Wabunge wakiwa ndani ya bunge maalumu la katiba mjini Dodoma, Tanzania.
WAKATI Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akiwataka wanasiasa nchini kuacha kuchezea Muungano, Jukwaa la Katiba limesema limefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Bunge hilo kwa sasa.
Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, alisema juzi mjini Dodoma kuwa walipata tabu sana kuamini kama Bunge hilo lingeweza kuendelea kutokana na mvutano uliopo na kundi la Ukawa, lakini kutokana na maelezo waliyoyapata kutoka kwa wajumbe na baadhi ya wenyeviti wa Kamati, ni dhahiri kazi hii itafanikiwa.
Kibamba alibainisha hayo wakati Ujumbe wa Bodi ya Jukwaa la Katiba, likiongozwa na Mwenyekiti huyo, ulipofika ofisini kwake kwa lengo la kujua hatua ambayo Bunge hilo limefika katika kutengeneza katiba hiyo na mwenendo mzima kwa ujumla Kibamba alishauri kuwepo kwa mazingira ya kuvumiliana kwa kila pande zinazovutana ili kunusuru jamii inayowazunguka kuathirika na mivutano hiyo kwa kuwa nao wanaibeba kama ilivyo.
“Tunaomba sana muendelee kuwa na uvumilivu katika mchakato huu wa kutunga katiba, mnapogombana nyie ndani ya Bunge hili na wananchi nao wanajigawa katika makundi hayo na pia wao wanagombana kutoka na tofauti za itikadi zenu. Hii inatupa shida hata sisi kuendelea kutoa elimu kuhusu katiba kwa sababu na Taifa nalo linajigawa,” alisema Kibamba.
Alishauri wajumbe kutoka Kundi la Ukawa na CCM kuvumiliana na kumaliza tofauti zao ili wananchi wapate Katiba yao mapema kuliko kuendelea kukosa uvumilivu katiba baadhi ya masuala ambayo kimsingi yanahitaji mazungumzo ili kuyatatua.
Awali, Sitta alisema Bunge Maalumu la Katiba limefanya mabadiliko madogo katika kanuni kwa lengo la kuziboresha zaidi ili ziweze kukidhi matakwa ya kisheria, hususani siku ambazo bunge hilo limeongezewa muda wake ili kukamilisha kazi yake.
Akitoa maelezo kuhusu aina ya Muungano unaohitajika katika Katiba mpya, Sitta alisema suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar sio suala la kisiasa tu, ni suala la damu.
Alisema makabila mengi ya bara na Zanzibar yamefanya kuoana tangu enzi hizo na hivi sasa kizazi kilichopo ni cha undugu zaidi, hivyo kuleta siasa kwenye suala la muungano wa aina hii ni kuhatarisha mahusiano ya watu hao.
“Agenda yetu sio suala la kuwa na serikali ngapi au muundo wa namna gani, bali ni kwa namna gani masuala yote yanayogusa wananchi moja kwa moja yanapatiwa ufumbuzi kupitia katiba hii mfano, wajibu, haki za raia na makundi mbalimbali, na kadhalika,” alisema.
Wakati Sitta akitoa kauli hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu amevitaka vyama vya upinzani kurejea Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, ambayo imebainisha wazi kuwa Rais Jakaya Kikwete, hawezi kulivunja au kuliahirisha Bunge la Katiba.
Pia mkurugenzi huyo amevitaka vyama hivyo vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuwasilisha hoja zinazohusu Katiba kwa Katibu Kiongozi, ili kusaidia upatikanaji wa Katiba mpya lakini wasitarajie kusimamishwa kwa mchakato kwani ni kinyume cha Sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema katika sheria hiyo ya Katiba haina sehemu yoyote inayotoa mwanya kwa Rais au mtu yeyote kusitisha Bunge hilo la Katiba.
“Msimamo wa Ikulu ni uleule hakuna mabadiliko, Bunge la Katiba halitositishwa litaendelea na shughuli zake kama kawaida,” alisisitiza Rweyemamu.
Alisema anashangazwa na umoja huo kwa kitendo chake cha kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete alivunje Bunge hilo linaloendelea na vikao vyake bungeni na kusahau kuwa wao wenyewe wamekuwa wakidai kuwa Rais huyo hana mamlaka ya kuingilia mchakato wa Katiba.
Akizungumzia mabadiliko ya Kanuni, Sitta alisema: “Tunashangaa baadhi ya watu kuanza kutusakama eti tumebadili kanuni kwa lengo la kuchakachua mchakato. Naomba ieleweke wazi kuwa tunafanya kazi kufuatana na matakwa ya kisheria, kanuni zilizofanyiwa marekebisho ni kwa lengo la kwenda na muda uliopo ili tuweze kutekeleza kazi yetu kwa muda uliotengwa.
Akielezea zaidi kazi iliyofanywa na Bunge Maalum wakati wa marekebisho ya Kanuni, Sitta alisema hivi sasa mabadiliko yaliyofanywa yanatoa fursa kwa Bunge hilo kumaliza muda wake ndani ya kipindi cha siku 60 walizoongezewa na Rais kwa mujibu wa Sheria tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Kimsingi kanuni hizo za zamani zilitoa fursa kwa mjadala kuwa mrefu zaidi, hususani kujadili sura moja baada ya nyingine.
Sitta amewahakikishia wajumbe hao kuwa sio kweli kuwa Bunge linajadili rasimu mbadala kama inavyoenezwa na baadhi ya watu huko nje.
Alisema kazi inayofanywa na Bunge hilo ni kuendelea kujadili Rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba na sio vinginevyo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa jukumu la kutunga katiba ni la Bunge maalumu na kazi hiyo inaendelea kama kawaida kulingana na matakwa ya kisheria yanavyoainisha Bunge hilo kufanya hivyo.
Awali akitoa taarifa kwa Ujumbe huo wa Jukwaa la Katiba, Sitta amesema anafurahishwa na mwenendo wa Kamati za Bunge Maalumu, ambapo kutokana na mabadiliko haya ya kanuni, hivi sasa kamati nyingi zinaendelea kujadili sura ya 2,3,4,5, na leo nyingine zinamalizia sura ya 7.
“Jana (juzi) wenyeviti wa kamati wamenipa taarifa ya hatua waliyofikia na wote wanaendelea kuichambua rasimu vizuri na mambo mengi wanakubaliana nayo isipokuwa sehemu chache kidogo ndio kuna mapendekezo mapya katika baadhi ya ibara.” alisema Sitta.
Sitta alisema wamefurahi rasimu iliyopo imetoa fursa kwa kutambulika kwa baadhi ya masuala kama vile haki za wakulima, wavuvi, na wafugaji hivyo katika ngazi ya kamati, mapendekezo hayo yanaendelea kuboreshwa ili kuwa na kila kundi kuwekewa mipaka yake vizuri.HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / siasa
/ BARAKA TELE !!!. JUKWAA LA KATIBA YAELEZA BUNGE MAALUMU LA KATIBA MPYA LITAFANIKIWA DODOMA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment