainali zianze hakuna siku mume wangu alirudi mapema nyumbani, siku zote anarudi usiku wa manane," alisema Anastazia Mangi.
Baadhi ya wanaume walijitetea kuwa, ushabiki wa soka uko kwenye damu zao hawawezi kufikiria mambo mengine mabaya pale wanapoenda kuangalia mpira na wenzao baa huku wakiburudika kwa kunywa bia.
“Mimi tangu fainali hizi zianze hadi hii leo sijatoka naangalia mpira nyumbani kwangu nikiwa na mke wangu na tuna ‘enjoy’ sana ….. bila shaka wale wenzangu wanaofuata Kombe la Dunia baa wana mambo yao tu yenye utata . …… sasa wanatarajia nini lazima wenza wao watalalamika tu,” alisema Saaid Halfani.HABARILEO

0 comments:
Post a Comment