MBINU YA KUREJESHA MABILIONI YA USWISI ENDAPO SERIKALI YA TANZANIA ITAHITAJI.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya akiteta jambo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika moja ya Vikao vya Bunge mjini Dodoma.
Dar/Uswisi. Kuna njia tatu ambazo Serikali ya Tanzania ikiamua kuzitumia inaweza kurejesha mabilioni ya fedha zake ambazo zimefichwa nchini Uswisi na kwingineko duniani, Mwananchi limebaini.
Uchunguzi ulifanywa na gazeti hili nchini Tanzania na Uswisi unaonyesha kuwa, Mosi, Serikali inaweza kuharakisha kurejesha fedha hizo ikiwa itatumia vyombo vyake vya dola kama vile mahakama kutaka maelezo na majina ya walioweka fedha katika nchi husika.
Pili Tanzania inaweza kupata fedha zake ikiwa itajiunga na Taasisi iitwayo Organization of Economic Cooperation (OECD), ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wanachama wake kurejesha fedha ambazo zimekuwa zikihamishwa kwa njia ya ukwepaji wa kodi (transfer pricing), na tatu ni kujiunga ‘Global Forum on Transparence and Exchange’.
Taarifa ya 2012 ya Benki Kuu ya Uswisi (SNB) iliripoti kuwapo kwa Sh314 bilioni kutoka Tanzania, lakini katika taarifa yake ya mwaka jana, 2013 kiasi hicho kiliripotiwa kupungua na kufikia Sh291 bilioni.
Dk Mark Herkenrath ambaye ni Ofisa Programu wa Taasisi ya Alliance Sud inayojishughulisha na harakati za kupinga uwekaji wa fedha haramu nchini Uswisi, alimwambia mwandishi wa gazeti hili nchini humo kuwa Tanzania inaweza kuwasiliana na Serikali ya Uswisi ikiwa inahitaji taarifa zozote kuhusu fedha zake zilizofichwa nchini humo.
“Kama kuna ombi la kimataifa na likakubaliwa na mamlaka ya Uswisi, taarifa zinaweza kutolewa. Serikali zinazodai kuibiwa fedha zinapaswa kuomba zenyewe taarifa ili zipewe, lakini katika uhalisia hili halitokei. Ni sawa na kumwomba mwizi ajitaje mwenyewe,” Herkenrath na kuongeza:
“Kwa mfano kama kuna uchunguzi Tanzania ambao unahusisha watu na ushahidi ukapatikana, Uswisi iko tayari kusaidia. Ni kwa fedha zilizopatikana kwa njia haramu tu.”
Mkuu wa kikosi kazi cha kurejesha fedha na mali cha Uswisi, Pascale Baeriwyl akizungumza na mwandishi wa Mwananchi mjini Bern, alisema Tanzania inaweza kurejesha fedha zake kama Serikali itakuwa na nia ya dhati ya kufanya hivyo.
“Hadi sasa Uswisi imesharudisha Dola za Marekani 1.8 bilioni kwenye nchi zilizotoka,” alisema Baeriwyl na kuongeza: “Zinaitwa fedha za watawala (potentate funds) ambazo huwekwa kwenye taasisi za nje za fedha. Uswisi inayo mikakati ya kuhakikisha kuwa fedha na mali haramu haziingizwi katika taasisi zake za fedha,” alisema.
Hata hivyo, Balozi Anne Lugon- Moulin ambaye ni mkuu wa kitengo kinachoshughulikia nchi zinazozungumza Kifaransa kusini mwa Jangwa la Sahara alisema, Uswisi peke yake haiwezekani kufanikisha urejeshwaji wa fedha kama Serikali ya Tanzania haitatoa ushirikiano wa kutosha.
“Uswisi peke yake haiwezi kufanikisha kazi hii kama Tanzania haitoi ushirikiano. Ndiyo maana tunafadhili taasisi zinazopambana na utoroshwaji wa fedha haramu na mashirika ya misaada ambayo pia yanafanya kazi Tanzania,” alisema Moulin.
Kupitia OECD
Balozi wa Uswisi nchini, Olivier Chave alisema njia kuu na rahisi ya kuiwezesha Tanzania kurejesha fedha zake ni kujiunga na Shirika la Uchumi na Maendeleo (OECD) linalotatua matatizo ya uchumi, jamii na utawala.
“Tunachoweza kuwasaidia, kwa kawaida ni ushirikiano wa kodi ambapo nchi zinakubaliana na sheria za kimataifa na makubaliano. Sheria hiyo na kanuni zinafanya kazi chini ya OECD),” alisema Chave.
Dk Herkenrath alisema urejeshaji wa fedha zilizofichwa Uswisi hutegemea njia zilizotumika katika utoroshaji.
“Kwa fedha halali lakini hazikupitia mkondo sahihi hiyo ni rahisi kwani inahitaji makubaliano ya nchi mbili tofauti. Hadi sasa hakuna nchi ya Afrika iliyofanya makubaliano na Uswisi katika masuala ya ukwepaji wa kodi.”
Hata hivyo, alisema kwa ufahamu wake ni kwamba kwa kiasi kikubwa fedha za Tanzania zilizofichwa nchini humo zimepatikana kwa njia haramu ikiwa pamoja na rushwa. OECD iliyoanzishwa mwaka 1960 hadi sasa ina wanachama 34, lakini hadi sasa hakuna nchi ya Afrika iliyojiunga.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akizungumza na gazeti hili jana alisema, “Kwetu sisi ikiwa taasisi yoyote inaweza kutusaidia kupata fedha ambazo zimefichwa huko, Serikali haina kipingamizi chochote cha kujiunga nayo.”
Hata hivyo, alisema hana uhakika iwapo mchakato wa kujinga na OECD umeanza. “Sina hakika sana na hilo ila ninavyofahamu kujiunga na taasisi zozote za kimataifa pia huwa kuna mambo mengi ya kuangalia, kama vile masharti yake, viwango vya ada maana siyo vizuri kujiunga na taasisi kama hizi halafu mkashindwa hata kulipa ada zinazotakiwa.”
Akizungumza katika mkutano na wahariri, Meneja wa Kitengo cha Kodi za Kimataifa cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Bajungu alisema OECD ni taasisi inayozisaidia nchi nyingi za Ulaya kukabiliana na ukwepaji wa kodi.
Mmoja wa maofisa waandamizi katika Wizara ya Fedha ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema ikiwa Tanzania inataka kufanikiwa katika vita dhidi ya rushwa hasa utoroshaji wa fedha nje lazima iweke wazi taarifa zote za walipa kodi wakubwa.
“Lazima tujiunge na ‘Global Forum on Transparence and Exchange’. Huko taarifa zote za walipa kodi zinawekwa wazi. Ila Serikali yetu bado inasuasua, tumeshaishauri sana wizara lakini kuna urasimu fulani,” alisema.
Hatua za Serikali
Tayari Tanzania imeomba msaada kwa taasisi iitwayo International Centre for Asset Recovery (ICAR) (Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji wa Mali) ya Uswisi kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo.
Hata hivyo, viongozi wa Serikali wakiongozozwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekuwa wagumu kuzungumzia maendeleo ya uchunguzi huo, kwa maelezo kwamba ukikamilika utakuwa wazi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema aliwahi kukiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya uchunguzi huo lakini akakataa kutaja watu na kampuni zinazofanyiwa uchunguzi.
“Hatuwezi kutaja majina ya watu waliofunguliwa kesi kwa sababu kwanza tutakuwa tumeingilia haki zao kisheria. Pia, tunaweza kuwataja lakini baadaye ikabainika kuwa siyo kweli bali ni tuhuma tu na wakaja kutushtaki na tatu, tutakapowataja watu hao tuliowafungulia kesi tutaharibu upelelezi wetu.”MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment