NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NAMNA ANAVYONG'ANG'ANIA KUWANIA URAIS 2015 NDANI YA CCM.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema hatakatishwa tamaa na hatorudi nyuma katika harakati zake anazoziita za fikra mpya na mawazo mapya za kushika dola na kwamba wazee wakae kando.
Hata hivyo, Makamba ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli (CCM) amewashukuru watu wanaozungumzia nia yake ya kuwania urais mwaka 2015 na kutengeneza mjadala unaoendelea nchini, jambo ambalo alisema linaashiria kuwa dhamira yake imeeleweka.
Akiwa London nchini Uingereza mapema mwezi huu, Makamba alitangaza nia hiyo na kusema amefikia uamuzi huo kwa asilimia 90 lakini bado asilimia 10 katika baadhi ya mambo anayoendelea kuyatafakari, yakiwamo ya kuzungumza na makundi mbalimbali ya wazee, viongozi wa dini na viongozi waliopita ili apate ushauri wao kuhusu namna ya kufanya jambo hilo.
Julai 9, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete, ambaye anamzidi januari kwa miaka 24, alisema kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Soni, Bumbuli mkoani Tanga kuwa Makamba anataka mambo makubwa, lakini hajamshirikisha.
Rais Kikwete alimtaka Makamba “asilazimishe” kwa kuwa wakati ukifika atapata kile anachokitaka. “Mie hajaniambia na mie nasikia,” alisema Kikwete.
Akizungumzia na gazeti hili jana kuhusu kauli ya Rais Kikwete, Makamba alisema: “Ni kweli sijamwambia. Siku itakapofika yeye ni mwamuzi na mwenyekiti wa chama hivyo nitamweleza. Sitaki kumkwaza kwani na yeye ni wale waliopo katika kundi la asilimia kumi,” alisema.
“Zama za kizazi kipya za kutatua changamoto kwa kipindi cha miaka 30 hadi 50 ijayo zimewadia. Nitahakikisha mabadiliko ya haraka katika ardhi ya Tanzania kwani inawezekana rasilimali za kutosha zipo kilichobaki ni kuweka nidhamu katika nyanja zote.”
Aliwashangaa wanaombeza akisema kuwa hawamkatishi tamaa kwa hilo.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment