Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Dar es Salaam.
Wakati Serikali ikiahidi kuongeza nguvu vita dhidi ya watu wanaoharibu maliasili za taifa, utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa baadhi ya mawaziri, wabunge na madiwani wanahujumu nchi kwa kufanya biashara ya mazao ya misitu nchini.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa mawaziri wanafanya biashara hiyo kwa asilimia 39, watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama asilimia 61, maofisa misitu asilimia 43, wabunge asilimia 23, madiwani asilimia 72 na wakurugenzi watendaji kwa asilimia 25.
Ripoti ya Kitengo cha Udhibiti na Utafiti katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iliyotolewa hivi karibuni na kuwekwa kwenye tovuti, inasema kuwa mawaziri wanajihusisha zaidi na biashara ya magogo na mbao kwa asilimia 12.5, mkaa asilimia 6.3, milango na madirisha asilimia 5.1 na vinyago asilimia 2.1.
Wabunge wanafanya biashara ya magogo kwa asilimia 2.1, mbao asilimia 8.3, mkaa asilimia 8.2, milango na madirisha asilimia 2.1 na vinyago asilimia 2.2. Madiwani na asilimia zao kwenye mabano kama ifuatavyo, magogo (2.1), mbao (16.7), mkaa (33.3), milango na madirisha (16.7) na vinyago (2.3).
Wakurugenzi watendaji wanafanya biashara ya magogo kwa asilimia 3.5, mbao asilimia 8.3, mkaa asilimia 4.2, milango na madirisha asilimia 6.3 na vinyago kwa asilimia 2.1.
“Imeelezwa na waliohojiwa kuwa baadhi ya askari polisi wasio na maadili wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na kuwaachia watuhumiwa badala ya kuwakamata na kuwakabidhi kwa maofisa misitu kwa hatua za kisheria au kuwafikisha mahakamani,” inaeleza ripoti hiyo.
Ripoti hiyo iliyowahoji watu 776 katika mikoa 10 ya Tanzania Bara, inaeleza kuwa pamoja na kwamba sheria ya misitu haijakataza wanasiasa, watumishi wa sekta ya misitu na watumishi wengine wa umma kushiriki katika biashara ya mazao ya misitu, ushiriki wao unasababisha migongano ya kimaslahi huku rushwa ikishika asilimia 63.4.
Pia, inaeleza kuwa upungufu mkubwa wa watumishi na vitendea kazi katika sekta ya misitu umeathiri usimamizi endelevu wa rasilimali ya misitu nchini huku asilimia 82 ya watu waliohojiwa walisema uvunaji haramu wa mazao ya misitu unachochea biashara hiyo.
Vilevile, imebainika kuwa asilimia 71.9 ya misitu inavunwa bila vibali, huku maeneo yasiyoruhusiwa ni asilimia 70.3, uvunaji wa miti isiyokomaa asilimia 73.4 na miti inayozidi kiasi kilichopangwa kuvunwa asilimia 67.2.
Mikoa ya Kigoma, Pwani, Ruvuma na Tabora imetajwa kukithiri wa uvunaji haramu wa misitu ya asili. Asilimia 73.7 ya mazao ya misitu yamesafirishwa kwa njia za panya na matumizi ya kibali kimoja cha kusafirishia zaidi ya mara moja kwa asilimia 64.4.
Utafiti huo unaeleza kuwa asilimia 56 ya mazao ya misitu husafirishwa ndani au nje ya nchi. Kutokana na sababu hizo, inakadiriwa kuwa, nchi inapoteza hekta 403,000 kila mwaka.
Mikoa 10 iliyofanyiwa utafiti ilikidhi vigezo vya uwepo wa misitu ya asili na misitu ya miti ya kupandwa katika mashamba ya Serikali kwa wingi ukilinganishwa na mikoa mingine. Mikoa inayoongoza kwa usafirishaji wa mazao ya misitu kinyume na sheria ni Kigoma, Pwani, Ruvuma na Lindi.
Waziri azungumza.
Akizungumzia ripoti hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema viongozi wanaojihusisha na biashara hiyo wanajiingiza kwenye mgogoro wa kimaslahi, jambo linalowafanya washindwe kuwajibika ipasavyo.
Alisema zipo sheria na taratibu zitakazotumika iwapo watendaji hao watabainika kufanya makosa.
“Ripoti ya Takukuru itakuwa sahihi kwa sababu wao ni wataalamu. Sikatai kuwa wapo wanaoweza kuwa wamehusika, kama wamekiuka kanuni na taratibu za kazi watachukuliwa hatua,” alisema.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Ester Bulaya alisema hivi sasa dunia inazungumzia kupunguza uharibifu wa mazingira kwa kuhifadhi misitu, kwa hiyo ni jambo la kushangaza kusikia kundi fulani la viongozi linaongoza kwa kufanyabiashara ya mkaa.
Pia, alisema wananchi wanaposikia viongozi wao wanajihusisha na biashara, hata kama ni halali wanajiona wanyonge kwa sababu wanaamini madaraka yanatumika kufanikisha shughuli hiyo.
Mfanyabiashara wa mkaa katika Mtaa wa Bojonga, Kijichi, Mwanahamisi Kondo alisema ripoti hiyo inatoa majibu ya maswali ambayo wananchi wamekuwa wakijiuliza kwa nini kuna watu wanasafirisha mkaa bila ya vibali na hakuna kiongozi anayewasumbua.
“Kuna msimu ambao vibali vyote vya kusafirisha mkaa hufungwa, lakini kitu cha kushangaza utakuta wenzetu wanaendelea na biashara wakati sisi tumezuiwa. Hii inaonyesha kuwa wakubwa wanahusika,” alisema.MWANANCHI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / UTAFITI WAFICHUA MTANDAO WA WIZI UNAOFANYWA NA MAWAZIRI, WABUNGE NA MADIWANI KWA KUHUJUMU MALIASILI YA TANZANIA, WAZIRI NYALANDU ANAJISUMBUA ?.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment