CCM YAICHIMBIA MKWARA SERIKALI, YAITAKA KUFUTA VIBALI VYOTE VYA UVUNAJI MBAO MSITU WA SAO HILL IRINGA.
Iringa.
Chama cha Mapinduzi mkoani hapa kimeitaka Serikali kufuta vibali vyote vya uvunaji mbao vilivyotolewa katika msitu wa Sao hill uliopo wilayani Mufindi kutokana na madai kuwa vilitolewa kwa upendeleo.
Mwenyekiti wa chama hicho mkoani hapa, Jesca Msambatavangu aliliambia gazeti hili jana kuwa hatua hiyo ndiyo pekee itakayowatendea haki wakazi wa Wilaya ya Mufindi ambao kwa muda wote wamekuwa watunzaji wakuu wa rasimali hiyo muhimu kwa uchumi wao na taifa kwa jumla.
Msambatavangu alifafanua kuwa katika kikao cha Halmshauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Iringa wajumbe wa mkutano huo walikubaliana kwa kauli moja na kumtaka Waziri mwenye dhamana Lazaro Nyalandu kufuta vibali hivyo kwa madai mazingira yake yamezungukwa na rushwa.
“Wananchi wa Mufindi wametueleza kuwa vibali vimetolewa kwa misingi ya ukabila, upendeleo na rushwa na watu waliopata vibali walilazimika kutoa rushwa ya Sh3 milioni, wametuambia hivyo na Serikali ina macho tunaomba ifuatilie suala hili,” alisema.
Jesca alifafanua kuwa chama hicho kimewasikiliza wananchi wa Mufindi na kuona hoja zao ni za msingi kwani wameeleza mambo mengi, yakiwamo utoaji wa vibali kwa msingi wa ukabila na upendeleo.
“Msitu ule uko Mufindi, wananchi ndiyo waliotoa maeneo kupanda miti na ndiyo walinzi wakuu wa rasimali ile, kwanini wasipatiwe upendeleo na kunufaika,” alihoji .
Alisema mwaka jana, Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakati ule, Balozi Hamisi Kagasheki alifuta vibali vyote na kuamuru vitolewe upya na kuongeza kuwa hilo litaondoa manung’uniko na kuwajengea imani wananchi kuwa Serikali yao inawajali na kusikiliza kero zao.
0 comments:
Post a Comment