Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Ilolangulu wakiimba nyimbo wakati wa hafla fupi ya upokeaji wa msaada wa vitabu vilivyotolewa kwa shule 17 zilizopo eneo la mradi wa vijiji vya Milenia mbola.
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, amesema elimu ya Tanzania ipo “hoi bin taaban” na ametaka ubuniwe mikakati thabiti ya kuinusuru ili ijibu mahitaji ya ajira ya sasa.
Alisema hayo wakati akiwa mgeni rasmi katika mkutano wa 25 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati wa kutathimini kazi za kanisa na zilizopangwa kufanywa katika kipindi hiki.
Mkutano huo pia unatarajiwa kumchagua mrithi wa kiti cha Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, kilichoachwa wazi baada ya kufariki dunia Askofu Dk. Thomas Laizer, mwaka mmoja na miezi mitano iliyopita.
Alisema mwaka 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alieleza kwa undani suala la maaduni watatu wa taifa kuwa ni umaskini, ujinga na maradhi.
“Leo hii Tanzania sisi ni akina nani tusiangalie elimu, lakini Mwalimu yeye alikwenda mbali zaidi na kuweka elimu ya kujitegemea ili iweze kujibu mahitaji ya Watanzania. Tunapaswa sana na kutafakari sana kuhusu kufikiria suala la elimu,” alisema.
Alisema maadui hao ndiyo kikwazo kwa maendeleo ya taifa na akasisitiza kuhusu elimu ya kujigemea.
“Sisi ni nani tusiangalie vipaumbele hivyo, sisi ni nani. Sasa hivi elimu yetu ipo hoi bin taaban…imeundiwa tume na tume na kwa bahati mbaya taarifa zake hazijawekwa wazi, sasa sijui tatizo ni tume au serikali bado haijatekeleza ripoti hizo,” alisema.
Alitoa mfano mwingine wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair, alipoulizwa kuhusu vipaumbele vyake, alitaja, “kipaumbele ya kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu.”
Alisema miaka 15 baada ya kumaliza awamu yake ya uongozi alipokuwa nchini Singapore nako huko aliulizwa iwapo bado vipaumbele vyake ni vile vile naye akasema ni elimu, elimu, elimu.
Akahoji: “Sasa sisi ni nani tusiangalie vipaumbele hivyo?”Alisema mmoja wa Marekani aliwahi kuwatafuta manguli wa elimu na kuwafungia maeneo fulani wakifanya utafiti na baadaye waliweza kutoka na mpango mkakati ulioweza kutekelezwa hali ambayo imeifanya elimu ya Marekani kuwa nzuri.
Akahoji: “Sasa sisi ni nani tusiangalie vipaumbele hivyo?”Alimpongeza pia Marehemu Askofu Dk. Laizer kuwa amefanya kazi kubwa ya kichungaji pamoja na kuweka kipaumbele katika elimu.
Alisema kwa mfano, marehemu Askofu Dk. Laizer, wakati wa uhai wake alikukuza elimu kwa ujenzi wa shule mbalimbali na akafanikisha upatikanaji wa kiwanja kikubwa wilayani Monduli ambacho kimepangwa kujengwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini.
Alisema hata Biblia Takatifu imesema, ‘mshike sana elimu usimwache aende zake.’
“Elimu yetu ni lazima izingatie ajira, kwa bahati nchi yetu sasa hivi ina gesi ya kutosha. Na mahali pazuri pa kuelekeza gesi ni kwenye elimu, elimu bora itakayozingatia mahitaji ya sasa, la sivyo, gesi hii inaweza kuwa laana kwetu.
“Sehemu kubwa ambayo inaweza kuajiri vijana, wakiwamo wasomi wa aina aina mbalimbali wa makundi tofauti ni kwenye viwanda na kilimo.
“Tunatakiwa kujenga viwanda vingi na hasa vya pamba, hivi vinatoa ajira kwa waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne, sita na hata vyuo vikuu,” alisema.
Alisema kwa mfano, serikali ya Misri, huwa inatoa mikopo kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu na huwa inawapatia matrekta na mashamba na baadaye wanafanikiwa kurejesha mikopo hayo.
“Tujenge viwanda hasa vya pamba (nguo) na fedha za gesi zipelekwe huko…sasa hivi tabaka la walio nacho na wasio nacho ni kubwa sana, tusipoliondoa hatutakuwa salama, tutakula nao sahani moja,” alionja.
Akiwa muumini wa kanisa hilo, Lowassa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, walitaka wajumbe wa mkutano huo kumchagua mtu ambaye watashirikiana naye katika uongozi wa kanisa na kufuata nyayo za marehemu Askofu Dk. Laizer.
Alipendekeza eneo ambapo mkutano huo ulikuwa ukifanyika, katika Shule ya Sekondari ya Peace House inayomilikiwa na kanisa hilo, ambalo Dk. Laizer alishiriki kwa namna kubwa kulipata, liitwe Dk Thomas Laizer kwa heshima yake.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongella, alisema alilipongeza kanisa hilo na kusema serikali inatambua mchango wake hususan katika eneo hilo.
“Kama jamii tumeguswa na mchango wa kanisa hili na hata kwa mtu mmoja mmoja naye pia ameguswa,” alisema.
Alipongeza marehemu Askofu Dk. Laizer kwa kazi nzuri aliyokuwa amefanya enzi za uhai wake na hata katika kipindi cha mwisho alipokuwa amelazwa kwa ugonjwa hakuacha kutoa maelekezo ya kuliongoza kanisa hilo.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Lowassa kuzungumzia umuhimu wa kutatua tatizo la ajili Tanzania kupitia ajira.
Lowassa anatajwa kuwa muasisi wa shule za kata ambazo zilipanua wigo wa elimu ya sekondari kwa watoto wengi wa Kitanzania. Awamu ya kwanza ya wanafunzi waliopita shule za kata wanahitimu vyo vikuu mwaka huu. CHANZO: NIPASHE
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment