VIONGOZI WA UKAWA WAMGOMEA MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA SAMWEL SITTA.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa,Profesa Ibrahim Lipumba.
Wakati Kamati ya Mashauriano ya Bunge Maalumu la Katiba ikitarajiwa kuanza vikao vyake jijini Dar es Salaam leo, wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walioteuliwa kuunda kamati hiyo wameshikilia msimamo wao kutoshiriki vikao hivyo.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, aliliambia NIPASHE jana kuwa hawatashiriki kwa kuwa vikao hivyo ni sehemu ya mwendelezo wa shughuli za Bunge hilo, ambalo walishalisusia kutokana na kukiuka misngi ya rasimu ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Profesa Lipumba alisema hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakijawahakikishia kama kiko tayari kuheshimu misingi ya rasimu ya serikali tatu, ambayo ndiyo maoni ya wananchi.
Alisema hata barua waliyopewa ya ushiriki inaonyesha kuwa kamati hiyo ni kwa ajili ya shughuli za Bunge hilo, ambalo wao haliwahusu.
“Kamati ni sehemu ya Bunge Maalumu la Katiba. Hata barua inaeleza hivyo. Na sisi Ukawa tulishatoka katika masuala ya Bunge hilo kutokana na kukiukwa kwa misingi ya rasimu yenye maoni ya wananchi. Hivyo, hatuwezi kushiriki katika kikao hicho,” alisema Profesa Lipumba.
Aliongeza: “Hata CCM haijatuhakikishia kama wako tayari kuheshimu misingi ya rasimu yenye maoni ya wananchi, ambayo ni serikali tatu. Ukishayaondoa inakuwa haina maana ya kujadili rasimu.”
Msimamo huo uliungwa mkono na Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, ambaye alipoulizwa na NIPASHE jana, alijibu kwa ufupi kuwa: “Hatutashiriki.”
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kwa kushirikiana na Makamu wake, Samia Hassan Suluhu, Julai 14, mwaka huu, waliteua wajumbe 30 wa Bunge hilo kuunda kamati hiyo, wakiwamo wajumbe wa Ukawa.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis, Julai 14, mwaka huu, ilieleza kuwa uteuzi huo ulifanywa chini ya masharti ya kanuni ya 54 (4) na (5) ya kanuni za Bunge hilo za Mwaka 2014.
Ilieleza kuwa lengo ni kutathmini kazi ya Bunge hilo iliyokwishafanyika awali pamoja na kuangalia mbele namna ya kumalizia kazi ya bunge hilo waliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya Watanzania. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment